Dar es Salaam. Shirika la ndege Tanzania (ATCL) limerejesha safari zake katika anga la Afrika ya Kusini kuanzia leo Novemba 30, 2024 ikiwa ni baada ya siku 1,881 tangu kusitishwa kwa safari hizo.
ATCL iliyokuwa ikifanya safari zake mara nne kwa wiki ilisitisha rasmi safari zake Oktoba 7, 2019 ikiwa ni baada ya ndege yake aina ya Airbus A220-300 kuzuiliwa katika Uwanja wa Oliver Tambo jiji Johanessburg kwa amri ya Mahakama Kuu ya Guateng, Agosti 23,2019 kabla ya kuachiwa.
Ndege hiyo ilizuiliwa kwa amri ya mahakama kutokana na kesi ya madai iliyokuwa imefunguliwa na Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alikuwa akidai fidia baada ya mali zake zilizotaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.
Akizungumza katika hafla ya kurejea kwa safari Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Peter Ulanga amesema kwa kipindi kirefu baada ya safari za shirika hilo kusitishwa hakukuwa na safari rahisi na rafiki kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini na ujio wake unatibu kilio kilichokuwapo awali kwa waliokuwa wakitaka huduma hiyo ya usafiri.
Kurejesha kwa safari hizo kutaimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili, huku ikiwa ni kichocheo cha kuimarisha biashara ya mizigo barani Afrika na kuboresha huduma kwa abiria wake.
“Safari hizi zitaongeza ufanisi kwani abiria kwani sasa watatumia saa 3:15 katii ya Dar es Salaam na Johannesburg ikilinganishwa na saa 6 hadi 7 walizokuwa wakitumia kwa kupitia nchi mbalimbali, pia safari hizi pia zitaunganisha abiria kutoka mataifa mengine kama Mumbai, Guanzhou, Dubai na abiria wengine wa ndani ya nchi,” amesema Ulanga.
ATCL itakuwa ikifanya safari zake mara tano kwa wiki isipokuwa Jumanne na Alhamisi na itakuwa ikiondoka nchini saa 5 asubuhi.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza ATCL kufanya tathmini ya kina juu ya safari za kimataifa ili kuongeza miruko zaidi kulingana na mahitaji halisi ya soko, tathmini ya kina ya juu ya mkakati wa biashara ili kupunguza gharama za uendeshaji na hasara ili uwekezaji unaofanywa na Serikali ulete tija.
Profesa Mbarawa naye amesema safari hiyo ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji wa sekta ya anga na Uchumi wa Taifa kwa ujumla kwani kutafungua fursa za biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini na kukuza sekta ya utalii.
Profesa Mbarawa amesema pia Serikali itaendelea kutenga fedha za mtaji wa uboreshaji wa ATCL na kuimarisha miundombinu wezeshi ili kutoe huduma ambazo zinaweza kuhimili ushindani wa soko la ndani na kimataifa.
Oktoba 3, 2019, ATCL ilitoa taarifa kwa umma ikitangaza kusitisha safari zake za Johannesburg kuanzia Oktoba 7 mwaka huo ambapo pia iliwaelekeza mawakala wa tiketi wote kurejesha nauli za wateja hao ambao tayari walikuwa wamekata tiketi.
Alipoulizwa na Mwananchi Oktoba 5, 2019 juu ya uamuzi huo, aliyekuwa Mkurugenzi wwa ATCL, Ladslaus Matindi alisema, “Sababu ni hiyohiyo iliyoelezwa awali kama kungekuwa na nyingine tungeeleza na kama kutakuwa na la ziada tutaeleza hapo baadaye kama tulivyoeleza hili. Lakini tunajipanga tukishakuwa vizuri tutarejea,” alinukuliwa.
Awali ATCL ambayo ilikuwa ikifanya safari hiyo mara nne kwa wiki (Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili) iliacha kufanya safari kati ya miji hiyo Agosti 23, 2019 baada ya ndege yake aina ya Airbus A220-300 kuzuiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jiji Johanessburg kwa amri ya mahakama kuu ya Guateng.
Amri ya mahakama ya kuzuia ndege hiyo, ilitokana na kesi ya madai iliyokuwa imefunguliwa na Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alikuwa akidai fidia baada ya mali zake zilizotaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.
Kwa mujibu wa taarifa, Januari 1982 Serikali ya Tanzania ilitaifisha mali za Steyn ikiwemo kampuni ya mbegu ya Rift Valley Seed Company Limited na mali nyinginezo na kufuatia hilo, alikuwa akiidai Serikali Sh373 milioni.
Hata hivyo, takribani wiki mbili baadaye tangu kuzuiliwa, ndege hiyo Agosti 23, 2019 iliachiwa huru kwa uamuzi wa mahakama.
Awali, ilielezwa baada ya kuachiwa kwa ndege hiyo safari zingeanza mara moja lakini siku moja baadaye aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema Serikali imeamua kusitisha safari kwenda katika nchi hiyo kutokana machafuko yaliyokuwa yakiendelea dhidi ya wahamiaji kutoka Afrika (Xenophibia).