Waasi walifika Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria, siku ya Ijumaa, katika shambulio la kasi kubwa dhidi ya majeshi ya Bashar Assad, ambayo yanaungwa mkono na washirika wa Urusi na Iran.
Mapigano hayo ni miongoni mwa makubwa zaidi katika miaka kadhaa, ambapo watu 255, wengi wao wakiwa wapiganaji, wameuawa, kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binadamu la Syria lenye makao yake Uingereza.
Yalianza Jumatano katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS). Waasi wanaoungwa mkono na Uturuki, wakijiita Jeshi la Kitaifa la Syria, walijiunga na mapigano hayo.
Raia wauwa katika mapigano
Jeshi la Syria limeapa kuwarejesha nyuma waasi hao, lakini hata kabla ya kuingia Aleppo, waasi walitwaa udhibiti wa zaidi ya miji na vijiji 50 kutoka kwa majeshi ya Assad.
Wakati huo huo, kamanda wa kijeshi wa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Syria, Abu Mahmoud Omar, alisema, “saa zijazo zitakuwa za maamuzi kwa mapigano baada ya kuwasili kwa vikosi vikubwa vya jeshi la Syria na majeshi washirika mjini Aleppo.”
Soma pia: Mamia ya watu wauawa katika mapigano ya waasi na jeshi nchini Syria
Umoja wa Mataifa umesema raia wasiopungua 27 wameuawa katika siku tatu zilizopita.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ilisema “zaidi ya watu 14,000, karibu nusu yao wakiwa watoto, wamepoteza makaazi” kutokana na ghasia katika siku tatu zilizopita.
“Nimeshtushwa na hali inayozorota kaskazini-magharibi mwa Syria na athari zake kwa maisha ya raia,” alisema David Carden, Naibu Mratibu wa Kikanda wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu nchini Syria.
“Tunapokea ripoti za watoto walio na majeraha mengi ya vipande vya mabomu kutokana na mashambulizi hayo,” aliongeza.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria havijawahi kuisha kabisaa
Ni takriban miaka 14 tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, mzozo uliotokana na mapinduzi ya wananchi yaliyokandamizwa kwa ukatili na serikali ya Syria inayoongozwa na Assad.
Urusi na Iran ziliiunga mkono serikali ya Syria baada ya maandamano ya kupinga serikali kubadilika kuwa vita.
Soma pia: Mapambano makali yaendelea Syria kati ya wapiganaji na jeshi
Uturuki imeunga mkono makundi ya upinzani na kuanzisha uwepo wa kijeshi kaskazini-magharibi mwa Syria, wakati Marekani imeunga mkono vikosi vya Wakurdi wa Syria vinavyopambana na wanamgambo wa “Dola ya Kiislamu” (IS) mashariki mwa Syria.
Tangu mwaka 2020, mzozo huo umetwama kwa sehemu kubwa, kukiwa tu na mapigano ya kiwango cha chini kati ya waasi na majeshi ya Assad.
Uturuki na Urusi ziliongoza makubaliano ya kusitisha vita mwaka 2020, na serikali ya Syria ikasitisha harakati za kutwaa maeneo yanayoshikiliwa na waasi katika mkoa wa Idlib.