Tarime. Mpaka wa Sirari wilayani Tarime, mkoani Mara umekuwa ukitumiwa na ngariba kuvuka kati ya Tanzania na Kenya kutekeleza vitendo vya ukeketaji.
Imebainika takribani wasichana 100 hukeketwa kila msimu kutokana na mbinu hiyo ya ngariba kuvuka mipaka na kutekeleza tendo hilo ambalo kimila linajulikana kama tohara, japo kwa jicho la sheria ni jinai.
Maeneo yanayotajwa kuhusika na vitendo hivyo ni Kata za Nyanungu, Itiryo, Muriba, Nyasincha, Nyakinga, Susuni, Mbogi, Mwema, Sirari na Pemba.
Meneja miradi wa kituo cha kupinga ukeketaji cha Masanga, wilayani Tarime, Valerian Mgani anasema mbinu hiyo inayowezesha ngariba wa Kenya kufanya ukeketaji Tanzania na kinyume chake, imebuniwa kutokana na jitihada zinazofanywa na wadau kwa kushirikiana na Serikali za kuzuia vitendo hivyo.
“Wanachofanya sasa ni kuwasafirisha ngariba kutoka upande mmoja kwenda mwingine kwa kuwa wanakuwa hawajulikani, mnapofanya ufuatiliaji na kuwabaini, tayari wanakuwa wamemaliza kazi na kuondoka,” amesema Mgani katika mahojiano na Mwananchi.
Mbali na hilo, amesema wakazi wa maeneo ya mpakani pia wamekuwa wakiwasafirisha mabinti kwenda kukeketwa nchi jirani.
Mbinu hiyo anasema hufanikiwa kutokana na mwingiliano wa kijamii katika vijiji vilivyopo mpakani mwa Tanzania na Kenya.
“Wana mbinu nyingi, mfano watoto wa kike watatu hadi watano au hata mmoja wanaondoka na majembe kama vile wanakwenda kupalilia mashamba yaliyopo upande wa pili, kumbe ndiyo safari ya kwenda kukeketwa,” anasema.
Anaeleza mabinti pia huvusha mpaka mifugo inapopelekwa machungani au wanapokwenda kufuata mahitaji upande wa pili na kwamba hayo hufanikiwa kutokana na uratibu wa karibu wa wazee wa mila wa pande zote.
Kwa mujibu wa Mgani, utaratibu wa jamii katika mpaka huo, mzee wa mila wa koo zilizopo nchi moja anaongoza pia upande wa pili, wakiamini wao ni wamoja na ni ndugu.
Kwa uratibu wa viongozi wa koo, anasema maandalizi hufanyika na mabinti wanapovuka mpaka hutengewa maeneo maalumu kwa ajili ya kuwapokea na kufanikisha ukeketaji.
Mgani anasema mabinti hugawanywa katika meneo tofauti kuepuka msongamano ili wasigundulike, akieleza wanaokeketwa ni wa umri kati ya miaka minane na 16.
Hata hivyo, anasema kutokana na ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali na wanaharakati kutoka mataifa hayo mawili, ukeketaji umepungua kwa kuwa awali walikuwa wanavuka makundi kwa makundi.
Anasema maandalizi ya ukeketaji hufanywa na wazee kwa usiri na miongoni mwayo ni kuchagua wasichana wanane na wavulana wanane maarufu ambao ni kielelezo cha uwepo msimu wa tohara salama.
Wahusika hao hufanyiwa tohara na ukeketaji kabla ya msimu kuanza na kisha hufuatiliwa na wazee wa mila na iwapo kutatokea kifo, msimu huo hakufanyiki tohara au ukeketaji, ikielezwa ni mkosi.
Anasema ni fahari kwa familia ambayo mtoto amechaguliwa kuwa miongoni mwa manane ikiaminiwa kuwa ni baraka.
Ngariba mstaafu aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema ukeketaji wa kuvuka mpaka ni mbinu mbadala inayitumika kunapotokea ulinzi mkali katika nchi mojawapo wakati wa msimu.
Anasema mangariba huvuka mpakani kwa kutumia pikipiki chini ya uratibu wa wazee wa mila.
“Maandalizi hufanyika kwa umakini, wakati mwingine hata mangariba hawajui eneo lililopangwa, ila siku ikifika unapelekwa kufanya kazi kisha unaondoka,” anasema.
Anasema ukeketaji hufanyika mafichoni na nyakati za usiku, akieleza kwa msimu ngariba anaweza kupata hadi Sh5 milioni kwa kazi hiyo na kwamba gharama za ukeketaji hutofautiana kati ya binti mmoja na mwingine, ingawa bei ya chini ni Sh30, 000.
Anasema gharama ya kumkeketa msichana aliyeanza uhusiano wa kimapenzi ni kubwa zaidi ya aliye bikira.
Kuhusu vifo, anasema hutokea kama ajali zingine na iwapo binti atafariki dunia akiwa anakeketwa nje ya nchi yake, suala hilo hushughulikiwa kwa usiri na wazee wa mila.
“Sijui huwa wanafanyaje, lakini wanapewa taarifa juu ya mwili kisha wao wanakutana wanaongea na kushirikisha familia ya marehemu, lakini hayo mambo hufanyika kwa siri, hasa ikizingatiwa kifo kimetokea nchi ya ugenini,” anasema.
Anasema kwa usiku mmoja ngariba mmoja anaweza kukeketa mabinti zaidi ya 10 kulingana na umbali uliopo baina ya maeneo yaliyotengwa.
Mkazi wa Kijiji cha Kegonga, Marwa Mugosi anasema ni vigumu kwa mtu mgeni kufahamu kuhusu maandalizi ya ukeketaji wa kuvuka mpaka, lakini wenyeji wa eneo husika wanafahamu.
Anasema wengi hawapo tayari kutoa taarifa kwani ikitokea wamegundulika na watu kukamatwa, atatengwa na jamii chini ya maagizo ya wazee wa mila.
“Si kutengwa wewe mtoa taarifa tu hata familia yako yote itatengwa, watoto wako watazuiwa kucheza au kushirikiana na wengine na hakuna kitu kinamuumiza Mkurya kama kutengwa na jamii, kwa hiyo wanaamua kukaa kimya. Wazee wa mila wana nguvu kubwa katika jamii hii, kila wanachoamua huwa kinatekelezwa kwa asilimia kubwa,” amesema.
Mkazi wa Kijiji cha Nyantira, Nyangi Wegesa amesema baada ya ukeketaji, mabinti hukaa huko hadi wanapopona ndipo hurudi nyumbani.
“Kwa asilimia kubwa watu wa vijiji vilivyopo mipakani wanakuwa na ndugu pande zote, hivyo siyo shida. Mwingine atafikia kwa mjomba, shangazi, mama mdogo, bibi au ndugu wengine na wanaishi kwa amani hadi atakapopona,” anasema.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Claud Mtweve anasema licha ya jitihada zinazofanyika, ukeketaji wa kuvuka mpaka bado upo.
Anasema ukeketaji katika maeneo hayo hufanyika kwa ushirikiano baina ya pande zote mbili kutokana na mwingiliano wa mila na tamaduni za watu hao.
Anasema kwa Tanzania vitendo hivyo uhusisha baadhi ya kata zilizopo wilayani Tarime na Kaunti ya Migori, nchini Kenya.
Mtweve anasema kutokana na hali ilivyokuwa awali, wadau waliunda kikosi kazi kupambana na vitendo hivyo, lengo likiwa kupeana taarifa, kufuatilia na kuzuia vitendo hivyo.
Mtweve ambaye pia ni mratibu wa kikosi kazi hicho upande wa Tanzania, anasema kiliundwa mwaka 2019 na kina wajumbe 16, wanane kutoka Tanzania na wanane Kenya.
Wajumbe wa kikosi kazi hicho wanatoka Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali na wadau wengine. Anasema vikao kwa ajili ya mipango na tathmini hufanyika kila baada ya miezi mitatu.
“Mwenyekiti wa kikosi kazi ni mkuu wa wilaya, tuna utaratibu wa kufanya vikao kwa mzunguko Tanzania na Kenya. Kwa kiwango kikubwa kimeleta mabadiliko chanya kwani idadi ya mabinti wanaovuka imepungua hata kwa kuangalia tu, awali walivuka kwa makundi wakati wa msimu,” anasema.
Mtweve anasema mwaka 2022 kupitia kikosi kazi, mangariba wawili wa Tanzania na mmoja wa Kenya walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Anasema ukeketaji ni suala la mila na tamaduni, haliwezi kupata mabadiliko chanya kwa haraka, hivyo elimu endelevu ni muhimu.
Anasema licha ya kushirikisha jamii, wakiwemo wazee wa mila na ngariba, bado haohao ndio wanahakikisha ukeketaji unafanyika.
“Kuna koo 12 ambazo zina wazee na si kwamba mzee wa mila anakuwa mmoja kwenye ukoo, hawa wanakuwa wengi kwa hiyo mkiandaa jambo na kuwaomba washiriki anatumwa msaidizi na si mzee mwenyewe, na hii yote ni kwamba, hii mila hawajawa tayari kuiacha,” anasema.
Anasema mwaka 2018 wazee wa mila na mangariba wilayani Tarime walipelekwa Biharamulo mkoani Kagera kupata mafunzo ya ujasiriamali ukiwa mkakati wa kuhakikisha ukeketaji haufanyiki lakini wakiwa huko waliratibu shughuli hiyo kwa kushirikisha wenzao wa Kenya.
Mtweve anasema kesi nyingi za ukeketaji zinaishia mahakamani bila watuhumiwa kuchukuliwa hatua kutokana na wahusika kutokuwa tayari kutoa ushahidi.
“Hakuna Mkurya atakayekuja kutoa taarifa kuwa mtoto wake amekeketwa kwani wanaamini kufanya hivyo ni kusaliti mila na desturi yao.
“Hivyo ikitokea amekamatwa yeyote huwezi ukapata ushahidi hata wa binti mwenyewe. Siku ya kesi atakwambia nilienda mwenyewe, kwa hiyo lazima utamuachia mtuhumiwa,” anaeleza.
Anasema umefika wakati watunga sheria waangalie namna ya kutunga sheria kali na mahususi kwa ajili ya kupinga ukeketaji, kama ilivyo Kenya, badala ya kuumika Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai inayohusisha makosa mengi kwa ujumla.
Meneja Mradi wa Shirika la Plan International mkoani Mara, Shaban Shaban amesema wanaelimisha jamii kuhusu athari za ukeketaji kwa kuandaa matamasha ya kimichezo, kuratibu semina za mafunzo kwa wadau wakiwemo viongozi wa Serikali, wazee wa mila, mangariba, wanafunzi na viongozi wa dini ili kujenga uelewa wa pamoja wa namna ya kushiriki mapambano dhidi ya ukeketaji ukiwepo wa kuvuka mpaka.
Anasema jitihada hizo zimesaidia kupunguza ukeketaji katika Mkoa wa Mara kutoka asilimia 32 hadi asilimia 28 kwa mwaka 2023.
Anasema unahitajika utashi wa kisiasa kupambana na ukeketaji, akieleza mwaka 2022 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee alitangaza msako wa nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji na kuwakamata waliohusika na ukeketaji wa mabinti 76.
Anasema sheria zinatakiwa kufanyiwa marekebisho kwani zinatoa mwanya wa kutenda vitendo hivyo kuendelea, akitoa mfano wa faini ya Sh500,000 kwa ngariba anayepatikana na hatia ya ukeketaji.
“Mtu kwa msimu anapata zaidi ya Sh5 milioni sasa akikamatwa unafikiri atashindwa kulipa faini? Hata akishindwa lazima atachangiwa na jamii, wakati mwingine hata wanasiasa wanashiriki kuwalipia faini,” anasema.
Imeandaliwa kwa ushirikiano wa Bill and Melinda Gates Foundation