DPP awafutia kesi vigogo wa Jiji la Dar, awafungulia nyingine

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amewafutia kesi ya uhujumu uchumi,  watumishi 16 wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kisha kuwafungulia nyingine inayofanana na mashtaka kama ya awali.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka yao 142 waliyokuwa wanakabiliwa yakiwemo ya kuisababishia hasara Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kiasi cha Sh8.9 bilioni na kisha kufunguliwa mengine.

Uamuzi wa kuifuta kesi hiyo umetolewa jana Novemba 29, 2024 na Jaji Sedekia Kisanya wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.

Jaji Kisanya ameifuta kesi hiyo, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hiyo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Achiles Mulisa aliieleza Mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri huyo, hivyo anaomba mahakama iifute na kuliondoa shauri hilo.

Jaji Kisanya baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alisema kama upande wa mashtaka walivyoomba, washtakiwa hao wanafutiwa mashtaka hayo, chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Muda mfupi baada ya kufutiwa kesi hiyo, washtakiwa hao walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Polisi na kisha kupelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo walisomewa mashtaka mapya 138 yanayofanana na yale ya awali.

Hadi kesi hiyo inafutwa jana, tayari mashahidi watano wa upande wa mashtaka walikuwa wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao Mahakama Kuu.

Hata hivyo,  kifungu hicho cha sheria kimempa DPP mamlaka ya kufuta kesi yoyote ya jinai muda wowote ikiwa katika hatua ya kutajwa na kusikilizwa kabla ya kutolewa uamuzi.

Anapotumia kifungu hicho, DPP halazimiki kubainisha sababu wala hawezi kuhojiwa na mtu au mamlaka yoyote.

Washtakiwa hao walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walisomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 138 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia hasara Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kiasi cha Sh8.9 bilioni.

Washtakiwa hao ni Tulusubya Kamalamo (53) Mkazi wa Ukonga na mwenzake  James Bangu (57) Mkazi wa Kibada, ambao wote ni weka hazina wa jiji hilo.

Wengine ni wahasibu wa jiji hilo ambao ni Mohamed  khais (41), Abdallah Mlwale(52), Deogratias Lutataza(55) na karani wa fedha Judica Ngowo (51) maarufu kama Lightness Munis.

Wahasibu wengine ni Febronia Nangwa (44), Glory Eugen(45), Said Bakari, Josephine Sandewa (48), Dorica Gwichala (45) Jesca Lugonzibwa(53) na Alinanuswe Mwasasumbe (60) ambaye ni mkazi wa Mbagala Majimatitu.

Wengine ni Ofisa Afya wa Halmashauri hiyo, Patrick Chibwana (40) Ally Baruani (38) ambaye ni Meneja Mkuu pamoja na Khalid Nyakamande (34)ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Mtaa.

Kati ya mashtaka hayo 138, lipo la kuongoza genge la uhalifu; matumizi mabaya ya madaraka; kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo; ufujaji wa fedha na ubadhirifu; kughushi na kuisababishia hasara mamlaka.

Jopo la mawakili watatu waandamizi wa Serikali, wakiongozwa na Achiles Mulisa, Magreth Mwaseba na Nickson Shayo waliwasomea kesi mashtaka yao mapya 138 kwa kupokezana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Washtakiwa wao wanatetewa na jopo la mawakili saba ambao ni Mwesigwa Muhingo, Emmanuel Hyera, Suleah Tumba, Robert Rutaihwa, Erick Kanga, ⁠Khamis Kijazi na Anthony Massawe.

Kabla ya kusomea mashtaka yao, Hakimu Lyamuya, alisema washtakiwa hao hawatakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi inayowakabili ni ya uhujumu uchumi na Mahakama hiyo, haina uwezo wa kusikikiliza shauri isipokuwa kwa kibali Maalumu.

Hakimu Lyamuya baada ya kueleza hayo, wakili Mulisa alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 33647/ 2024 na kisha kuwasomea mashtaka yao.

Wakili Mulisa alidai washtakiwa wanadaiwa kati ya Julai Mosi 2019 na Juni 6, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh8.9bilioni, mali ya Halmashauri ya Jiji.

Inadaiwa washtakiwa walitenda kosa hilo  kati ya Julai  Mosi 2019 na  Juni 30, 2021 katika ofisi  jijini Dar es Salaam, walijipatia Sh8, 931, 598, 500 kwa njia ya ulaghai mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika shtaka la matumizi mabaya ya madaraka, washtakiwa wote wamedaiwa katika tarehe hizo, katika ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nyadhifa zao mbalimbali, walishindwa kuingiza mapato ya halmashauri ya jiji hilo yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kwenye akaunti za jiji hilo iliyopo katika benki za NMB, CRDB, NBC na DCB na hivyo kujipatia manufaa yasiyo halali na hivyo kuisababishia hasara ya Sh8.9bilioni.

Katika shtaka la kuingiza taarifa za udanganyifu katika mfumo wa kompyuta, washtakiwa hao wanadaiwa siku na eneo hilo, waliingiza taarifa za uongo kuonyesha mapato yaliyokusanywa  katika Jiji la Dar es Salaam, waliingiza mapato hayo katika akaunti ya benki ya NBC, CRDB, NBC DCB, inayomilikiwa na jiji hilo.

Pia wanadaiwa kughushi nyaraka kuonyesha kuwa ni halali wakati wakijua kuwa sio kweli.

Kuhusu shtaka la kuisababishia hasara, washtakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho, wakiwa watumishi wa halmashauri hiyo, kwa makusudi waliisababishia hasara Jiji la Dar es Salama kiasi cha Sh8.9bilioni.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya kusajili nyaraka muhimu Mahakama Kuu.

Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana kiasi wanachotuhumiwa nacho, Mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana isipokuwa Mahakama Kuu.

Kwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa wanaweza kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Mahakama ya Kisutu, Juni 26, 2023 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 32/2023 yenye jumla ya mashtaka 142.

Hata hivyo, Julai 6, 2024 washtakiwa hao walisomewa maelezo na mashahidi na vielelezo,  baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika na Serikali ilisema inatarajia kuita mashahidi 71 na vielelezo 370.

Related Posts