Chanzo cha H. Pylori na jinsi ya kuiepuka

Dar es Salaam. Unaweza ukawa na maumivu makali ya tumbo yanayokufanya uhisi kama linawaka moto, limejaa gesi huku ukihisi kichefuchefu na hata kutapika, ukafikiria una vidonda vya tumbo.

Ukipata dalili hizi ni vyema kufika hospitali kufanyiwa vipimo na uchunguzi wa kitabibu kwa sababu huenda ukawa unasumbuliwa na bakteria aina ya H. Pylori.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na tatizo hilo hivi karibuni, Saraphina Sanga, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam anasema kwa muda wa takribani miezi sita alikuwa akisumbuliwa na tumbo kujaa gesi.

Anasema alijaribu kutumia dawa mbalimbali, ikiwemo zile za mitishamba, kulamba jivu akilenga limsaidie kuondoa hali hiyo ya kuhisi gesi kujaa tumboni, lakini hakupata ahueni yoyote.

“Nilipoona hali imezidi kuwa mbaya nikaenda hospitali na baada ya vipimo, niligundulika nina H. Pylori, baada ya kupatiwa matibabu nilipona kabisa,” anasema.

Kwa mujibu wa wataalamu na tovuti mbalimbali za afya, H. Pylori ni kifupi cha neno Helicobacter pylori, ni aina ya bacteria inayoingia mwilini mwa binadamu na kujificha ndani ya mfumo wa chakula unaoanzia mdomoni hadi kwenye tundu la haja kubwa.

Akizungumza tatizo hilo, Daktari wa magonjwa ya binadamu, Shita Samwel anasema kimelea huyo pia ana tabia ya kusababisha vidonda vya tumbo.

Bakteria wa H. Pylori kwa kawaida huenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kugusana moja kwa moja kwa mate, matapishi au kinyesi.

Pia huenea kupitia chakula au maji yaliyochafuliwa. Njia kamili ya bakteria ya H. Pylori kusababisha shambulizi au kuleta vidonda vya tumbo kwa baadhi ya watu bado haijulikani.

Anasema mtu aliyeambukizwa H. Pylori anaweza kuhisi maumivu ya tumbo au kuungua tumbo.

Maambukizi ya H. Pylori husababisha muwasho na uvimbe kwenye utando wa tumbo, madhara ambayo yanaweza kusababisha maumivu ya muda mrefu ya tumbo kuuma kidogo au hisia za kuungua.

“Mtu mwenye tatizo hili huvimba kwenye tumbo la juu, kichefuchefu na kutapika. Ukosefu wa hamu ya kula chakula kwa muda mrefu. Kupata haja kubwa iliyochanganyika na damu,” anasema.

Anaongeza kuwa changamoto hiyo isipotibiwa kwa muda mrefu inaweza kusababisha kuharibu utando wa kinga wa tumbo na utumbo mwembamba au kuufanya kuvimba.

“Hii inaweza kuruhusu asidi ya tumbo kuunda kidonda wazi (kidonda). Takriban asilimia 10 ya watu walio na H. Pylori watakuwa na kidonda.

 “Maambukizi ya H. Pylori yanaweza kuathiri tumbo na kusababisha shambulizi (gastritis) na uvimbe sambamba na saratani ya tumbo. Maambukizi ya H. Pylori ni sababu kubwa ya hatari kwa aina kadhaa za saratani za mfumo wa chakula,” anasema daktari huyo.

Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji na magonjwa ya mfumo wa chakula na ini kutoka Muhimbili, Dk Andrew Swalo anasema asidi inatengenezwa ndani ya tumbo, inachujwa na kuja katika nafasi ya wazi ya tumbo, inakaa pale, yenyewe ina kazi maalumu ya kuua vijidudu vyote vinavyoingia na chakula.

Anasema pale kinapokaa chakula, asidi huwa haigusani kabisa na seli zilizotengenezwa, ndiyo maana kuna watu wanapata vidonda vya tumbo na wengine hawapati.

Kwa sababu bakteria wa H. Pylori huingia tumboni kwa kubebwa na chakula ambacho kimeguswa na kinyesi.

“Bakteria huyu anaishi kwenye kinyesi cha binadamu. Magonjwa mengi ya tumbo ya kuharisha tunayapata kwenye vinywaji chanzo ni chakula kilichochanganyika na kinyesi.

“Bakteria huyu akiingia tumboni anaenda kuishi kwenye kuta za tumbo. Na akiingia huko ataharibu uwiano wa nguvu tetezi zilizopo ndani ya tumbo na akifanikiwa kuchimba, asidi ikija itaingia moja kwa moja kwenye kile kidonda na huweka makao pale. Na ataendelea kupachimba kwa kuwa kila siku tumbo linatengeneza asidi ya kutosha mpaka kinakuwa kidonda,” anasema Dk Swalo.

Njia za kuzuia au kujikinga

Kwa upande wake, Dk Daudi Gambo anasema mtu anaweza kujikinga na vimelea hivyo kwa kuzingatia kanuni za kiafya kwa kuwa msafi na kuhakikisha unanawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka. “Ni muhimu sana kufanya hivyo baada ya kutumia bafu au haja, nawa kabla ya kula. Hakikisha vyakula vyote unavyokula visafishwe kwanza na kupikwa kwa usalama na maji ya kunywa ni vema yakawa safi na salama,” anasema.

Hata hivyo, Dk Shita anasema kisayansi, matibabu ya tatizo hilo ni kutibu uambukizi wa vijidudu vya H Pylori kwa mseto wa dawa tatu hadi nne na kwamba ndani ya dawa hizo kuna antibaotiki na dawa za kupunguza au kuzuia tindikali ya tumbo.

Related Posts