Dar es Salaam. Wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikitimiza miaka 25 tangu iliporejeshwa mwaka 1999, baadhi ya wakuu wa nchi wanachama wamependekeza tafakari pana ya kubaini kama nchi wanachama zinafaidika vya kutosha na fursa zilizopo ndani ya jumuiya hiyo.
Hayo yameelezwa leo, Novemba 30, 2024, katika mkutano wa 24 wa wakuu wa nchi wanachama wa EAC, ambapo Rais wa Kenya, William Ruto, amekabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi hicho, bado jumuiya hiyo inapaswa kutafakari kama uchumi wa nchi wanachama unafaidika vya kutosha na fursa zilizopo.
“Moja ya mafanikio ya jumuiya yetu ni kupanuka kutoka nchi tatu hadi nane. Tuna kila sababu ya kuona fahari kwa hatua hii, lakini tunapaswa kujiuliza kama chumi zetu zinafaidika vya kutosha na fursa zilizopo ndani ya ukanda wetu, kiasi cha kufurahia kutanuka kwetu. Hayo ni mambo tunatakiwa kuyazungumza ndani ya jumuiya na kuweka mikakati ili tuweze kufaidika vyema na ipasavyo,” amesema.
Suala hilo la fursa pia lilizungumziwa na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombanza, kuwa miaka 25 ni hatua kubwa inayostahili kusherehekewa, lakini pia ni wakati wa kutafakari kama jumuiya imefanikiwa kufikia malengo yake.
“Ni hatua muhimu sana ya kututaka tukue, sio kukua tu kwa kimo bali pia kwa ufanisi. Kwa kuzingatia kaulimbiu yetu ya kuimarisha biashara, maendeleo endelevu, amani na usalama, tunapaswa kuboresha maisha ya watu wetu,” alisema.
Vilevile, hoja hiyo iligusiwa na Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mahmoud, kuwa kuongezeka kwa wanachama ni moja ya mafanikio makubwa ya jumuiya na kuwa Somalia imechukua hatua za kuendana na malengo ya EAC.
“Tangu tumejiunga, Somalia imechukua hatua madhubuti kuendana na malengo ya jumuiya, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa soko la pamoja, umoja wa forodha, itifaki ya fedha, na shirikisho la siasa,” alisema.
Mapema, baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais wa Kenya William Ruto alisema atatoa kipaumbele katika kuhakikisha EAC inatekeleza maono yake ili kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
“Katika kipindi changu, nitatoa kipaumbele katika kuboresha maisha ya wananchi wa jumuiya yetu. Tutajikita katika kuongeza ushindani wa uzalishaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani, kukuza biashara za mipaka, na kuongeza uwekezaji,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kutimiza wajibu wao wa kutoa michango ili kuhakikisha sekretarieti ya EAC ina rasilimali za kutosha kutekeleza majukumu yake.
“Nawaomba viongozi wa nchi wanachama kutimiza wajibu wao wa kutoa michango na kuhakikisha upatikanaji wa fedha katika jumuiya. Hii itahakikisha sekretarieti ya EAC ina rasilimali za kutosha na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yake,” alisema.
Pamoja na masuala mengine, Waziri wa Sheria wa Rwanda, Justice Emmanuel Ugirashebuja, alieleza changamoto mbili zinazoikabili jumuiya hiyo, ikiwa ni pamoja na nchi wanachama kutotoa michango yao.
Waziri hiyo aliyemwakilisha Rais Paul Kagame, aliomba hatua kali zichukuliwe kuhakikisha michango inatolewa.
“Tunahitaji hatua madhubuti za kuhakikisha tunatimiza malengo yetu. Hatua hizo ni pamoja na zile zilizowekwa na Umoja wa Afrika, ambazo zimewezesha kuleta mafanikio kwa wanachama,” alisema bila kuzifafanua.
Waziri huyo alikosoa hatua ya majeshi ya Afrika Mashariki kujiondoa katika operesheni za kulinda amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akisema inakiuka maagizo ya viongozi wa jumuiya.
“Hatua hii ya kumaliza mamlaka ya kijeshi inakiuka agizo la pamoja la wakuu wa nchi wanachama. Hii imeleta usumbufu, imeondoa imani, uwazi na uwajibikaji pamoja na maana ya ushirikiano,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametumia kikao hicho kumpongeza Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, mmoja wa marais watatu waliorejesha jumuiya hiyo mwaka 1999 baada ya ile ya awali kuvunjika mwaka 1977, kwa mchango wake mkubwa ndani ya jumuiya.
“Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, wazee wetu, Rais Yoweri Museveni, Hayati Daniel Arap Moi na Hayati Benjamin Mkapa, ambaye alipokea maono kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi, walikusudia kurejesha maono ya viongozi waasisi kwa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mheshimiwa Museveni amekuwa mwalimu, msuluhishi na muunganishi wetu ndani ya jumuiya; tunapotaka kukengeuka, anaturudisha katika misingi ya jumuiya,” alisema Rais Samia.