BEKI wa zamani wa Namungo FC, Derick Mukombozi, raia wa Burundi amemalizana na waajiri wake hao wa zamani kwa ajili ya kuitumikia msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mukombozi amesema amemalizana na Namungo, lakini kuhusu muda uongozi utatangaza amesaini mkataba wa muda gani.
“Nimeitumikia (Namungo) kwa misimu mmoja naifahamu vizuri simuhofii mtu naamini katika upambanaji na nitamuheshimu kila mmoja ambaye nitamkuta ndani ya timu hiyo,” alisema.
“Anaheshimu uwezo wa kila mchezaji aliyepo ndani ya kikosi cha Namungu ameamua kurudi kuungana nao ili waweze kuipambania timu hiyo iweze kufikia malengo.”
Beki huyo baada ya kumaliza mkataba wake na Namungo alirejea nchini kwao Burundi ambapo hakufanikiwa kupata timu hadi sasa alipoamua kurejea tena.
Kurejea kwake kutarudisha utulivu eneo la ulinzi la timu hiyo ambayo haijawa na msimu mzuri kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri wamecheza mechi 11 wameshinda tatu hakuna sare na vipigo nane.
Wakati beki huyo akikana kuthibitisha mkataba wake ni wa muda gani ndani ya Namungo, Mwanaspoti linafahamu kuwa beki huyo wa timu ya taifa ya Burundi amesaini mkataba wa miezi sita.