Bulaya Cup yajivunia kuibua vipaji vya soka ikiingia msimu 14

Michuano ya Bulaya Cup imetajwa kuwa ni sehemu sahihi kwa vijana kuibuliwa vipaji vyao baada ya kufanikiwa kufanya hivyo kwa zaidi ya wanasoka 10 kutoka wilayani Bunda mkoani Mara.

Mashindano hayo yamekuwa yakifanyika katika Jimbo la Bunda Mjini kwa kipindi cha miaka 13 mfululizo.

Akizungumza mjini Bunda leo Jumamosi Novemba 30, 2024 wakati wa uzinduzi wa msimu wa 14 wa mashindano hayo pamoja na mambo mengine, Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya amesema nidhamu pamoja na kujituma ndio siri kuu ya mafanikio kwa wanamichezo.

“Umri wa kucheza ni mfupi sana lakini ukiutumia vizuri unapata mafanikio kwani michezo ni fursa lakini pia ni ajira, sasa ili uweze kupata mafanikio hayo kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa kitaifa na kimataifa suala la nidhamu na kujituma ndio msingi wa kila kitu,” amesema Bulaya.

Amewataja baadhi ya wachezaji ambao wameibuliwa kutokana na mashindano hayo ni Sixtus Sabilo (JKT Tanzania), Lameck Lawi (Coastal Union), Benjamin William (Simba), Daniel Lugoye (Dodoma Jiji).

Wengine baadhi wanaocheza nje ya Tanzania ni Alfonce Mavuka (Serbia), Baraka Majogoro (Afrika Kusini) na Baraka Juma (Kenya).

Amesema katika msimu huu, mashindano hayo yanatarajiwa kutumia zaidi ya Sh40 milioni ikiwa ni gharama za vifaa vya michezo, uendeshaji pamoja na zawadi mbalimbali huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada hizo kwani jimbo hilo lina vipaji vingi lakini vinakosa kuwezeshwa.

Bulaya amefafanua kuwa lengo la mashindano hayo mbali na kuibua  vipaji lakini pia ni kuwakutanisha vijana bila kujali itikadi ya vyama vya siasa huku akisema wakazi wa Bunda ni wapenzi wa michezo na kwamba matamanio yake ni uwepo wa mwendelezo wa shughuli za michezo katika jimbo hilo kwa mwaka mzima.

Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo mbali na kumshukuru mbunge huyo pia wamesema katika kipindi cha miaka 14 kumekuwepo na matokeo chanya hasa kwa vijana kupitia michezo.

“Kuna timu ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Bunda Queens ambayo ipo Ligi Kuu ya Soka Wanawake hapa nchini na wengi wa wachezaji kwenye timu ile wametokana na mashindano haya ya Bulaya cup lakini pia kuna timu ya Bunda Girls ambayo iko Ligi Daraja la Kwanza pia wachezaji wengi pale chimbuko lake ni haya mashindano,” amesema Esther William.

Yohana Timba amesema mashindano hayo ni tafsiri sahihi ya kauli mbiu ya  michezo ni ajira, michezo ni fursa kwani wapo vijana wengi ambao kwasasa wamepata ajira huku wakichezea timu kubwa ndani na nje ya nchi.

“Mtu kuchezea timu kama Simba, JKT au nchini Serbia, Kenya, Afrika Kusini sio jambo dogo, hii inamaana hawa kwasasa wanazihudumia familia zao, ndugu, jamaa na marafiki kupitia michezo,” amesema Timba.

Mashindano hayo yatakayofanyika kwa wiki mbili, yanahusisha michezo ya mpira wa miguu kwa timu 25 za wanaume na tatu za wanawake, mpira wa pete, mpira wa wavu, bao, karata, mbio kwa watu wenye ulemavu pamoja na michezo mingine.

Related Posts

en English sw Swahili