ACT Wazalendo yataka uchaguzi serikali za mitaa urudiwe

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo, kimesema uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Jumatano Novemba 27,2024 haukuwa huru na haki na hivyo unapaswa kubatilishwa na kurudiwa upya.

Mbali na hilo, chama hicho kimesema hakikubaliani na  matokeo yaliyotangazwa na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa na kuwa mchakato huo ulivurugwa na kusababisha wananchi kuporwa haki yao.

“Msimamo wa ACT Wazalendo, tunataka uchaguzi huu ubatilishwe na uchaguzi mpya wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ufanyike baada ya kupata sheria mpya ya uchaguzi huo na Tume Huru ya Uchaguzi,” amesema Semu.

Juzi Jumatano Novemba 27, Waziri Mchengerwa alisema uchaguzi huo  uliohusisha vijiji 12,333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 ulikwenda vizuri kwa asilimia 98  na maeneo ya changamoto yaliyobainika na changamoto yaliongezewa muda.

Leo Ijumaa Novemba 28,2024, akitoa taarifa ya awali kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema mchakato huo ulighubikwa na kasoro kuanzia utungaji wa kanuni, uandikishaji wa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, upigaji wa kura na utoaji wa matokeo.

Semu amesema taarifa ya awali ya chama hicho imetokana na kikao cha dharura cha kamati ya uongozi kilichoketi jana Alhamisi Novemba 28, 2024 kilichofanya tathmini ya awali ya uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, Chama cha Mapinduzi (CCM), ndicho kimetangazwa kushinda viti vingi kwa asilimia 99.

“Mchaķato wa uchaguzi ulitawaliwa na matukio ya vitisho dhidi ya raia hasa wanaochukua fomu, ukamataji kutishwa ķwa mawaķala wetu, matumizi ya kura bandia. Viongozi na wanachama wetu waliojaribu kukabiliana na hujuma hizi walishughulikiwa kwa vipigo na kukamatwa,” amedai Semu.

Semu amesema ACT Wazalendo itafanya mawasiliano na vyama makini vya siasa na asasi muhimu za kiraia ili kuitisha kikao kwa ajili ya kupata mwafaka wa pamoja katika kupata ufumbuzi sitofahamu hiyo.

“Maeneo tunayotaka yafanyiwe kazi kwa pamoja na vyama na asasi makini ni mabadiliko ya Katiba ili kupata mpya, sheria za uchaguzi na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Sekretarieti Huru ya Tume ikiwa na wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na makarani wa uchaguzi,”.

“Yote haya yakamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. ACT Wazalendo tunakusanya taarifa ya matukio yote yaliyojitokeza tutatayarisha taarifa kamili ya chama,” amesema Semu.

Related Posts