Mhe. Balozi Kombo ambaye ameshiriki Mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwenye wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Julai 2024, ameungana na Mawaziri wenzake wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda katika Jumuiya hiyo kupitia, kujadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali zinazolenga kuboresha utendaji wa Jumuiya kwa manufaa ya Nchi Wanachama ambazo zitawasilishwa kwenye Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 na 30 Novemba 2024 kwa ajili ya kuridhiwa.
Akichangia agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo, Mhe. Balozi Kombo amewahikishia ushirikiano Mawaziri wenzake kutoka kwake binafsi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla ambapo pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha Mawaziri hao Tanzania hususan Mkoa wa Arusha na kuwaomba kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Novemba 2024.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Deng Alor Kuol amewapongeza Mawaziri kwa kushiriki mkutano huo na kuwaomba kutoa michango yao chanya katika agenda zilizowasilishwa kwao kabla ya kuziwasilisha kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 29 na 30 Novemba 2024.
Miongoni mwa agenda zilizojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa ya utekelezaji wa program mbalimbali katika sekta za miundombinu, forodha na biashara, utalii na ajira; taarifa ya mwaka ya ukaguzi wa hesabu za jumuiya kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2024 na ripoti ya kamati ya utawala na fedha, pamoja na kupitia na kupitisha ratiba ya shughuli za Jumuiya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2025.
Kadhalika masuala mengine yaliyojadiliwa ni maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo ambayo yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 29 Novemba 2024.
Mkutano wa Mawaziri, ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama vilivyofanyika kuanzia tarehe 22 hadi 27 Novemba 2024.
Mbali na Mhe. Balozi Kombo ujumbe wa Tanzania pia uliwajumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samuel Shelukindo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Mhe. Elijah Mwandumbya, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Zanzibar, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Bw. Rashid Ali Salim na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Miongoni mwa majukumu ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ni kutunga sera za Jumuiya, kufuatilia na kufanya mapitio ya mara kwa mara juu ya utekelezaji wa program mbalimbali za Jumuiya kwa maslahi mapana ya Nchi Wanachama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi nane za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Somalia imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Mtangamano huo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.