Namungo, Yanga mechi ya kurudisha imani

Namungo na Yanga zitakutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kesho huku timu zote zikiwa hazijapata ushindi kwenye michezo ya hivi karibuni hivyo kila moja itakuwa inakwenda kwenye mechi hii ikiwa na nguvu kubwa.

Kwa upande wa Namungo ambayo imepoteza mechi nane kati ya 11 ilizocheza wakati Yanga ikipoteza mechi mbili.

Mabingwa watetezi Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Azam Novemba 2, 2024 ilipokubali kipigo cha bao 1-0 kabla ya kufungwa tena mabao 3-1 mechi iliofuata dhidi ya Tabora United Novemba 7, 2024, ambapo mechi zote mbili zilipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Namungo inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi tisa katika mechi 11 ilizocheza wakati Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 24 katika mechi 10 ilizocheza.

Yanga ambayo imetoka kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa Novemba 26, 2024 dhidi ya Al Hilal kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikikubali kipigo cha mabao 2-0 ikiwa na kocha wake mpya Sead Ramovic inakwenda kukutana na Namungo ambayo nayo inahitaji matokeo mazuri baada ya kuwa na mwendelezo mbaya wa matokeo kwenye Ligi Kuu.

Sead Ramovic ataiongoza Yanga kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu tangu achukue mikoba ya Miguel Gamondi, ndivyo ilivyo kwa kocha wa Namungo Juma Mgunda ambaye ataiongoza timu hiyo kwenye mechi ya pili tangu achukue mikoba ya Mwinyi Zahera ambaye amebadilishwa kuwa mshauri wa benchi la ufundi.

Yanga itaingia kwenye mchezo huu ikihitaji matokeo mazuri ili kupunguza nafasi ya ya pointi ambapo inazidiwa pointi nne na watani zao wa jadi Simba inayoshika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 28.

Namungo na Yanga zimekutana mara 10 kwenye Ligi Kuu ambapo Yanga imeshinda mechi tano na kupata sare mechi tano huku Namungo ikiwa haijawahi kupata ushindi. Katika mechi tano za ushindi, Yanga imeshinda mechi mbili ugenini na mechi tatu imeshinda ikiwa nyumbani huku ikipata sare mbili ikiwa nyumbani na mara tatu ikiwa ugenini.

Namungo na Yanga zimefunga mabao 22 ambapo Namungo imeifunga Yanga mabao saba wakati Yanga imeifunga Namungo mabao 15 katika mechi 10 walizokutana. Namungo itakuwa nyumbani ikiikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa Mkoani Lindi.

Related Posts