Ruangwa. Mkazi wa Mitope, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Justin Galus (33) ameuawa na watu wasiojulikana kisha mwili wake kutelekezwa kwenye bustani za kilimo cha mbogamboga ukiwa na majeraha.
Kando ya mwili huo zimekutwa silaha za jadi na pembeni yake kukiwa na kabichi tatu, zinazodhaniwa huenda alikuwa ameziiba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema juhudi za kuwasaka waliohusika na mauaji hayo zinaendelea na wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Pia, amesema Jeshi la Polisi linalaani vitendo vya baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuwataka wananchi kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Akizungumzia mauaji hayo leo Ijumaa Novemba 29, 2024, Erasmus Libaba aliyeuona mwili huo leo saa 12 asubuhi, amesema aliukuta mwili huo ukiwa na majeraha ya kupigwa na silaha za jadi na pembeni kukiwa na kabichi tatu.
“Ameuawa na watu ambao hadi sasa hawajafahamika. Tunadhani alikuja kuiba kabichi, ndipo akakutana na watu wakamuua na kumwekea kabichi tatu pembeni ya mwili wake,” amesema Libaba.
Hata hivyo, Halima Said, mkazi wa Kijiji cha Mitope, amesema waliposikia taarifa za kufariki kwa Justin, walipata mshangao kwa kuwa hakuwahi kusikia taarifa ya wizi wa kijana huyo.
“Leo niliposikia taarifa ya kifo cha Justin, nimehuzunika sana kwa kuwa sijawahi kusikia taarifa mbaya za huyu kijana, alikuwa ni mcheshi sana kwa kila mtu,” amesema Said.