WATATU WAFARIKI DUNIA KWA AJALI YA BARABARANI

WATU watatu wafariki dunia kwa Ajali ya gari ambayo imetokea Tarehe 27.11.2024 saa 12:30 jioni eneo la Mbembela Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Tunduma, Gari lori namba T.537 DNC na Tela namba T.241 ARG aina FAW iliyokuwa imepakia madini ya Sulphur ikitokea Dar es Salaam kuelekea Tunduma Mkoa wa Songwe ilipoteza uelekeo na kugonga magari sita, bajaji nne, Pikipiki moja.

Ajali hiyo kusababisha vifo vya watu watatu, wawili papo hapo na mmoja amefariki dunia leo Novemba 28, 2024 akiwa anaendelea na matibabu.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga – SACP imeeleza kuwa Magari yaliyohusika katika ajali hiyo ni T.199 DYF Toyota Coaster, SU 44682 Toyota Double Cabin mali ya Shirika la Posta Mbeya iliyokuwa ikiendeshwa na Fredy Mwasanga [48] mkazi wa Soweto, Gari T.134 DXK Toyota Double Cabin iliyokuwa ikiendeshwa na Lusekelo Mwaseba [48] mkazi wa Sae, Gari T.370 ABN Toyota Land Cruiser, Gari T.344 BTS Toyota Cresta na Gari T.474 EHL/t.449 EHL aina ya FAW iliyokuwa ikiendeshwa na Alon Ruben [50] mkazi wa Isanga.

Aidha, katika ajali hiyo Bajaji nne ziligongwa ambazo ni MC.446 DYK, MC.649 DWL, MC.138 DKC na MC.261 EBN na Pikipiki moja ambayo haijafahamika namba zake za usajili. Waliofariki katika ajali hiyo bado hawajatambulika, wawili jinsia ya kiume na mmoja jinsia ya kike. Majeruhi tisa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu Gari kwenye eneo lenye mteremko. Jitihada za kumtafuta Dereva kwa kushirikiana na mmiliki wa Gari zinaendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Related Posts