Desemba Mosi 2024, siku ya Jumapili ni siku ya Ukimwi/VVU duniani. Huu ni ugonjwa sugu unaoambukiza na ni moja ya kihatarishi cha kujitokeza kwa uvimbe mbalimbali, ikiwamo saratani.
Katika kuelekea kuadhimisha siku hii, leo tutapata ufahamu kuhusu uvimbe hafifu na saratani. Ni kawaida kwa mwanadamu yeyote kupata mshtuko pale anapopata uvimbe wowote mwilini. Mara nyingi kwa haraka huweza kufikiria kuwa ni saratani.
Kwa kawaida mwilini huweza kuwa na aina mbili za uvimbe, yaani uvimbe hafifu kitabibu ni Benign tumour na uvimbe mbaya au saratani hujulikana kama Malignant tumour.
Cancer ni neno la Kiingereza likiwa na maana uvimbe saratani, ambao ndio uvimbe mbaya na tishio kwa mwili, kwani huongezeka, kusambaa na kusababisha madhara mbalimbali.
Si kila uvimbe mwilini ni saratani, hii ni kwa sababu unaweza kuwa na uvimbe lakini ni wa muda tu kama ilivyo kwa uvimbe wa jipu au ni uvimbe wa muda mrefu lakini kumbe sio uvimbe hafifu.
Uvimbe hafifu huundwa na seli ambazo hazitishii kuvamia tishu nyingine, hivyo kutokuwa tishio, zaidi huwa na madhara kidogo, ikiwamo kugandamiza tishu, mishipa ya fahamu au ya damu hatimaye kuleta dalili, ikiwamo maumivu.
Seli zake zinakuwepo hapo katika huo uvimbe pekee na si kwingine mwilini, ingawa uvimbe unaweza kuwa sehemu yoyote mwilini. Ni uvimbe usio tishio na unaweza kutibiwa kwa upasuaji pekee au ukaachwa bila kutibiwa, na kufuatiliwa mwenendo wake wa ukuaji.
Kwa upande wa saratani, uvimbe mbaya unaweza kuenea katika sehemu nyingine za mwili na mara nyingi hujirudia baada ya kuchelewa kuondolewa au usipotibiwa kwa tiba kemikali au mionzi.
Tofauti na uvimbe wa saratani, uvimbe wa kawaida huwa ni hafifu, hukua polepole na hausambai katika maeneo mengine ya mwili. Ingawa pia kuna aina nyingi za uvimbe hafifu.
Uvimbe wa saratani sifa zake ni pamoja na kukua kwa kasi, uwezo wa kusambaa na kuvamia tishu nyingine mwilini, kitabibu metastasis, kupoteza utofauti wa seli na usawa.
Vilevile huwa na kiwango kikubwa cha uharibifu wa chembe za urithi, yaani DNA na huku huleta usumbufu wa shughuli za kawaida katika mwili.
Mara nyingi sababu za uvimbe hazijulikani. Lakini, ukuaji wa uvimbe mbaya unaweza kuhusishwa na sumu za mazingira, kama vile kukabiliwa na mionzi, maumbile, chakula, mfadhaiko, majeraha, shambulizi na maambukizi, ikiwamo VVU.
Inaweza kutibiwa kwa lengo la kuondoa uvimbe saratani bila kuharibu tishu zinazozunguka, aina nyingine za matibabu zinaweza kujumuisha kemikali dawa au mionzi tiba.
Uvimbe wa saratani huvutia mishipa ya damu zaidi kuliko tishu za uvimbe kawaida. Hii huruhusu uvimbe wa saratani kukua zaidi, kwani mishipa ya damu huwaletea virutubisho.
Pia zinaingia kwenye mkondo wa damu, zinaweza kukaa katika eneo jipya na kuwa ‘metastatic’, yaani saratani imeenea kutoka katika uvimbe wa awali hadi eneo la pili.
Seli za kawaida za uvimbe hafifu hazifanyi hivi kwa sababu protini ndogo kwenye nyuso zao husaidia kuziweka mahali pazuri. Tofauti hizi ndio zinatupa ufahamu kuwa si kila uvimbe ni saratani.