Watoto hatarini usugu wa dawa za antibaotiki

Mwanza. Utafiti mpya umeonesha watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na watu waishio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) ni waathirika zaidi wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibaotiki mwilini (Uvida).

Utafiti huo uliofanywa jijini Dar es Salaam, ulilenga kuangalia tabia za bakteria wenye kuhimili dawa nyingi miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na watu wazima walioathirika na virusi vya Ukimwi.

Kati ya watoto 200 waliochunguzwa sampuli zao, utafiti ulibaini 112 walikutwa na vimelea wenye usugu wa dawa (ESBL-PE).

Utafiti huo ulifanywa na Mhitimu wa Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (Cuhas-Bugando), Dk Upendo Kibwana kati ya mwaka 2020/22.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutunukiwa PhD yake na Askofu wa Jimbo la Bunda, Askofu Simon Masondole kwenye mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliyofanyika Novemba 16 mwaka huu, Dk Upendo anasema utafiti huo uliangalia kundi la vijidudu hatari zaidi.

“Utafiti huu umeonesha kwamba kati ya watoto 200 ambao sampuli zao zilichunguzwa, asilimia 56 (112) walikuwa na vijidudu vya ESBL-PE kwa kiwango kikubwa kulinganisha na tafiti zilizofanyika kwa watu mbalimbali nchini Tanzania.

“Pia maambukizi ya damu ya ESBL-PE yalikuwa makubwa kwa watoto waliobeba vijidudu hivyo (asilimia 78.4) ikilinganishwa na wale wasio na maambukizi,” anasema Dk Upendo na kuongeza;

“Kati ya vijidudu 142 vya ESBL-PE asilimia 68 (vijidudu 97) vilionesha usugu kwa dawa ya ciprofloxacin. Utafiti huu pia umebaini kwamba kati ya vijidudu 57 vya enterococci vilivyopatikana kutoka kwa wathirika wa VVU, asilimia 11 (vijidudu 6) ya vijidudu vilikuwa na usugu wa dawa nyingi.”

Dk Kibwana anasema utafiti huo uliokuwa wa maabara, utambuzi na upimaji wa bakteria ulifanyika kwa kutumia kipimo vya kubaini vimelea sugu na vijiumbe pamoja na upimaji mzima wa jeni za vijidudu.

“Lengo la utafiti huu lilikuwa kubaini wingi na ukaribu wa kijenetiki wa vijidudu vya ESBL-PE na VRE, vilivyopatikana kutoka kwa makundi yenye hatari kubwa, yaani watoto chini ya miaka mitano na watu wazima wenye VVU jijini Dar es Salaam,” anasema Dk Kibwana.

Anasema kupitia mapitio ya kimfumo yaliyofanyika, yalionesha asilimia 31.3 ya vijidudu vya mfumo wa mkojo barani Afrika vimeonyesha uhimili kwa ciprofloxacin, huku viwango vya juu zaidi vikiwa kaskazini mwa Afrika (asilimia 55.72).

“Utafiti huu umesaidia kuimarisha maarifa na ushahidi kwa njia ya ufuatiliaji, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kitaifa ya kupambana na janga la usugu wa dawa. Uwepo wa juu wa vijidudu vyenye jeni za uhimili dhidi ya viuavijasumu vingi vinavyotumika katika jamii kwa watoto,” amesema mtafiti huyo.

Tayari utafiti huo umeshachapishwa katika majarida ya kimataifa ya Journal of Global Antimocrobial Resistance, BMC Infectious Diseases na lile la Frontiers Tropical Diseases.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2019 takriban vifo milioni 1.27 vilisababishwa na usugu wa wadudu aina ya bakteria kwa dawa za antibayotiki.

Inakadiriwa kuwa vifo milioni 10 vitatokea kila mwaka duniani ifikapo mwaka 2050 kama hatua za kupambana na tatizo hilo zisipochukuliwa.

Umewahi kujiuliza, mtoto anapopata homa, hasa kupanda kwa joto kuliko kawaida, lakini akifanyiwa vipimo vya damu, mkojo, haja kubwa, malaria, typhoid, amoeba na maambukizi katika njia ya mkojo majibu huonyesha hakuna tatizo, lakini kila mara majibu ya daktari husema ana mchafuko wa damu?

Sayansi inaeleza kuwa maambukizi kwenye damu ‘blood infection’ si ugonjwa bali ni matokeo ya ugonjwa uliopo katika mwili.

Mwili ukiwa na maradhi hujitengenezea kinga yake ambayo ni viwango vya chembe hai nyeupe ili kupambana na maradhi ambazo huongezeka kwenye damu. Ongezeko la chembe hizo ambalo huonekana kupitia kipimo cha damu ni ishara ya uwepo wa ugonjwa mwilini.

Hata hivyo, utafiti mpya uliochapishwa Desemba 9 mwaka jana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ulionyesha vimelea vinavyosababisha maambukizi kwenye damu vimejenga usugu wa dawa kwa zaidi ya asilimia 50, hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa.

Hata hivyo, baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa dawa nyingi za antibaotiki kwa wagonjwa tofauti na kiwango kinachotakiwa kimataifa, huku zile za mstari wa tatu na nne ambazo hazishauriwi, zikitumika.

Hali hiyo imekuwa ikichangia ongezeko la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibaotiki mwilini ‘Antimicrobial resistance AMR’.

Hiyo ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) zilizoonyesha Tanzania imefikia matumizi ya asilimia 88.0 kwa dawa za antibaotiki kinyume na mwongozo uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoelekeza nchi zitumie asilimia 20.0 hadi 26.8.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha makadirio ya usugu wa vimelea dhidi ya antibaotiki ni asilimia 59.8, huku utafiti ukionyesha wengi hutumia antibaotiki bila ushauri wa daktari.

Mfamasia na mkufunzi wa shule ya famasia kutoka Muhas, David Myemba anasema utafiti ulioangazia matumizi ya antibaotiki katika vituo mbalimbali vya afya iwapo wanafuata mwongozo wa matumizi ya dawa hizo uliowekwa na WHO, ulionyesha mapungufu.

“Tulibaini wastani wa wagonjwa wanapewa dawa nyingi tofauti na kiwango kinachotakiwa na kati ya hizo, idadi ya dawa za antibiotiki ni kubwa. Lakini pia tuliangalia zinaandikwaje, iwapo zinaandikwa kwa majina sahihi na kama zipo kwenye mwongozo wa dawa za Serikali,” anasema.

Anasema mwongozo wa WHO unataka dawa anazopatiwa mgonjwa kwa asilimia 100 ziwepo katika orodha ya dawa muhimu, lakini tafiti zilibaini katika vituo vingi zipo chini ya asilimia hiyo.

Anasema mwongozo huo umeainisha dawa kwa mistari minne zipo zinazoshauriwa kutumika, lakini wataalamu wengi wamekuwa wakitumia dawa zisizoshauriwa ambazo ni za mstari wa tatu na nne.

“WHO inashauri dawa za mstari wa kwanza ndizo zitumike na mstari wa pili zinashauriwa zitumike mara chache, mstari wa tatu na nne zisitumike kabisa. Mgonjwa asifike kwa mara ya kwanza na kupewa aina hizo kwa kuwa zina nafasi kubwa ya kujenga usugu.

“Hivyo zikitumika mara kwa mara ni rahisi wadudu au bakteria kupata usugu kwa urahisi na za mstari wa chini zinashauriwa kwa kuwa si rahisi kutengeneza usugu na hizi za mstari wa nne zinaunganishwa mbili kwenye dawa moja, zinatakiwa zisitumike kabisa, lakini tumezikuta zinatumika kwenye vituo vya afya,” anasema.

Myemba anasema dawa hizo zinazuiwa si kwamba zina madhara kuweza kumuua mgonjwa, lakini hazina ushahidi wa kisayansi wa kutosha kwamba ukiunganisha ampicillin na dawa nyingine inaweza kuwa na matokeo zaidi ikilinganishwa na kila moja ikitumika kivyake.

Hata hivyo, anasema sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu ni kwamba zinapochanganywa dawa hizo mbili uwezekano wa kupata usugu ni mdogo.

Anasema tafiti nyingine ambayo Muhas waliifanya wakiangalia matumizi ya antibaotiki kwa watoto wadogo na wataalamu kwa kipindi cha mwaka 2019/2022 wakiangazia vitu vinavyoongeza matumizi ya dawa hizo. Anasema waliangalia upande wa watumiaji ambao ni wazazi, jamii, wataalamu wa afya, wafamasia na madaktari.

“Tulilenga kuangalia kitu gani kinachangia matumizi ya antibiotiki, kinachochangia matumizi sahihi na yasiyo sahihi,” anasema.

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Mugisha Nkoronko, anataja sababu kuu mbili za kuongezeka kwa usugu wa dawa za antibaotiki kuua vimelea vya maambukizi.

“Usugu wa dawa umeongezeka baada ya wagonjwa kununua dawa na kuzitumia bila ushauri wa daktari, utafiti mpya wa WHO unaonesha usugu wa vimelea vya maambukizi umeongezeka zaidi baada ya ujio wa Uviko19,” anasema.

Related Posts