Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani katika kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, moja ya vitu vinavyotajwa kuchochea ukatili huo ni ndoa za utotoni.
Miongoni mwa changamoto zinazotokana na ndoa za utotoni ni unyanyasaji wa kimwili, ikizingatiwa wanaoolewa kuna nyakati hukumbana na vipigo na mateso kutoka kwa wenza wao na hata ndugu, hivyo kukiuka haki zao za msingi.
Si hayo pekee, ndoa hizi husababisha ukatili wa kijinsia wa kihisia na kisaikolojia. Watoto wanaolazimishwa kuingia kwenye ndoa mara nyingi wanakosa uwezo wa kujieleza, kushiriki maamuzi ya familia, au kudai haki zao. Wanapozuiliwa kujieleza, wanapewa jukumu la kuwatunza watoto au familia wakiwa bado hawajakomaa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.
Pia husababisha unyanyasaji wa kiuchumi, watoto hukosa fursa ya kupata elimu na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Kukosa elimu na fursa za kiuchumi kunawaweka katika hali ya utegemezi wa kifedha kwa waume zao, hivyo kusababisha hatari ya kunyanyaswa kijinsia kwa kutokuwa na uwezo wa kujitegemea.
Ni kutokana na ndoa hizi, watoto huathiriwa kwa kuzaa mapema kabla miili yao haijakomaa, hali ambayo huongeza hatari ya matatizo ya kiafya kama vile fistula, kifafa cha mimba na hata vifo vya uzazi.
Ndoa za utotoni huwanyima wasichana nafasi ya kujenga mahusiano yenye usawa, badala yake, wanajikuta wakitumikishwa nyumbani, na kubaguliwa.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya
Malaria Tanzania (TDHS-MIS) mwaka 2022, asilimia 20.3 ya Watanzania wenye miaka 15-19 wameolewa, wanaishi pamoja au walikwisha kuwa kwenye mahusiano na wametengana. Kati ya walioolewa wa umri huo asilimia 30.6 wanandoa zilizosajiliwa na wana vyeti.
Vilevile takwimu hizo zinaonyesha wanawake wenye miaka 25-49 waliolewa wakiwa na wastani wa miaka 19.8.
Utafiti unaeleza elimu na hali ya umasikini vinachangia kwa kiwango kikubwa, kwani wastani wa umri wa wanawake wasio na elimu na ni masikini kuolewa ni miaka 18.1 ukilinganisha na wale waliohitimu sekondari au elimu ya juu walioolewa na miaka 23.7.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha wanawake huanza kujihusisha na ngono miaka mitatu kabla ya kuolewa wakiwa na wastani wa miaka 17 na wanaolewa wakiwa na miaka 19.8.
Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa na maoni mbalimbali yanayopingana na ndoa za utotoni.
Padri Longino Rutangwelera anasema Kanisa Katoliki haliungi mkono ndoa hizo, akieleza maana ya ndoa katika mustakabali wa dini.
Padri Rutangwelera anasema katika dini ndoa ni maagano ya watu wawili waliokomaa kimwili na kiakili na si vinginevyo.
“Ndoa ina wajibu wake, misingi na haki zake inamtaka mtu awe na ukomavu wa kiakili na kiimani pia, unapomlazimisha msichana kuingia kwenye ndoa za utotoni unapingana na uhalisia,” anasema.
“Kumuoza binti ambaye hajakomaa kiakili, kimwili na kifikra ni kupingana na matakwa na mapenzi ya Mungu na kupingana na uhalisia.
“Unapomlazimisha mtoto kuingia katika ndoa anakosa elimu na kuingizwa kwenye makubaliano ambayo kwa akili na ukomavu wake hana uelewa wa kutosha, hivyo atapata watoto wakati uwezo wake wa kuwa mama au baba hautoshi, ni vema wakaachwa hadi wawe wakomavu, kimwili, kiakili na kihisia ili kupokea majukumu hayo kikamilifu,” anasema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema kuna umuhimu wa kutenda uadilifu kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa kiume na wa kike, ikiwamo suala zima la kupata elimu kwa kadri ya uwezo wao.
“Hata hivyo, bado kuna changamoto kwa mtoto wa kike, ikiwamo ya kuozwa katika umri mdogo na kukosa haki yake ya kielimu.
“Ninachokitamani ili kuondoa ukatili huu, kuwepo sheria ambayo itamsaidia mtoto wa kike kutoingia kwenye ndoa za utotoni,” anasema.
Akifafanua kuhusu Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Sheikh Mataka anasema imeweka kidato cha nne kuwa ni elimu ya lazima.
Kiongozi huyo anasema kama sera itaongezwa na kudadavua kwamba elimu ya lazima iwe kidato cha sita, itamsadia mtoto wa kike.
“Hadi atakapohitimu kidato cha sita, huyu mtoto atakuwa amefikisha miaka 17 hadi 18, katika umri huu changamoto cha ndoa za utotoni itakuwa imeondoka,” anasema.
Anasema Sheria ya Ndoa namba 5 ya mwaka 1971 nayo itamke mwanafunzi wa elimu ya lazima haruhusiwi kuoa wala kuolewa na Sheria ya Elimu namba 5 ya mwaka 1978 iseme mtoto haruhusiwi kuoa wala kuolewa hadi ahitimu elimu ya lazima, hivyo itasaidia kuwalinda watoto wa kike.
“Atakapohitimu elimu ya lazima atakuwa amepata ukomavu ambao hata akiolewa atakuwa na uwezo wa kulea familia,” anasema.
Mchugaji Monica Lugome wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani anasema ajenda kubwa ya kumlinda mtoto wa kike na ndoa za utotoni ni kutoruhusu aolewe chini ya miaka 18.
Anasema anapoolewa chini ya umri huo ni mateso kwake na hata vitabu vya dini haviruhusu hilo.
“Biblia inatuagiza kumlea mtoto katika njia impasayo ikiwamo kuhakikisha anapata haki zake katika nyanja zote ikiwamo elimu. Unapomuoza katika umri mdogo ni kumnyima haki yake ya msingi,” anasema Mchungaji Monica.
Taasisi ya kimataifa ya Norwegian Church Aid iliandaa mjadala wa kitaifa kujadili umri sahihi wa kuoa au kuolewa, uliowahusisha wadau mbalimbali kutoka mikoa 10 nchini.
Msimamizi wa miradi wa taasisi hiyo Tanzania, Sarah Shija anasema mjadala huo uliofanyika Novemba 28, ulilenga kukosoa na kushauri kuhusu changamoto zinazosababisha ukatili wa kijinsia.
“Hii itasaidia kuleta mabadiliko, kuna makundi kama viongozi wa dini yana nafasi na ushawishi katika mabadiliko ya kisheria, hususani kwenye umri wa binti kuolewa na madhara ya ndoa katika umri mdogo,” anasema.
Rebeca Gyumi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative anasema pamoja na mambo mengine, mjadala huo pia umeangalia uzoefu wa nchi mbalimbali kwenye masuala ya mabadiliko ya umri wa ndoa.
Rebeca aliyefungua kesi za kikatiba kupinga vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vilivyotoa mwanya kwa watoto wa kike kuolewa wakiwa na umri wa miaka 14 kwa kibali cha Mahakama na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi, anasema mchango wa viongozi wa dini ni mkubwa ili kufikia lengo la kutokomeza ukatili wa kijinsia, hususani ndoa za utotoni.
Rachel Boma, kutoka Shirika la UN Woman Tanzania anasema nchi mbalimbali zimefanya mabadiliko ya kisheria na kuweka umri wa ndoa kuwa miaka 18.
“Nchi kama Indonesia au Misri ambazo mfumo wao wa sheria ni kama kwetu, Serikali ziliona mabadiliko katika sheria zao na wao umri wa kuolewa ni miaka 18, hivyo katika mijadala kama hii tuna vitu vingi vya kujifunza kutoka kwa wenzetu.
Akizindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema Serikali itayajadili maombi yote yaliyotolewa na mtandao wa kupinga ukatili wa kijinsia (Mkuki) ikiwamo suala la kutunga sheria mahususi ili kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia na kuyatokomeza.
Alisema watakaa pamoja kuyajadili ili kuona namna gani hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa.
”Katika sheria zetu mbalimbali tuna sheria nyingi zinazopinga ukatili wa kijinsia na zinaelezea masuala hayo na kutoa adhabu kali ikiwemo Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 mkiisoma sheria hiyo imeelezea ukatili katika maeneo mengi,” alisema.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa Novemba 23 itafikia tamati Desemba 10. Kaulimbiu ni ‘Kuelekea miaka 30+ ya Beijing, Chagua kutokomeza ukatili.’
Kaulimbiu hiyo inawakumbusha watu kujitafakari na kitathmini yale yanayofanywa kama yana tija.
Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dk Monica Muhoja anasema kuna haja ya kutungwa sheria maalumu kupinga ukatili wa kijinsia.
“Mwaka huu tumekuja na maombi mengine ikiwamo kufika kwenye ajenda za kiusalama kuhakikisha masuala ya ukatili wa kijinsia yanaingizwa rasmi katika mipango na mikakati ya kiusalama ya kitaifa,” alisema.
Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya alisema dhamira ya kampeni hiyo ni kushawishi na kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo inayochochea unyanyasaji na ukandamizaji wa kijinsia huku ikikuza usawa, heshima na haki kwa wote.