Hatima ya Mdude yasogezwa hadi Desemba 2

Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, leo Ijumaa Novemba 29, 2024 imeahirisha tena shauri la kada wa Chama cha Demokrasia na Mandeleo (Chadema), Mdude Nyagali hadi Desemba 2, 2024.

Shauri hilo namba 33247/2024 lilifunguliwa Novemba 26, 2024 na Wakili Boniface Mwabukusi akishirikiana na Philipo Mwakilima, wakitaka upande wa Jamhuri kumfikisha mahakamani au kumwachia huru mteja wao, Mdude.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mussa Pomo alianza kusikiliza hoja za waleta maombi na wajibu maombi jana Novemba 28, 2024 na kisha kuaihirisha hadi leo Novemba 29, 2024 kabla ya kulipiga tena kalenda mpaka Desema 2, 2024 atakapotoa uamuzi.

Jaji Pomo amewaeleza mawakili wa mleta maombi na wa Serikali, Joseph Mwakasege kuwa sababu za kuahirisha shauri hilo ni kwamba alikuwa anasikiliza kesi za mauaji na kuzitolea hukumu.

Akizungumza na vyombo vya habari, Wakili Mwabukusi amesema msimamo wao ni kutaka Jeshi la Polisi kumfikisha mahakamani Mdude au kumwachia huru na kuacha “kumficha kama hirizi na kumzuia kuonana na mawakili wake.”

Amesema shauri lao ni kutaka mleta maombi kama ana kesi ya kujibu afikishwe mahakamani au aachiwe, jambo ambalo utekelezaji wake umekuwa mgumu.

“Kitendo cha kushindwa kumfikisha mahakamani Mdude kinalipaka matope Jeshi la Polisi na viongozi katika masuala la ulinzi na haki za binadamu kwa kutumia mamlaka yake vibaya, hali inayoandika rekodi mbaya ya nchi,” amesema Mwabukusi.

Amesema Watanzania wameona ukamatwaji wa Mdude kwa kupigwa na kuteswa hadharani na kisha kufichwa na kuwapa jukumu mawakili wake kumtafuta, hali ambayo si nzuri katika misingi ya utawala bora.

Mwabukusi amesema hawatakata tamaa, wataendelea kufuata maelekezo ya Mahakama, lengo ni kutetea haki mteja wao na kuhakikisha anafikishwa mahakamani au kuachiwa huru.

“Nasisitiza Jeshi la Polisi liache kufanya kazi kihuni, kinyume cha sheria, kutesa raia na kama inabainika ana kosa ni vema akafunguliwa shtaka na kufikishwa mahakamani na sio kuwaficha watu kama hirizi mifukoni.

Novemba 22, 2024, kada huyo wa Chadema, akiwa na Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Kanda, Joseph Mbilinyi (Sugu), walikamatwa na Polisi Mkoa wa Songwe walipokuwa wakielekea kwenye mkutano wa hadhara katika Mji wa Tunduma.

Hata hivyo, viongozi na makada wengine wa chama hicho waliachiwa kwa dhamana lakini kada huyo aliendelea kushikiliwa kwa kilichoelezwa ni uchunguzi wa makosa mbalimbali aliyofanya ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Related Posts