Mvua kubwa kunyesha mikoa 14, Dar yapewa angalizo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa angalizo la uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo machache ya mikoa 14 nchini.

Hayo yamo katika taarifa ya utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3.00 usiku wa leo Jumamosi Novemba 30, 2024.

TMA imetoa angalizo la vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa katika maeneo machache ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe),

Pia maeneo machache ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Angalizo hilo pia linahusu maeneo machache ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara), na Kanda ya Kati (mikoa ya Dodoma na Singida).

TMA katika taarifa hiyo imesema mikoa ya Ruvuma, Singida na Dodoma, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro; mikoa ya Rukwa, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe itakuwa na hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika baadhi ya maeneo na vipindi vifupi vya jua.

Mamlaka imesema Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba; mikoa ya Dar es Salaam na Pwani (ikijumuisha Visiwa vya Mafia) kutakuwa na hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vifupi vya jua.

Taarifa ya TMA imesema mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Arusha, Kilimanjaro Manyara, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu itakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.

Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, TMA imesema kutakuwa na hali ya mawingu, mvua katika maeneo machache na vipindi vifupi vya jua.

Kuhusu upepo wa Pwani, mamlaka hiyo imesema unatarajiwa kuvuma kutoka Kusini Mashariki kwa Pwani yote kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa kwa Pwani ya Kaskazini na kwa kasi ya kilomita 40 kwa saa kwa Pwani ya Kusini.

TMA imesema hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi madogo hadi makubwa. “Matarajio kwa Jumatatu Desemba 2, 2024 ni mabadiliko kidogo,” imesema TMA.

Related Posts