Maandamano yanaendelea baada ya uchaguzi nchini Msumbiji

Maandamano yanaendelea baada ya mazungumzo yaliyopangwa kumaliza machafuko nchini Msumbiji kutibuka.

Msumbiji imekumbwa na maandamano mabaya ya wiki kadhaa kuhusu uchaguzi wa urais wa tarehe 9 Oktoba, ambao umefichua kutoridhika kwa umma na utawala wa nchi hiyo.

Maandamano hayo yalianza tarehe 21 Oktoba baada ya Venancio Mondlane, mgombea anayeungwa mkono na chama cha upinzani cha Podemos, kuitisha maandamano dhidi ya mauaji ya wakili wake Elvino Dias na Paulo Guambe, afisa wa Podemos.

Dias aliripotiwa kukusanya ushahidi wa udanganyifu katika shughuli ya upigaji kura wakati yeye na Guambe walipouawa kwa kupigwa risasi mjini Maputo tarehe 19 Oktoba.

Tarehe 24 Oktoba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE) ilitangaza Frelimo na mgombea wake Daniel Chapo kuwa washindi wa kura kwa kupata asilimia 71 ya kura.

Mondlane alikataa matokeo ya CNE ambayo yalimpa 20% ya kura na akaitisha maandamano nchini kote dhidi ya madai ya udanganyifu katika uchaguzi.

Chama cha upinzani cha Renamo kinachoongozwa na Ossufo Momade na Democratic Movement cha Msumbiji kinachoongozwa na Lutero Simango kilijiunga na wito wa Mondlane wa maandamano ya nchi nzima kudai “kurejeshwa kwa ukweli wa uchaguzi”.

Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kireno (CPLP) na Jumuiya za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) zilisema kuwa ingawa kwa kiasi kikubwa kulikuwa na amani, mchakato wa kuhesabu kura uligubikwa na kasoro .

Mamlaka iliwataka raia wa Msumbiji kusitisha maandamano na baadaye kuyapiga marufuku na kuvuruga mtandao huku maelfu ya watu wakijitokeza kwa “zaidi ya maandamano 200 yenye vurugu” tangu tarehe 21 Oktoba.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, likiwemo Amnesty International, yamekosoa majibu ya vikosi vya usalama dhidi ya maandamano hayo.

Kituo cha kiraia cha Uadilifu wa Umma kilisema tarehe 20 Novemba kwamba watu 65 wameuawa, zaidi ya 1,000 wamejeruhiwa na zaidi ya 4,000 wengine kuzuiliwa wakati wa mgogoro wa kisiasa.

Takwimu za shirika hilo zimekuja siku moja baada ya Rais Filipe Nyusi kusema kuwa watu 19 waliuawa na wengine 807 kujeruhiwa katika machafuko ya baada ya uchaguzi.
 

Related Posts