Guinea,Sudan zipaisha Tanzania FIFA | Mwanaspoti

USHINDI wa mechi mbili dhidi ya Sudan na Guinea umeipaisha Tanzania kwenye viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Stars ilikutana na Sudan katika michuano ya CHAN kutoka na sare ya matokeo ya jumla ya kufungana 1-1, kila taifa likishinda kwake nyumbani kwa bao 1-0 mechi ya mwisho ya marudiano ikipigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Kwenye mechi hiyo ya mwisho Stars iling’olewa kwa matuta lakini Fifa huangalia matokeo ya dakika 90, ambayo ndio yaliyoipa pointi Tanzania kupitia matokeo hayo.

Baada ya mchezo huo Stars, ilishinda nyumbani tena kwa ushindi kama huo dhidi ya Guinea, matokeo yaliihakikishia Tanzania kufuzu kwenda Fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika Desemba, 2025 nchini Morocco.

Matokeo hayo yameifanya Stars kupanda kibabe kutoka nafasi ya 112 mpaka 106, katika viwango vya FIFA, huku ikiwaacha majirani zake Kenya.

Kenya ambayo hapo awali ilikuwa nafasi ya 106 sasa imeshuka mpaka 108, huku ikiwa na rekodi ya kutokufuzu katika michuano ya Afcon 2025, ikipata sare kwenye mechi zake za mwisho dhidi ya Namibia na Zimbabwe, yaliyowanyima tiketi ya kwenda Morocco.

Uganda ambao imefanikiwa kufuzu Afcon 2025 imeshuka katika viwango hivyo kutoka nafasi ya 87 mpaka 88 baada ya kupoteza mechi yake moja kati ya mbili za mwisho dhidi ya Congo Brazavile na Afrika Kusini.

Kupitia rekodi hizo Tanzania imeonyesha ubora wake kuwa haupo tu kwenye ligi ya ndani bali sasa imeota mbawa na kuanza kupanda hadi katika viwango vya FIFA.

Akizungumzia hilo Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema ingawa Tanzania imeendelea kupiga hatua lakini bado wataendelea kutafuta pointi zaidi ili nchi ifike kwenye viwango vya namba mbili za ubora.

“Ni hatua nzuri ambayo Tanzania inaendelea kuonyesha, kwa miaka ya hivi karibuni tumekuwa na hatua ya kupanda zaidi kuliko kushuka kwa kuwa kuna mkazo mkubwa wa kupata matokeo mazuri unaofanywa na TFF ikishirikiana na serikali.

“Tunapanda sawa lakini malengo ya TFF ni kwamba tunataka kuendelea kupaa ili totoke kwenye hizi ranki za namba tatu yaani 106 twende mpaka kwenye namba mbili yaani kuanzia 99 kwenda juu,” alisema Ndimbo.

Kwenye viwango hivyo bado Argentina imeendelea kuwa namba moja ikifuatiwa na Ufaransa wakati Hispania ikishika nafasi ya tatu, England ikaa nafasi ya nne huku Brazil ikishika nafasi ya tano.

Related Posts