Yanga yapewa njia mpya CAFCL

MATOKEO ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani kutoka kwa Al Hilal kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yameendeleza mkosi ambao Yanga imekuwa nao kwenye mechi za mwanzo za hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika huku makocha wakiwapa njia mbadala.

Mabao ya Adama Coulibaly katika dakika ya 63  na Yasir Mozamil katika dakika ya 90 ya mechi ya Jumanne iliyopita, yameifanya Yanga kutowahi kupata ushindi kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika, mara zote sita ambazo imewahi kushiriki.

Mara ya kwanza kwa Yanga kushiriki hatua hiyo ilikuwa ni mwaka 1998, ilipotinga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mechi ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na Manning Rangers ya Afrika Kusini.

Mwaka huo, Yanga ilimaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi lake ikikusanya pointi mbili.

Yanga ilisubiri tena hadi 2016, ilipoingia katika hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo wa kwanza ilipoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya MO Bejaia ya Algeria na mwaka huo ilimaliza ikiwa nafasi ya mwisho na pointi nne.

Mwaka 2018 ikatinga tena hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na mchezo wa kwanza ikapoteza kwa mabao 4-0 ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Yanga ilimaliza ikiwa na pointi nne na kuishia hatua ya makundi.

Mara ya nne ilikuwa ni msimu wa 2022/2023, ilipofanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mechi ya kwanza ilifungwa mabao 2-0 na Monastir ya Tunisia ingawa msimu huu ilifika hadi fainali ya mashindano hayo.

Msimu uliopita, Yanga ilianza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria lakini hata hivyo ilipambana hadi kufika hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, pamoja na matokeo hayo makocha mbalimbali wamezungumza na Mwanaspoti na kuwapa Yanga chini ya Saed Ramovic mbinu mpya ambayo inaweza kuwasaidia kucheza michezo ijayo na kutinga hatua ya robo fainali.

Mkwassa Yanga inahitaji muda

Kocha wa zamani wa timu hiyo, Boniface Mkwasa amesema Yanga haiwezi kubadilika kwa siku moja au mbili kutokana na uwepo wa benchi jipya la ufundi hivyo, jambo muhimu ni kumuunga mkono kocha aliyepo kwani mazingira aliyotoka ni tofauti na huku.

“Ukiangalia Yanga unaona kabisa ina nyezo zote muhimu kwa maana ya wachezaji bora na benchi nzuri la ufundi ambalo lina uwezo wa kutumia teknolojia za aina mbalimbali, jambo wanalopaswa ni kumsaidia tu ili aingize falsafa zake kikosini.”

Mkwasa alisema, jambo nzuri kwa kocha mpya ni kwamba anaweza kupata msaada wa haraka kwa sababu baadhi ya makocha ambao walikuwa na Miguel Gamondi aliyeondoka wameendelea kubakia ndani ya timu hiyo hivyo, watamsaidia katika makujumu yake.

“Amekuja kipindi kigumu sana na kama unavyojua timu hizi presha yake ni kubwa kuanzia ndani na nje ya uwanja, alisema mwenyewe ni mgeni hivyo, ni lazima wampe muda zaidi kwa kushirikiana na wenzake huku akiingiza falsafa zake taratibu.”

Akizungumzia kiwango cha timu hiyo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Hilal ya Sudan ambao Yanga ilichapwa mabao 2-0, Mkwasa alisema shida kubwa aliyoiona ni kukosa fitnesi kwa wachezaji, jambo lililopelekea kushindwa kuendana na kasi ya mechi.

“Msingi wa mpira wa miguu ni fitinesi kwa mchezaji yeyote, sasa ukiangalia mechi ya Al Hilal wachezaji wa Yanga walikosa hilo ndio maana kila kitu walichokuwa wanakifanya uwanjani kilikuwa kinaenda sana tofauti na matarajio yao,” alisema.

Kwa upande wa Hans van der Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga SC, amesema kuwa timu hiyo inapaswa kurekebisha mambo muhimu ya kiufundi na kiakili kwa wachezaji wake. 

“Wachezaji wanapaswa kukumbushwa thamani yao na nafasi ya klabu katika soka la Afrika. Wanapokuwa na imani zaidi, hata kwenye mazingira magumu, wanaweza kufanya makubwa,” alisema huku akitoa wito kwa benchi la ufundi kuendelea kuwapa hamasa. 

Kocha huyo wa zamani wa Yanga amesisitiza kuwa michezo iliyosalia ni fursa nzuri ya kufuta makosa. Alisema, “Huu ni wakati wa kuchambua upya wapinzani walio mbele na kutumia kila mchezo kuonyesha kuwa Yanga si timu ya kubezwa. Mafanikio hayawezi kupatikana kwa bahati, yanahitaji mipango madhubuti na naamini kama Yanga ikifanya kila kitu vizuri itafika mbali.”

Kocha wa zamani wa Biashara, Kagera Sugar, Francis Baraza amesema Yanga bado ina ubora uleule kinachowaangusha ni fatiki kutokana na wachezaji wake kutumika kwenye mataifa mbalimbali ambao pia ndio wanatumika kikosi cha kwanza.

Pia mbinu wanazotumia makocha tayari wameanza kuwasoma kabla ya mchezo hivyo wanajikuta wanacheza wao lakini wanafungwa.

“Wapinzani wasijaribu kuwabeza na kuingia kichwa kichwa wakiamini kuwa Yanga imeishiwa mbinu na imeshuka kiwango bado wanatimu nzuri na ya ushindani kinachotakiwa kufanyika ni kubadili aina ya uchezaji na kuwaheshimu wapinzani wao,” alisema na kuongeza;

“Nina imani kubwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri licha ya kuanza vibaya wanachotakiwa kufanya ni kutulia na kufanya kazi yao bila kujali nini kinazungumzwa walichokipata ni sehemu ya matokeo bado wana nafasi ya kuwa imara.”

Related Posts