Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile umewasili nchini kutoka India na kupokewa na viongozi mbalimbali, wakiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu.
Naibu Spika aliambatana na viongozi wengine wa Serikali wakiwemo mawaziri watatu Wiliam Lukuvi (Sera Bunge na Uratibu), George Simbachawene (Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) na Jerry Silaa wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mbali na viongozi hao kulikuwa na watumishi wa Bunge la Tanzania, familia, ndugu, jamaa na marafiki.
Mapokezi hayo yamefanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na baada ya kupokewa umepelekwa moja kwa moja katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kuhifadhiwa.
Dk Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, mwaka huu nchini India alikokuwa anapatiwa matibabu. Alitarajiwa kuanza kazi WHO Februari, 2025.
Akizungumza na Mwananchi, Simbachawene amesema mchango wa taaluma ya Dk Ndugulile hauwezi kusemwa kwa muktadha wa ki-inchi pekee bali hata Afrika.
“Kusema kweli kama Afrika imepoteza mtu. Namfahamu Dk Ndugulile tangu alipoingia bungeni mwaka 2010 na baadaye tulifanya kazi pamoja kama wabunge na tukaingia serikalini ingawa yeye alipitia nafasi tofauti naibu waziri na waziri,” amesema.
“Kama wanasiasa wenzake kweli tumepoteza mtu muhimu katika wakati muhimu. Nasema mtu muhimu alikuwa ni mtaaluma alikuwa mwenye misimamo katika jambo analoamini, alikuwa mzalendo anayependa kusimama na ukweli,” amesema.
Simbachawene amesema alikuwa mtu asiyependa kubabaika na Taifa limepoteza kwani lilikuwa linatarajia kuanza kuvuna matunda baada ya kuteuliwa kwake katika nafasi mpya WHO.
Mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee amesema Dk Ndugulile alikuwa naye bungeni kwa muda mrefu, na jambo lililompatia heshima ni kuamini anachokisimamia bila kujali chama anachotoka.
“Ilikuwa kama ana msimamo wake atasimamia ilimradi hajavunja sheria na kumvunjia mtu heshima yake. Nakumbuka kipindi ambacho Waziri wa Ardhi ni Profesa Anna Tibaijuka alikuwa anapambana na migogoro ya ardhi ambayo kimsingi wabunge wote ilikuwa inatusumbua,” amesema.
Halima amesema katika suala hilo, Dk Ndugulile aliona ni muda sahihi na bila unafiki wowote kusimamia kuona wananchi anaowaongoza wanapata haki zao.
“Kuwa na mbunge anayetoka chama tawala anasimama mara kwa mara kushika shilingi bungeni na kung’ang’ania hadi mwisho hao ni wabunge ambao hawapatikani, alikuwa mtu ambaye hana majivuno,” amesema.
Amesema Taifa limepoteza mtu mzuri ambaye alikuwa mcheshi na aliyefanya vitu vikubwa na kwamba: “Sote tuko njiani tumuombee.”
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba amesema: “Hakika Mungu ana siri nzito katika maisha yetu, funzo tunalolipata kadri tunavyoishi katika dunia hii tuwe watu wema, tukumbukwe kwa wema.”
Amesema Dk Ndugulile wanamkumbuka kwa tunu ya wema na wabunge wote wa Jiji la Dar es Salaam alikuwa mwenyekiti wao akiwasaidia kwa mengi.
“Kwa uchache ninayoyakumbuka alikuwa kinara wa kupigania ujenzi wa miundombinu ya barabara kupitia mradi wa DMDP awamu ya pili, alikuwa mhimili mkubwa kati yetu na Serikali.
“Mafanikio ya Dar es Salaam kujengwa vizuri zaidi ana mkono wake kwa asilimia kubwa, Yeye tulimweka mbele katika kupigania na kutafuta masilahi ya wananchi wa Dar es Salaam,” amesema.
Mwili wa Dk Ndugulile uliwasili JNIA saa 8.19 na kupokewa na viongozi waliokuwapo wakitanguliwa na familia ya marehemu. Maziko kwa mujibu wa familia yatafanyika Jumanne Desemba 3, Kigamboni.