Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda baada ya kubainisha mambo matatu yanayoifanya mahakama hiyo kutomtia hatiani.
Uamuzi wa kesi hiyo ya jinai namba 1883/2024, yenye kosa la kulawiti, umesomwa leo Ijumaa Novemba 29, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Erick Marley.
Upande wa Jamhuri kwenye shauri hilo uliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Magreth Mwaseba, Benedicto Dube na Japhet Ngusa, huku mshtakiwa Dk Nawanda akitetewa na jopo la mawakili Constantine Mutalemwa, Alex Mgongolwa, Kalaghe Rashid na Kennedy Mgongolwa.
Katika hukumu, hakimu Marley amesema baada ya kuwasikiliza mashahidi 10 wa upande wa Jamhuri na utetezi na kupitia vielelezo 17, mahakama imemkuta Dk Nawanda hana hatia ya kumlawiti mlalamikaji aliyetambulika mahakamani kama TMN.
Akisoma hukumu, Hakimu Marley amesema mashahidi walilioletwa mahakamani na kutoa ushahidi wao ni pamoja na mwathirika wa kitendo hicho (aliyedai kulawitiwa), mama yake mzazi, maofisa upepelezi wa Jeshi la Polisi, mtaalamu wa tehama kutoka Rock City Mall na daktari aliyemfanyia uchunguzi mwanafunzi huyo.
Hakimu Marley amesema mahakama baada ya kusikiliza maelezo ya ushahidi wa pande zote, imejiridhisha kuwa maelezo ya ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanzia shahidi wa kwanza hadi wa sita hayaoani, huku akieleza ushahidi wa mama unakinzana na wa mwathirika TMN.
“Katika ushahidi wake mama wa mwathirika alisema hakuwahi kupokea ofa yoyote ya fedha ili kutofungua kesi hii mahakamani ilhali mwathirika (TMN) aliieleza mahakama hii kuwa Dk Nawanda alifika hotelini alipofikia mzazi wake kwa lengo la kuomba radhi na kumpatia fedha ili asifungue shauri hili,” ameeleza Marley.
Amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuonyesha ushahidi wa kisayansi.
Amesema daktari aliyemfanyia uchunguzi baada ya kudaiwa kufanyiwa ukatili huo, aliieleza mahakama kuwa baada ya kumchunguza alikuta kuna michubuko sehemu ya haja kubwa inayoashiria kuwa aliingiliwa na kitu butu.
Hakimu amesema pamoja na kubaini kuwa TMN ameingiliwa, shahidi aliieleza mahakama kuwa alishindwa kubaini ni kitu gani kilichomuingilia mwathiriwa huyo jambo alilodai linahitaji uthibitisho kwa kulinganisha vinasaba.
Mbali na hilo, Marley amesema mahakama haijapokea ushahidi wa kisayansi wa vinasaba (DNA) ambao ndiyo ushahidi uliokuwa na nguvu ya kuthibitisha iwapo kuna vinasaba kwenye sampuli zilizochukuliwa sehemu ya haja kubwa ya mwathiriwa.
“Shahidi namba moja (mama wa TMN) aliieleza mahakama kuwa mwathiriwa alifikishwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi baada ya saa 19 kupita kutokana alipoulizwa kwa nini alichelewa, akadai kwa sababu tukio lilitokea usiku na mlolongo wa kupatiwa fomu namba tatu ya Polisi (PF3) ulikuwa mrefu,” amesema hakimu.
Amesema mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, imebaini kuwa mwathiriwa alikuwa na mawasiliano na mshtakiwa, jambo ambalo linaonyesha walikuwa wakifahamiana hata kabla ya kudaiwa kutendewa kitendo hicho.
“Kwa kesi ya aina hii inatakiwa credibility (ushahidi usioacha mashaka) kutoka kwa mhusika na uoane na ushahidi wa mashahidi wengine. Hivyo basi kwa mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa havikujitosheleza kumtia hatiani mshtakiwa (Dk Nawanda) hivyo mahakama inamuachia huru,” amesema.
Hakimu Marley amesema iwapo upande wa mashtaka haujaridhishwa na uamuzi huo, una haki ya kukata rufaa.
Dk Nawanda alipofikishwa mahakamani alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024, katika maegesho ya magari yaliyoko eneo la Rock City Mall wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza. Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Julai 9, mwaka huu.
Baada ya kupandishwa kizimbani, alisomewa shtaka la kumlawiti ‘TMN’ kinyume cha kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16, shtaka ambalo alikana kulitenda kisha kesi ilipangiwa tarehe nyingine ya kusomewa maelezo ya awali (PH).
Baada ya kumsomea maelezo ya awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba, aliieleza mahakama kuwa upande wa Jamhuri utawasilisha mashahidi 10 na vielelezo 18 katika kesi hiyo.
Ilipofika Septemba 11, 2024, vyombo vya habari vilizuiwa kuingia kortini kwa kilichotajwa kuwa mwenendo wa kesi hiyo utasikilizwa faragha kwani kesi hiyo inahusisha ukatili wa kijinsia, ikiahidi kutoa mrejesho wa mwenendo huo itakapokuwa inaahirishwa.
Hata hivyo, jitihada za kuendelea kuripoti kuhusu mwenendo wa ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ziligonga mwamba, baada ya vyombo vya habari kupigwa danadana vilipohitaji kupewa mrejesho wa kinachoendelea mahakamani hapo.
Baada ya siku 79 kupita, bila vyombo vya habari kuripoti mwenendo wa kesi hiyo kutokana na kutopata taarifa, leo Novemba 29, 2024, mahakama imetoa hukumu na kumkuta Dk Nawanda akiwa hana hatia katika kesi hiyo.
Baada ya Hakimu Marley kuhimitisha kusoma hukumu, Dk Nawanda aliinuka alipokuwa amekaa akitokwa machozi, huku akisema mahakama imetenda haki.
Watu wengine wanaotajwa kuwa ndugu wa karibu wa Dk nawanda pia walitokwa machozi.
Huku wakimkumbatia kwa bashasha, ndugu hao walimpongeza Dk Nawanda huku wakisema: “Mungu ametenda.”
Wakati wote wa kusomwa hukumu ya kesi hiyo, familia ya mwathiriwa anayetajwa kuwa ni mwanafunzi wa Shahada ya Ugavi na Ununuzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza hawakuonekana mahakamani hapo.
Akiwa nje ya ukumbi wa mahakama, Dk Nawanda amemshukuru Mungu, familia yake, mawakili na mahakama hiyo kwa alichosema imetenda haki katika shauri hilo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, naishukuru familia yangu, naishukuru Mahakama imetenda haki, namshukuru kaka yangu Alex kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya. Basi Mungu ni mwema kila kitu kinatoka kwa Mungu kwa hiyo utukufu ni wake Mungu asanteni sana,” amesema Dk Nawanda kisha kupanda kwenye gari na kuondoka mahakamani hapo.