Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Dar es Salaam, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Ayoub Mumba baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mtoto wake wa kambo, Amina Ayoub (7).
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana Januari 27, 2020, kwenye msitu unaomilikiwa na Jeshi, KJ-Pugu, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam huku ukiwa hauna sehemu zake za siri na macho na nguo yake ya ndani ikiwa kando.
Katika hukumu ya Novemba 25, 2024 aliyoitoa Jaji Butamo Philip na nakala yake kupatikana katika tovuti ya Mahakama, Ayoub amepewa adhabu hiyo baada ya mahakama kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka na kwenye maelezo ya onyo, Ayoub alikiri kutenda kosa hilo.
Ayoub ameshtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Januari 24, 2020 baada ya kuachwa nyumbani na mtoto huyo, ambaye siku ya tukio alionekana barabarani amemshika mkono.
Ilidaiwa mama wa marehemu aliporudi nyumbani siku hiyo hakukumkuta mwanaye na aliwaomba majirani zake wamsaidie kumtafuta, huku mumewe, Ayoub, akiwa haonyeshi ushirikiano, licha ya kuwa ndiye wa mwisho kuonekana na mtoto huyo.
Ilielezwa kuwa Ayoub alipoulizwa na wanafamilia na majirahi kuhusu mtoto huyo, aliwaambia wasiwe na wasiwasi kwa kuwa yuko hai na atarejea nyumbani, lakini baada ya kubanwa alidai mganga wake ndiye anajua mahali alipo.
Kutokana na maelezo hayo, mshtakiwa alikamatwa na alipohojiwa alikiri kumuua mtoto.
Uchunguzi wa vinasaba (DNA) ulifanyika sampuli zikikusanywa kutoka kwenye chupi ya marehemu na kwa mshtakiwa, vililingana na uchunguzi wa mwili huo ulibainisha mwili ulibaini alikufa kifo kisicho cha kawaida.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mawakili watatu wakiongozwa na Erick Kamala, huku mshtakiwa akiwakilishwa na Wakili Zidadi Mikidadi.
Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi tisa, huku mshtakiwa akiwa shahidi pekee wa utetezi.
Shahidi wa kwanza, SP Lwitiko Kibanda aliyekuwa Kamanda wa Polisi (OCD) Wilaya ya Ukonga, alieleza kuwa Januari 25, 2020 alipata taarifa ya kupotea kwa Amina na aliamuru askari aliyepeleka taarifa awaite wazazi wa mtoto huyo.
Alisema siku iliyofuata akiwa ofisini alimpokea Ayoub aliyepelekwa na watu kadhaa wakidai ndiye alikuwa wa mwisho kuonekaan na mtoto huyo na alivyompeleka mshtakiwa huyo katika Kituo cha Polisi cha Stakishari kwa ajili ya usalama wake.
Alidai baada ya hapo, alimhoji mshtakiwa naye akakiri kumuua mtoto huyo, akamtoa sehemu za siri na macho na kumnyoa nywele na aliendakuwaonyesha polisi mahali alipompeleka na kumuua na walipoenda waliukuta mwili huo.
Alidai nguo ya ndani ya marehemu ilikuwa kando yake na walimkuta akiwa amevaa blauzi tu na mama wa mtoto huyo ndiye alimtambua na mwili ukapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi.
Shahidi wa pili ambaye ni mama mzazi wa marehemu, Mwajuma Issa alisimulia ilivtyokuwa siku ya tukio na kuwa aliporudi nyyumbani alimkuta mtoto mmoja pekee na alipomuuliza alipo dada yake, alimjibu kuwa aliondoka na baba yao (Ayoub).
Alidai katika harakati za kumtafuta Amina, alikutana na kijana mmoja ambaye alimwambia kuwa alimuona Amina (marehemu) akiwa na mshtakiwa.
Baada ya kusikia hayo, alimpigia simu mshtakiwa, lakini hakuipokea na alipompigia kwa kutumia simu ya mwenye nyumba wao aliipokea na alipomuuliza alipo mtoto, mshtakiwa alisema wamsubiri nyumbani.
Alisema mshtakiwa alipofika nyumbani alimkuta mkewe akiwa na majirani waliokuwa n walipomuuliza alisema hakuondoka naye, hivyo waliendelea kumtafuta mtoto, kabla ya kwenda kuripoti kituo cha Polisi.
Alidai Januari 27, 2020, alipokuwa nyumbani, alisikia kelele kutoka eneo la msitu linalomilikiwa na jeshi naye alienda kuona kuna nini.
Alidai alipofika msituni, aliona watu wengi wakiwemo polisi, Ayoub na marehemu akiwa amelala chini chali na sehemu zake za siri zilikuwa zimetolewa.
Innocent Mosha, daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alidai ulikuwa umevimba na kuanza kuoza, ukiwa umetolewa macho na sehemu za siri, hivyo haikuwezekana kufahamu sababu za kifo, ila alibaini hakikuwa cha kawaida.
Shahidi wa tano ambaye ni askari wa JWTZ, MT 76576 SGT Amani Albert Tillya, alidai Januari 27, 2020 askari polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Stakishari walifika ofisini kwake na alipokea maombi yao ya kutaka kuingia msituni humo.
Alidai askari polisi hao waliokuwa wakiongozwa na Koplo Ernest, walisema wanatafuta mtoto aliyepotea na alipowauliza nani angewaongoza kwenye eneo la tukio, wakamtaja Ayoub, kisha akaongozana nao msituni.
Alisema waliingia msituni na kugawanyika makundi mawili na Ayoub alikuwa akiwaongoza na kuwa walitumia zaidi ya saa moja, kisha wakafika eneo la tukio ambapo watu walianza kupiga kelele na kulikuwa na harufu kali.
Katika eneo la tukio alisema aliona maiti ya mtoto wa kike aliyekuwa amenyolewa nywele, sehemu za siri zimetolewa na nguo yake ya ndani ilikuwa kando yake ikiwa imejaa damu.
Akijitetea mahakamani hapo, Ayoub alidai kuwa Januari 24, 2020 akiwa nyumbani na watoto wao (Amina na Subira) na alikuwa nao hadi mkewe aliporejea, kisha akaenda kwenye shughuli zake na baadaye mkewe alimpigia kumuuliza kama ameondoka na Amina, akamjibu hakuondoka naye.
Alidai ilibidi arudi nyumbani mara moja na kushirikiana na mkewe kumtafuta mtoto, kisha wakatoa taarifa polisi na siku inayofuata waliendelea kumtafuta mtoto huyo lakini baadaye alishangaa shemeji yake na watu wengine walifika kumhoji kuhusu alipo Amina.
Alidai alipokana kujua alipo mtoto huyo ukaibuka ugomvi wakisisitiza anatakiwa kuwaonyesha alipo Amina na kuwa walianza kumrushia mawe, naye akawaambia bora waende polisi.
Alidai alipopelekwa Kituo cha Polisi Stakishari, akituhumiwa kumuua mtoto wake wa kambo na Januari 26, 2020 alifahamishwa mtoto huyo alikutwa akiwa amefariki.
Alidai pia kuteswa na kulazimishwa kusaini karatasi ambayo ndani yake hakujua kilichokuwa kimeandikwa. Pia alikana kuwapeleka polisi na watu wengine msituni kwenye eneo la mauaji.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Philip alichambua ushahidi huo na kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji ya mtoto wake wa kambo na kusisitiza kifo cha Amina hakikuwa cha kawaida.
Jaji alisema ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa na Jamhuri mahakamani hapo umekubalika kwa kuwa unakidhi vigezo.
“Nimejiridhisha kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka unamtaja mshtakiwa bila pingamizi kuwa ndiye aliyemuua marehemu na hakuna mtu ambaye angeweza kufikiria mwili wa marehemu ulikuwa msituni kama si mshtakiwa kukiri kupitia maelezo yake ya onyo,” alisema Jaji