Simulizi ya mwenyekiti wa mtaa aliyeongoza kwa miaka 39

Bukoba. Mkazi wa Mtaa wa Bulibata uliopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Alkadi Bagani (74) amekuwa mwenyekiti wa mtaa huo kwa kipindi cha miaka 39 sasa baada ya kuchaguliwa tena kwa miaka mitano ijayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 29, 2024 baada ya kula kiapo cha utii na uadilifu wa uongozi, Bagani amesema ameaminiwa na wananchi wa mtaa huo kwa sababu amekuwa akisaidia jamii na hupatikana muda wote pale wananchi wanapomuhitaji.

“Siri ya kuwa kiongozi kwa miaka 39 na kuaminiwa ni kwa sababu nimekuwa nikiwasaidia wananchi wangu kwa muda mwafaka, pale wanaponihitaji kutatua changamoto zao na nimekuwa mkweli kila wakati katika majukumu yangu,” amesema Bagani.

Amesema kuchaguliwa tena anaona ni matunda ya uongozi wake, hivyo hana wasiwasi na hali aliyonayo (ulemavu) wala uzee kumkwamisha katika kazi.

Bagani alizaliwa mwaka 1950 alisoma katka Shule ya Msingi Nyakato, iliyopo Bukoba mwaka 1963, baadaye alichaguliwa kwenda Nyarugongo Middle School alikohitimu mwaka 1967, kabla shule hiyo haijbadilishwa jina kuitwa Katoma.

Amesema hakuendelea na elimu ya sekondari bali aliishia hapo kutokana na utaratibu wa kielemu miaka hiyo.

Ameishauri Serikali kuendelea kuwasaidia watu wenye na wazee kupata matibabu ya kuaminika katika vituo vya afya, zahanati na hospitali kwa kupata matibabu kamilifu.

Mkazi wa Mtaa wa Bulibata, Ashura Juma amesema ameshuhudia mzee huyo akiongoza kwa ustadi, waledi, utulivu na uadilifu kwa kuwajali wananchi wake katika kutatua migogoro, ikiwemo ya familia, hivyo wanazidi kumwamini na kumpigia kura awe kiongozi wao.

“Haijalishi hali aliyonayo, nampenda sana kwa sababu ni mchapaka kazi, ukienda na tatizo analitatua au kulisukuma mahali husika ili lipatiwe ufumbuzi, nimefurahi sana na nimemchagua mwenyewe kwa kura yangu,” amesema Ashura.

Related Posts