Dk Ndugulile atakumbukwa kwa misimamo yake

Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile, alikuwa mtu mwenye msimamo, aliyesimamia maadili ya kitaaluma.

Dk Ndugulile (55) alifariki dunia usiku wa kuamia jana Jumatano, Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Wakati Tanzania ilipochukua njia isiyo ya kawaida kushughulikia janga la Uviko-19, Dk Ndugulile alithubutu kusimamia maadili yake ya kitaaluma.

Akiwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee, wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli, ugonjwa huo ulileta sintofahamu kwa wataalamu wa Wizara ya Afya, ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Waziri, Ummy Mwalimu.

Maambukizi ya Uviko-19 yalizuka mwishoni mwa 2019, lakini Tanzania ilirekodi maambukizi kwa mara ya kwanza Machi 16, 2020.

Dk Magufuli alitangaza Tanzania haina Uviko-19, aliungana mkono tiba za asili na mitishamba ikiwemo kujifukiza mchanganyiko wa mitishamba, akipinga wazi mbinu za kisayansi.

Mei 2020 Tanzania ilipokea shehena ya dawa ya mitishamba kutoka Madagascar kwa ajili ya Uviko-19, licha ya shaka ya kimataifa na onyo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kutothibitishwa kwa ufanisi wake.

Aprili 2020, Dk Magufuli alihimiza kujifukiza akieleza ingeweza kuua virusi, akihoji uaminifu wa maabara ya kitaifa ya afya, kwa kuwa alifanya majaribio ya siri kwenye papai, kware na mbuzi ambayo yalionyesha matokeo chanya ya Uviko-19. Mkurugenzi wa maabara hiyo, Nyambura Moremi, alisimamishwa kazi baadaye.

Dk Ndugulile Aprili 2020, aliwaonya wananchi dhidi ya matumizi ya kuvuta mvuke kama tiba ya Uviko-19, akisema ingeweza kuzuia mfumo wa upumuaji. Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni cha ndani, alisisitiza baadhi ya tiba za kiasili zinazotangazwa hazikuwa za kisayansi.

“Watu kadhaa wamesema kuhusu tiba fulani za kiasili kwa Uviko-19… Kumweka mgonjwa karibu na mvuke wa mimea inayochemshwa si chaguo sahihi kwa sababu inaweza kuathiri mfumo wa upumuaji usiovumilia joto kali,” alionya Dk Ndugulile.

Mei 2020, Dk Ndugulile aliondolewa katika wadhifa huo na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Godwin Mollel, hatua iliyotafsiriwa kuwa ilitokana na msimamo wake.

Akizungumza na gazeti la The Citizen jana, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko alimtaja Dk Ndugulile kama mtaalamu mwenye ujasiri aliyeishi kwa yale aliyojifunza darasani wakati wa janga la Uviko-19.

“Dk Ndugulile alionyesha kwa wenzake kuwa wakati fulani, lazima ushikamane na maamuzi ya kitaaluma bila kujali matokeo.

“Sauti yake kuhusu masuala ya afya, hasa juu ya Uviko-19, Ukimwi na malaria ilikuwa ya mantiki na utaalamu. Katika dunia tunayoishi, lazima tufuate njia za kitaaluma, hata kama ni ghali. Dk Ndugulile aliishi roho hiyo,” alisema.

Wakati kukiwa na mchanganyiko wa maelekezo kuhusu vipimo na matibabu ya ugonjwa wa njia ya mkojo (UTI), Dk Ndugulile alikuwa akisisitiza hadharani kuwa ugonjwa huo ni lazima upimwe maabara na majibu yapatikane ndani ya siku mbili au tatu.

“Huwezi kutambua kwa kumwangalia mtu hivi, au kumuuliza mtu maswali matatu. UTI inatakiwa kupimwa kwa kufanyika vipimo vya maabara na inachukua kati ya siku mbili mpaka siku tatu kujua.

“Nimekuwa nikisisitiza watoa huduma wetu wa afya na wananchi kwa ujuma, daktari anayekwambia una UTI kwa kwenda kumtembelea hospitali ndani ya dakika 15 huyo hakutendei haki,” alisema katika mahojiano na waandishi wa habari jijini Dodoma Februari, 2020.

Akiwa mbunge wa Kigamboni, Dk Ndugulile alitofautiana na Serikali kuhusu ujenzi wa mji mpya (Kigamboni Satellite city), akitaka wananchi washirikishwe kwanza.

Julai 11, 2012, Dk Ndugulile alidai bungeni kuwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alitumia fedha za Serikali kuwapeleka bungeni hapo baadhi ya wananchi wa Kigamboni ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusaka uungwaji mkono.

Kwa kauli hiyo, aliyekuwa Naibu Spika wakati huo, Job Ndugai alimtaka kuwasilisha ushahidi kesho yake, jambo ambalo hakulitekeleza.

Ndugai alisema kitendo alichofanya mbunge huyo hakikubaliki kwani ni kinyume cha kanuni za Bunge akaagiza aondolewe ukumbini, naye alitii.

Februari 23, 2013 Dk Ndugulile aliwalalamikia madiwani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mji Mwema kuwa hawana uelewa na ujenzi wa mji huo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Madiwani wa Kigamboni wakati huo, Selemain Methew aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa mbunge wao amekiuka taratibu za uongozi kutokana na kuwachonganisha na wananchi katika mradi huo.

Mvutano kati yake na Profesa Tibaijuka, uliendelea, ambapo Agosti 2014, wawili hao walikutana katika mkutano uliohusisha viongozi mbalimbali wa jimbo hilo, wakiwamo madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa.

Katika mkutano huo, Profesa Tibaijuka alimtaka Dk Ndugulile kuacha kuwapotosha wananchi kuwa mradi mpya wa Kigamboni haupo, badala yake washirikiane kuhakikisha wanajenga mji wa kisasa, ambao utaliletea Taifa heshima na faida kwa wakazi wake.

Hata hivyo, akihojiwa na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam Novemba 25, 2012, Dk Ndugulile alikanusha kupinga mradi huo, akisema alichotaka ni Serikali imhakikishie kuwa wananchi wanashirikishwa katika hatua ya maamuzi juu ya mradi wao.

Hata hivyo, mradi huo haukutekelezwa baada ya awamu tano ya Hayati John Magufuli kuingia madarakani.

Wakati Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakijenga daraja kuelekea Kigamboni, Dk Ndugulile alipinga wananchi kutoza fedha.

Akichangia mjadala wa kupitia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mei 24, 2022 jijini Dodoma, Dk Ndugulile alisema hoja ya wananchi wa Kigamboni ni kufuta tozo ya daraja. 

“Wananchi hawa wanachangia katika ujenzi wa madaraja mengine nchini na wanachangia kulipa madaraja mengine, iweje wananchi wa Kigamboni katika daraja linalowahusu wao walipe na wananchi wengine wasichangie katika hili?” alihoji.

Katika mchango mwingine akiwa pia bungeni, Dk Ndugulile alisema: “Ili mwananchi wa Kigamboni afike mjini maana yake ni lazima apite Ferry apande pantoni ambapo analipa tozo au inabidi au apite darajani kwa mguu au kwa wale wenye magari au vyombo vya usafiri ambako analipa tozo.

“Daladala moja inayopita pale inachajia kati ya Sh5,000 kwa kila tripu anayovuka pale, zikiwa tripu 10 kwa kwenda na kurudi hiyo ni Sh100,000. Mwananchi wa Kigamboni anahitaji nauli tatu hadi nne tofauti na wakazi wengine wa Jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Related Posts