Muya akiri mambo magumu Fountain Gate

Muya akiri mambo magumu Fountain Gate LICHA ya Fountain Gate kuwa moja ya timu zenye safu kali zaidi za ushambuliaji msimu huu wa Ligi Kuu Bara, changamoto ya kuruhusu mabao mengi imeendelea kuwa mwiba kwao.

Hali hiyo imeongeza presha kwa kocha Mohammed Muya aliyekiri kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanarejea kwenye mstari wa ushindi. 

Fountain Gate, ambao wanatoka Babati walikuwa na mwanzo mzuri wa msimu, lakini katika michezo minne iliyopita mambo yamekuwa magumu.

Timu hiyo imepoteza michezo mitatu dhidi ya JKT Tanzania (1-0), Pamba Jiji (3-1) na Singida Black Stars (2-0), huku wakilazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mashujaa FC. 

Kwa sasa, Fountain Gate wameshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 17, wakijivunia mabao 20 yaliyofungwa idadi ambayo ni ya pili baada ya Simba yenye mabao 22.

Hata hivyo, tatizo linabaki katika safu ya ulinzi, kwani wamefungwa mabao 21, idadi sawa na KenGold, timu inayoshika mkia wa ligi. 

Akizungumza kuhusu changamoto hiyo, Muya alisema: “Ni wazi tuna tatizo kwenye ulinzi na kama benchi la ufundi tunalifanyia kazi kwa nguvu. Tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini kuruhusu mabao mengi kunarudisha nyuma juhudi zetu. Tumejifunza kupitia michezo hii na naamini hali itakuwa tofauti katika mechi zijazo.” 

Kocha huyo ameonyesha matumaini kwamba timu yake itarejea kwenye wimbi la ushindi, “nina imani kubwa na wachezaji wangu. Tunahitaji nidhamu zaidi, haswa katika dakika muhimu za mchezo. Mashabiki wetu wasikate tamaa; tuko tayari kuwaletea furaha tena.”

Mchezo unaofuata wa Fountain Gate katika ligi utakuwa dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Desemba 13 baada ya kucheza na Mweta Sports kwenye kombe la FA mwanzoni mwa mwezi huu. Mshambuliaji wao nyota, Seleman Mwalimu ambaye anaongoza kwa mabao (6), anatarajiwa kuendelea kuwa silaha muhimu kwa timu hiyo. 

Related Posts