Magonjwa 10 yanayoongoza mkoani Dodoma

Dodoma. Imebainika kati ya  magonjwa 10 yaliyoongoza kwa watu wengi kuugua mkoani Dodoma katika kipindi cha miaka miwili mfululizo,  maambukizi ya njia ya juu ya kupumua (URI), yamechukua nafasi ya kwanza.

Magonjwa mengine yaliyoongoza katika mwaka 2021 na mwaka 2022 yalikuwa ni maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), Nimonia, kuhara, magonjwa mengine ya tumbo yasiyoambukiza.

Mengine ni maambukizi ya ngozi, shinikizo la damu, vidonda vya tumbo, mashimo katika meno na minyoo ya tumbo.

Hayo yamo katika kitabu cha pato la Mkoa wa Dodoma, Wasifu wa Kiuchumi na Kijamii kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Rais ya Mipango na Uwekezaji.

Matokeo yanaonyesha kwamba kati ya wagonjwa 894,648 waliorekodiwa mwaka 2021, asilimia 85.26 walikuwa wakisumbuliwa na mojawapo ya magonjwa matano ya kwanza.

“Hii inamaanisha kuwa idadi kubwa ya wagonjwa walikuwa wanaugua mojawapo ya magonjwa yaliyotajwa kwenye orodha ya kwanza, ambayo ni URI, UTI, nimonia, kuhara, au magonjwa mengine yasiyoambukiza ya mfumo wa utumbo,”kimesema kitabu.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, takwimu za afya za wagonjwa wa nje kwa mwaka 2021 zilionyesha kwamba URI ilishika nafasi ya kwanza kama chanzo kikuu cha magonjwa na kufuatiwa na UTI na kisha nimonia.

Akizungumza na Mwananchi, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema kunahitaji kudhibiti na kuzuia magonjwa hayo na mengine.

“Elimu kwa umma ndio msingi wa mapambano dhidi ya maradhi hayo, itakayosaidia kudhibiti magonjwa hayo. Elimu ilenge kutambua dalili na maelekezo ya namna ya kupata matibabu,” amesema.

Amesema jambo jingine la kufanya ni kuendelea kuwekeza kwenye uwezo wa vipimo vya kitaalamu, kupata majibu ya uhakika na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Dk Nkoronko amesema jingine ni ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ili kuchagiza jitihada za udhibiti wa maradhi na kuongeza ubunifu na jitihada za  utafiti  wa magonjwa na matumizi ya matokeo ya tafiti.

Pia, kuhamasisha ugharamiaji wa matibabu kabla ya kuugua kupitia skimu  za bima ya afya.

Mmoja wa wakazi wa Dodoma, Juliana Kambona amesema upatikanaji wa maji unachangia magonjwa hayo kuwa kwa kiwango kikubwa.

“Kuna maeneo mengi bado wanatumia maji ya visima vifupi na wakati mwingine sio salama kabisa kwa maisha ya watu, hayo hayo wanakunywa, hayo hayo wanafanyia shughuli za usafi ni ngumu kuepuka magonjwa,”amesema.

Ameomba Serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo ya pembezoni ili kuwasaidia watu wanaokabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama.

Related Posts