Morogoro. Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa BSM Washauri Tanzania Limited, Bakari Machumu amewapa mbinu tano wahitimu wa kozi ya uandishi wa habari zitakazowasaidia kupata mafanikio katika taaluma hiyo hasa katika kipindi hiki cha teknolojia.
Machumu ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), ametoa mbinu hizo akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 28 ya Chuo cha Uandishi wa Habari Morogoro (MSJ), yaliyofanyika leo Novemba 30, 2024.
Baadhi ya mbinu alizozitaja mkurugenzi huyo ni pamoja na kuwa tayari kujifunza na kubadilika kulingana na ulimwengu wa sasa unavyotaka kwani teknolojia imebadilika.
Mbinu nyingine aliyowapa wahitimu hao ni kuchagua maeneo maalumu ya kitaaluma ya kufanyia kazi na kuwa wabobevu katika maeneo hayo, kwa kuwa hilo litawafanya watambulike kwa umahiri wao na kuwa wa kipekee.
Machumu amewataka wahitimu hao wasiwe watu wa kujilaumu hasa pale wanapokosea badala yake wabadilike na kufanya bidii kwa kile wanachoamini kuwa kitawasaidia kitaaluma.
“Fani ya uandishi wa habari sio kazi ya kutumia nguvu kubwa ya msuli kama ilivyokuwa kazi ya kubeba mizigo, bali ni kazi ya kutumia akili na ubunifu, hivyo pamoja na mbinu nilizowapa, suala la nidhamu ni muhimu, nidhamu ya kazi na hata nidhamu ya maisha,” amesema Machumu.
Amesema mbinu nyingine ya kufanikiwa katika kazi ya uandishi wa habari ni kuepuka kuwa nguvu ya soda, bali wafanye kazi kwa uendelevu huku wakiamini kile wanachofanya.
Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Suzana Msosi amesema chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1995, kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 330 ambapo mpaka sasa kimefundisha waandishi wa habari 5,400 ambao wapo kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini.
“Katika mahafali haya, jumla ya wanafunzi 190 wamehitimu kozi ya uandishi wa habari kwa ngazi mbalimbali ngazi ya cheti, stashahada na kozi fupi,” amesema Ndosi.
Wakati huohuo, mkuu huyo wa chuo amesema chuo hicho kimeanzisha kozi mpya ya mawasiliano kwa umma na masoko, hivyo amewataka wazazi na walezi kuwapeleka vijana wao katika chuo hicho ili wasome.
Mmoja wa wahitimu wa kozi ya uandishi wa habari, ngazi ya stashahada, Hussein Pori amempongeza mgeni rasmi kwa kuwapa mbinu za mafanikio, kwani taaluma ya uandishi wa habari kwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kitaaluma.
“Ulimwengu umebadilishwa na teknolojia, uandishi wa habari wa miaka ya nyuma ni tofauti na uandishi wa sasa. Teknolojia imechukua nafasi kubwa, hivyo haya aliyotueleza Machumu yatatusaidia wakati tunatafuta ajira au tukiwa tumejiajiri,” amesema.