Wakulima waidai NFRA Sh63 bilioni

Dar es Salaam. Wakulima wa mahindi nchini Tanzania wamedai hawajalipwa Sh63 bilioni wanazodai kutoka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mazao waliyouza kati ya Julai na Novemba 2024.

Kwa mujibu wa NFRA, wakulima walikabidhi tani 429,000 za mahindi zenye thamani ya Sh305 bilioni katika awamu ya kwanza ya ununuzi.

Hata hivyo, ni Sh242 bilioni pekee zilizolipwa hadi sasa, hali iliyowaacha wakulima katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa mahindi wakiwa na masikitiko.

“Wengi wetu hatujalipwa kwa mazao tuliyouza Septemba. Hali hii imetuacha bila fedha za kujiandaa kwa msimu ujao wa kilimo,” amesema mkulima mmoja kutoka Songea, Mkoa wa Ruvuma, aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NFRA, Dk Andrew Komba amekiri kuhusu ucheleweshwaji wa malipo hayo, akihusisha tatizo hilo na changamoto za ukwasi zinazowakabili wakopeshaji wa shirika hilo.

“Ingawa tumetia saini mikataba na wakopeshaji kadhaa, changamoto zao za ukwasi zimetulazimisha kufanya malipo kwa awamu. Tunawalipa wakulima mara tu tunapopokea fedha,” amefafanua.

Dk Komba amesema malipo yatakuwa ya haraka wakati wa awamu ya pili ya ununuzi, inayotarajiwa kuanza Februari 15, 2025.

“Hali hii haitatokea wakati awamu ya pili itakapoanza Februari 15, 2025. Wakala utakuwa na fedha za kutosha kuwalipa wakulima baada ya kufanya biashara na wateja wetu: Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na Shirika la Chakula Duniani (WFP),” ameongeza.

Benki kadhaa zinazohusika zimeeleza kuwa ucheleweshwaji huo huenda umetokana na NFRA kuchelewa kuwasilisha maombi ya fedha.

“Kwa ninavyojua, hatuna maombi yoyote kutoka NFRA yanayosubiri kushughulikiwa. Tunashughulikia maombi yote haraka mara yanapowasilishwa,” amesema mfanyakazi mmoja wa benki ambaye hakutaka kutajwa.

Mkataba wa Dola450 milioni

Kwa msimu wa 2024/25, NFRA ina mkataba wa kusambaza tani milioni 1.25 za mahindi kwa Zambia, DRC, na WFP, zenye thamani ya dola milioni 450 (sawa na Sh1.17 trilioni).

Zambia imeshalipa kwa tani 195,000, kati ya hizo tani 40,000 zimeshawasilishwa. Hata hivyo, DRC haijalipa chochote kwa oda yake ya tani 500,000, huku WFP ikipokea tani 5,000 kati ya tani 35,000 walizoagiza.

Dk Komba amebainisha kuwa asilimia 74 ya ununuzi wa mahindi kwa mikataba hiyo umetekelezwa, huku NFRA ikiweka kipaumbele katika kutimiza ahadi zake kwa Zambia na WFP.

Dk Komba ametaja changamoto kadhaa zilizojitokeza katika awamu ya kwanza, ikiwamo uhaba wa maghala ya kuhifadhi mazao na ucheleweshwaji uliosababishwa na wakulima kusafisha na kupanga mahindi kwa mikono, ambayo yaliharibika kutokana na mvua.

Kukabiliana na changamoto hizi, NFRA imejenga hifadhi za muda, kuongeza mizani ya kidigitali kutoka 72 hadi 206 na inapanga kuanzisha teknolojia ya kisasa ya kusafisha mazao msimu ujao.

Hadi Novemba 2024, NFRA ilikuwa imenunua tani 429,000 za mahindi, tani 30,000 za mchele na hakuna ulezi kwa sababu ya uzalishaji mdogo katika maeneo yaliyolengwa.

Related Posts