KOCHA Msaidizi wa Namungo, Shadrack Nsajigwa amewakumbusha wachezaji wa sasa wa Taifa Stars kupambana kwa ajili ya nchi akirejea kumbukumbu tamu ya 2010 walipoiwezesha Bara kutwaa ubingwa wa Kombe la Cecafa.
Ushindi huo uliweka alama ya kipekee kwenye soka la Tanzania, ambapo Stars iliifunga Ivory Coast bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar.
Nsajigwa ambaye alikuwa nahodha wa kikosi hicho, amesema mafanikio hayo hayakutokea kwa bahati, bali yalitokana na nidhamu, mshikamano wa timu na kujituma kwa wachezaji. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni somo kwa kizazi cha sasa cha wachezaji kuhakikisha wanajituma zaidi ili kufanikisha ndoto za Watanzania.
“Ilikuwa fursa ya kipekee kuongoza kikosi cha Taifa Stars wakati huo. Ushindi dhidi ya Ivory Coast ulikuwa wa kihistoria na naliona hilo kama somo kubwa kwa wachezaji wa sasa. Wanapaswa kupambana kwa bidii ili kuacha alama katika historia ya soka la Tanzania,” alisema.
Tanzania Bara ambayo ilikuwa Kundi A katika michuano hiyo ilianza safari yake kwa kuvuna alama sita katika hatua ya makundi. Ilimaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Zambia waliokuwa na alama saba. Robo fainali ilikuwa kipimo cha nguvu, ambapo Stars iliifunga Rwanda bao 1-0 kabla ya kukutana na Uganda katika nusu fainali. Mechi hiyo ilikwenda hadi mikwaju ya penalti baada ya suluhu na Stars kushinda penalti 5-4.
Fainali dhidi ya Ivory Coast iliikutanisha Bara na wageni hao waliokuwa wameonyesha kiwango cha wakiwafunga Ethiopia bao 1-0 katika nusu fainali.
“Ilikuwa Desemba 12, 2010, siku ya kihistoria kwa Tanzania. Nilifunga bao la penalti, lakini siyo juhudi zangu pekee ilikuwa ni kazi ya pamoja ya wachezaji wote. Mashabiki walikuwa nyuma yetu,” alikumbuka Nsajigwa.
Licha ya mafanikio hayo Nsajigwa ameonyesha masikitiko kwamba tangu mwaka huo Bara haijawahi tena kutwaa ubingwa wa Cecafa. Hata hivyo alipongeza kizazi hiki kufuzu mara ya nne katika Afcon mwakani huko Morocco.