Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yapungua

Songea. Hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, inaonyesha matumaini baada ya kupungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia saba mwaka 2022.

Pia, kiwango cha ushamiri wa maambukizi ya VVU,  imepungua kutoka asilimia saba mwaka 2003/04 hadi asilimia 4.4 mwaka 2022/23.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa viashiria vya matokeo ya Ukimwi ya mwaka 2022/23 mkoani Ruvuma.

Amesema kinachoendelea kufanyika sasa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ni utoaji elimu, upunguzaji wa maambukizi, ushawishi na ubadilishaji wa tabia za jamii.

“Napenda kutoa rai kuwa suala la usambazaji wa taarifa hiyo liende sambamba na uelimishaji umma kwa makundi na rika zote ili kuhakikisha hakuna mtu, kikundi au wadau wanaoachwa nyuma katika mapambano haya,” amesema Jenista.

Ametaka mapambano dhidi ya Ukimwi yawahusishe kwa karibu viongozi wa dini, kimila, wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari, viongozi wa kisiasa na wazee maarufu.

Wengine amesema ni watu wenye ushawishi katika jamii husika na wadau wote katika ngazi zote nchini katika kusambaza na kufikisha ujumbe wa matokeo yanayotokana na ripoti ya utafiti huo.

Lengo ni kuweka mikakati mipya, amesema ni kutokomeza unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi na kutoa elimu kuhusu masuala yote yanayohusu ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA), Deogratius Rutatwa amesema utafiti uliofanyika umewapa fursa waathirika kushiriki.

Amesema ushiriki huo umehusisha kutoa maoni yao kwa Serikali na kuwezesha kupata takwimu muhimu katika kuandaa mipango na maboresho ya sera, mikakati na miongozo katika kufanya uamuzi na maandalizi ya programu mbalimbali za VVU na Ukimwi nchini.

Amesema taarifa hiyo ni nyenzo ya kimkakati kwa waviu na Watanzania katika kuwawezesha kupata taarifa zinazohusiana na changamoto mbalimbali.

‘’Utafiti umeweka mazingira wezeshi kwa waviu na Watanzania kwa ujumla kushiriki katika kutoa maoni yao kwenye mipango na mikakati mbalimbali, kwa lengo la kuboresha shughuli za mwitikio wa Ukimwi katika ngazi mbalimbali na makundi mbalimbali kijamiii na kitaifa pia,’’ amesema Rutatwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Ukimwi (UNAIDS), Dk Martin Odiit amesema wanaunga mkono juhudi za kitafiti kukabili Ukimwi.

Amesema utafiti huo utasaidia kutoa mwanga wa kupambana na maambukizi kwa vijana na wananchi wote wa Tanzanzia na kujenga taifa lenye watu wenye afya njema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile amesisitiza umuhimu wa kufanywa tafiti za kujua kiwango cha maambukizi katika mikoa ya mipakani.

Related Posts