Wavuvi Ziwa Victoria watakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa

Geita. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mkoa wa Geita limewatahadharisha wadau wote wa vyombo vya usafiri na wavuvi wanaotumia Ziwa Victoria kufuatilia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari za majini hususan kipindi hiki chenye mvua nyingi na upepo.

Ofisa Mfawidhi wa Tasac Mkoa wa Geita, Godfrey Chegere ameyasema hayo juzi Novemba 26, 2024 wakati akitoa elimu ya usalama kwa kuzingatia sheria na kanuni za usafiri majini kwa abiria na wamiliki wa vyombo vya usafiri katika mwalo wa Makatani na ule wa abiria uliopo Kata ya Nkome Wilaya ya Geita.

Chegere amesema Desemba huambatana na mvua na upepo mkali, hivyo wamiliki wa vyombo na wale wanaoviendesha wanapaswa kuangalia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari.

“Wamiliki wote wa vyombo na wale viongozi wa mialo tumeunda kundi kwenye simu kwa ajili ya kupeana taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye kitengo chetu cha hali ya hewa kilichopo Mwanza, kabla ya kuanza safari fika kwenye ofisi za hawa viongozi wa mwalo, watakupa taarifa kama kuna upepo, nawasihi msiingie ziwani maana mawimbi yatakua makali,” amesema Chegere.

Katika hatua nyingine Chegere amewataka wamiliki wa vyombo vya majini kuzingatia sheria kwa kubeba abiria kwa idadi inayolingana na uwezo wa chombo hicho na kuepuka kubeba mizigo pamoja na abiria kwenye vyombo vya abiria.

“Chombo cha abiria kibaki kwa abiria na mizigo ibaki mizigo msibebe abiria na mizigo kwenye chombo kimoja hii ni hatari,” amesema Chegere.

Aidha, amewataka wavuvi na abiria kuhakikisha wakati wote wa safari wanavaa ‘life jacket’ na kuzingatia sheria za usalama katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ambapo idadi ya abiria huongezeka kwa kiasi kikubwa.

Akizungumzia ajali za majini, Chegere amesema utolewaji wa elimu ya usalama umesaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita ziliripotiwa ajali tano na toka mwaka huu uanze hakuna ajali iliyotokea.

Katibu tawala mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zinazotumika kuongoza vyombo hivyo huku akiwataka kuchukua tahadhari msimu huu wa sikukuu kwa kutobeba abiria zaidi ya uwezo wa chombo.

“Tasac fanyeni ukaguzi angalieni uzingatiaji wa sheria hasa kipindi hiki cha sikukuu ambacho wasafiri wanakuwa wengi hakikisheni kuna vifaa vya uokozi karibu na wapakie abiria kulingana na uwezo wa chombo,” amesema Gombati.

Baraka Pantaleo, mvuvi katika mwalo wa Makatani, amesema elimu inayotolewa na Tasac pamoja na kaguzi wanazofanya mara kwa mara imesaidia kuondoa vyombo vibovu majini na kusaidia wamiliki kununua ‘life jacket’ ambazo zimesaidia kupunguza ajali.

“Zamani ilikuwa mtumbwi ukizama kumpata mtu ni kazi na wakati mwingine mnamkuta ameshapoteza maisha lakini sasa hivi inakuwa rahisi ‘lifejacket’ inasaidia kumuona mtu mapema na kumuokoa,” amesema Pantaleo.

Amesema utaratibu wa utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwenye simu umesaidia wavuvi kutoingia ziwani wakati wa mvua kubwa na upepo na hivyo kuepuka vifo visivyo vya lazima vilivyokuwa vikitokea miaka ya nyuma kutokana na upepo mkali ziwani.

Related Posts