CCM yataja sababu nne zilizowezesha ushindi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Tamisemi kutangaza matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji yaliyoonyesha CCM kushinda kwa asilimia 95, chama hicho kimetaja sababu nne zkuwa ziliwezesha “ushindi huo wa kishindo.”

Sababu hizo ni pamoja na uratibu mzuri wa kampeni, utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, maandalizi ya uchaguzi na migogoro ndani ya vyama vya upinzani.

Jana, Alhamisi Novemba 28, 2024, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alitangaza matokeo ya uchaguzi huo, yaliyoonyesha kati ya vijiji 12,271 kati ya nafasi 12,280 zilizopaswa kufanya uchaguzi, CCM ilishinda nafasi 12,150. Kwa mujibu wa Mchengerwa, nafasi za uenyekiti wa vitongoji zilikuwa 63,849 kati ya nafasi 63,886 zilizopaswa kufanya uchaguzi, ambapo CCM ilishinda nafasi 62,728.

Akizungumzia ushindi huo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amesisitiza kuwa chama hicho kilijiandaa vizuri huku akisema uchaguzi umekwisha na upinzani unapaswa kujiandaa na chaguzi zijazo.

Makalla amesema kuwa Watanzania wameridhika na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25, ambayo imefanikisha miradi ya maendeleo sambamba na utatuzi wa kero mbalimbali, hali iliyojenga imani ya wananchi kukiamini chama hicho.

“Miradi mbalimbali inayotekelezwa ipo katika mitaa na kata, tunaamini mafanikio yaliyopatikana yamejenga imani kwa wananchi kuendelea kuamini CCM,” amesema Makalla.

Makalla amrongeza kuwa CCM ilijiandaa mapema kuelekea katika uchaguzi huo, akibainisha walifanya tathmini ya viongozi waliopo madarakani katika mitaa, vijiji na vitongoji, sambamba na kuchambua changamoto na kukusanya maoni ya wananchi.

“Hatujakosea katika uteuzi wa wagombea waliopeperusha bendera. Hii ndio siri ya ushindi pia, kwa sababu tulifanya tathmini ya hali ya kisiasa katika vijiji na kila wilaya ili kukipa chama nafasi ya kuteua wagombea bora. Tulichukulia kwa uzito mkubwa uchaguzi huu, ndio maana ushiriki wetu ulikuwa mkubwa katika ngazi mbalimbali ikiwemo maandalizi ya kuwaandaa wananchi.

Kwa mujibu wa Tamisemi, CCM ndio chama pekee kilichoweka wagombea katika nafasi zote za vijiji, vitongoji na mitaa, huku vyama vya upinzani vikiweka wagombea katika nafasi 30,977, sawa na asilimia 38 ya nafasi zote 80,430 zinazoshindaniwa.

Sababu nyingine ya ushindi, kwa mujibu wa Makalla, ni uratibu wa kampeni za CCM kuanzia uzinduzi hadi kuzihitimisha, akisema kulikuwa na ushirikishwaji mzuri wa viongozi wa chama na jumuiya zake kuanzia ngazi ya taifa hadi mashina.

Katika uzinduzi wa kampeni hizo, CCM iliwatumia wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama waliotawanywa katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufanya mikutano ya hadhara, vivyo hivyo wakati wa kufunga mchakato huo.

Makalla pia amedai kuwa migogoro ndani ya baadhi ya vyama vya upinzani ilichangia ushindi wa CCM.

 “Wanasema adui yako muombee njaa, ni wazi migogoro katika vyama vya siasa vimeipa nafasi CCM kushinda uchaguzi huu,” alisema Makalla bila kutaja vyama hivyo.

Kupoteza baadhi ya mitaa, vijiji na vitongoji

Katika mkutano huo, Makalla amekiri kwamba licha ya ushindi mkubwa, baadhi ya vijiji, vitongoji na mitaa ambayo imekuwa ngome ya CCM kwa muda mrefu imechukuliwa na vyama vya upinzani.

“Sio sawa kulalamika, umevuna ulichopanda. Hata CCM tungetamani vijiji, vitongoji na mitaa tulivyopoteza vingekuwa vyetu. Ila tumekubali, ndio demokrasia, lazima tuendelee kufanya kazi na kutoa matumaini kwa wananchi.

“Niseme huwa tunakosea sana. Hii dhana ya demokrasia ya kweli ni pale chama tawala kinaposhindwa, hii dhana potofu. CCM inachaguliwa na wananchi, haijiweki yenyewe madarakani. Ikishindwa ndio demokrasia, ikishinda sio demokrasia?” amesema Makalla.

Akemea matukio ya mauaji, vurugu

Katika hatua nyingine, Makalla amekemea vitendo vya mauaji, watu kupigwa na kujeruhiwa, matukio ambayo yaliripotiwa kutokea wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Hata hivyo, Makalla ametoa angalizo akisema, “Tunapokemea, basi tukemee kwa pamoja. Sio vyama vya upinzani wakipata matukio hayo tukayakemea, lakini tukasahau CCM ambacho kimefanyiwa matukio kama hayo.

“Nataka kuweka rekodi sahihi. Kwa taarifa tulizonazo, CCM ina makada sita waliopigwa, kujeruhiwa na kuuawa. Mtakuwa mashahidi, Novemba 13, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Tosamaganga.

“Isije ikasemekana huko kwingine unaandika tu mtu kauawa, lakini CCM hatajwi. Matukio haya tunayalaani wote,” alisema Makalla.

Aidha, Makalla alitaja kuwa kuna taarifa za kujeruhiwa kwa makada wanne wa CCM katika wilaya za Rorya, Songwe na Tarime wakati wa mchakato wa uchaguzi, akiwataka Watanzania kuamini kuwa hata makada wa chama tawala wamekumbana na kadhia hiyo, sio upinzani pekee.

Related Posts