CBE chatakiwa kuwekeza nguvu kwenye programu atamizi

Mbeya. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kushirikiana na taasisi nyingine,  kuwekeza nguvu kwenye programu atamizi na uanagenzi,  kwa lengo la kutekeleza dira ya Serikali ya kuwandaa vijana kukabiliana na soko la ajira.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuibua bunifu za tafiti mbalimbali zitakazosaidia kupata ujuzi na kujiajiri wakiwa vyuoni na maeneo mbalimbali nchini.

Kigahe ametoa agizo hilo leo Jumamosi Novemba 30, 2024 wakati akimwakilisha Spika wa Bunge na mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson katika mahafari 59 ya shahada na astashahada ya chuo cha CBE, kampasi ya Mbeya ambapo wanafunzi 314 wamehitimu.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa vyuo vya elimu ya juu, sasa umefika wakati kuwekeza nguvu kwenye makundi hayo ili kuwajengea uwezo vijana wa kujiajiri,  kwa lengo la kutekeleza mipango mikakati ya Serikali.

“Serikali imeweka mkazo programu hizo kutokana na muhimu wake kwa maendeleo endelevu ya Taifa yatakayowezesha vyuo hivyo kufikia Dira ya Taifa ya miaka 50 na kuwa na tafiti nyingi zenye kuleta matokeo makubwa.

Amesema utekelezaji wa dira hiyo utawezesha taasisi za elimu ya biashara nchini  kuwa  kimbilio kwa kufanya tafiti zenye kuleta matokeo kwa Taifa na Watanzania hususani katika mchakato wa soko la ajira nchini.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa CBE katika kuzalisha wataalamu, ambao watakuwa chachu ya kuchangia uchumi na pato la taifa katika kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda.

Kigahe ameongeza kuwa amefurahishwa kuona CBE kampasi ya Mbeya, ina programu atamizi na uanagenzi ambazo zinawajengea vijana ubunifu na kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga amesema kwa kutambua hilo kwa mwaka 2023/24 walitenga Sh300 milioni na kufanya tafiti 103 za kibiashara, kati ya hizo 16 zimefanywa na kampasi ya Mbeya.

Amesema tafiti hizo zilishirikisha mashirika ya kiserikali 10 na sekta binafsi  kwa kutoa mafunzo ya elimu na biashara,  hali ambayo imesaidia vijana kujifunza stadi za kibiashara nchini.

Profesa Edda amesema sambamba na hilo, pia, wameanzisha programu ya elimu ya biashara katika shule za sekondari, lengo ni kuwaandaa vijana kujiendeleza katika masuala ya ujasiriamali.

Kwa upande wake, mdau wa chuo hicho, Dk Benny Mwenda ametaka wahitimu katika nyanja mbalimbali kutumia mifumo ya teknolojia za kidigital kama njia pekee ya kusaka masoko ya bidhaa ujasiriamali na kuepuka kwenda nje ya maadili ya Mtanzania.

“Maendeleo ya teknolojia lazima yaendane na maadili au uangalizi, tunahitaji vijana wanaoheshimu utamaduni kwa kuzingatia ustawi wa Taifa la Tanzania,’ amesema.

Katika mahafari hayo, jumla ya wanafunzi 314 wamehitimu katika ngazi ya shahada na astashahada, kati yao wanaume 161 na wanawake 153,  ambao watatunukiwa tuzo katika kozi tisa walizohitimu.

Related Posts