Hai. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kimeeleza kushangazwa na Mgombea wake katika Kijiji cha Useri, Kata ya Machame Narumu, Wilfred Ritte kutangazwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji hicho, licha ya kuondolewa katika kinyang’anyiro katika hatua za mapingamizi.
Katika matokeo hayo mgombea huyo wa Chadema anaonekana kupata kura 428 huku wa CCM akipata kura 408.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu, Katibu wa Chadema Wilaya ya Hai, Joseph Ntele amesema moja ya maajabu na miujiza waliyoiona katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni mgombea huyo kutangazwa mshindi licha ya kuondolewa katika hatua ya mapingamizi na hakushiriki kampeni wala kuweka wakala katika kituo hicho.
“Kata ya Machame Narumu ni moja kati ya kata ambazo wagombea wetu kwa zaidi ya asilimia 99 walienguliwa na miongoni mwa walioenguliwa ni Ritte. Mgombea alikata rufaa kupinga maamuzi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kijiji cha Usari na Kamati ya Rufani ilitupilia mbali malalamiko yake.
“Katika hali ya kushangaza na kustaajabisha tumeona kwamba ameshinda nafasi ya uenyekiti wa kijiji hicho, na katika kituo cha kupiga kura wenyewe hatukuwa na mawakala na hatukufanya kampeni kwa sababu mgombea alienguliwa.”
Alisema jana wagombea walitaarifiwa kwenda kuapishwa Ritte ni miongoni mwa watu waliopigiwa simu waende wakaape kwamba ameshinda nafasi ya uenyekiti, na alifika na ameapa.
Akizungumza na Mwananchi, Ritte amesema alitambua kuwa yeye ni miongoni mwa wagombea, baada ya kwenda kupiga kura asubuhi na kuona jina lake kwenye karatasi ya kura, hatua ambayo ilimsukuma na yeye kujipigia kura.
“Waliengua jina langu kwa mara ya kwanza tukaandika pingamizi, bado wakaondoa tukaandika rufaa wilayani, sikupata majibu. Baadaye siku ya kura jina likaonekana na baada ya jina kuonekana, wananchi wakanipigia kura.
“Nilipokuta jina langu nilijipigia kura na sikujua kama nitashinda maana baada ya kuondolewa jina langu sikufanya kampeni wala kuweka wakala.”
Amesema wakati matokeo yanatangazwa yeye alikuwa nyumbani na hakuwa amefuatilia kujua kilichotokea hadi asubuhi alipoambiwa na wananchi walioenda kuangalia matokeo kuwa ameshinda.
“Baada ya kuambiwa mimi ni mshindi nilijisikia vizuri kwa sababu wananchi waliniamini, nafurahia ushindi, kwamba wananchi wameniamini naweza kuwasaidia kutekeleza majukumu,” amesema.
Amewataka wananchi kumpa ushirikiano na watarajie mazuri na makubwa katika uongozi wake.
Akizungumza kwa njia ya simu, kuhusiana na suala hilo, Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Hai, Dionis Myinga amesema hajapokea lalamiko hilo kwa maandishi wala kutoka kwa Chadema, ingawa alikiri kulisikia kutoka kwa viongozi wa CCM wa kata hiyo.
Amesema kanuni ziko wazi, kama kweli limetokea suala kama hilo, kwa sababu shughuli za uchaguzi zimemalizika, angeshauri wanaolalamika waende mahakamani.
“Hatujapata lalamiko hilo kwa maandishi na wala kutoka kwa Chadema, isipokuwa jana wakati tunawaapisha, kulijitokeza suala hilo baada ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Kata ile ndio walikuja kutoa hiyo taarifa, walivyotoa taarifa hiyo na sisi tunaendelea kuifuatilia kuona kuna ukweli kiasi gani,” amesema Mayinga.
Ameongeza kuwa “Lakini kanuni ziko wazi, kama kweli limetokea suala kama hilo, kwa sababu sasa shughuli za uchaguzi tumeshazimaliza, kwa hiyo inapokuwa imetokea dosari yoyote baada ya kuwa uchaguzi umekamilika, maana yake sisi tunawashauri tu waende mahakamani, na mahakama inaweza kuliangalia hilo suala halafu baada ya hapo ikaeleza nani mwenye haki”.