Atupwa jela miaka 30 kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la tatu

Morogoro. Antony Myonga (36), mkazi wa Ubuyu Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na faini ya Sh500, 000 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 11.

Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa, Novemba 29, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ulanga, Christopher Bwakila, baada ya ushahidi kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 10, 2024, akiwa amepokea hifadhi kwa bibi wa mtoto huyo.

Kwa mujibu wa ushahidi, Myonga alimshawishi mtoto huyo kwa Sh2,000. Baada ya kumbaka mbele ya mdogo wake aliyepiga kelele zikamwamsha bibi yao na mshtakiwa akatoroka.

Hata hivyo, alikamatwa baadaye na kufikishwa mahakamani.

Hakimu Bwakila amesema: “Kitendo hiki ni cha kikatili na hakivumiliki katika jamii, hivyo mshtakiwa anastahili adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.”

Related Posts