Tanzania yaipiku Kenya bidhaa zinazoingizwa Uganda, Ruto apongeza

Dar es Salaam. Tanzania imeipiku Kenya kama chanzo kikubwa zaidi cha bidhaa za Uganda, ikionesha mabadiliko katika biashara, hasa ndani ya Afrika.

Kwa muda mrefu Kenya imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Uganda, lakini taarifa zinaonyesha kwamba nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, sasa iko nafasi ya pili baada ya Tanzania kwa kuwa chanzo kikubwa cha bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka ndani ya Afrika.

Katika ripoti ya Novemba 2024 iliyotolewa na The Citizen, imeonyesha kuwa Tanzania imeipiku Kenya kama chanzo kikubwa zaidi cha bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka Afrika.

Takwimu za Benki ya Uganda zinaonyesha kuwa katika mwaka ulioishia Juni 2024, Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola 4.17 bilioni (Sh10.98 trilioni) kutoka Soko la Pamoja na Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na sehemu nyingine za Afrika, ambapo karibu nusu ya bidhaa hizo zilikuwa kutoka Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), Uganda huagiza dhahabu, chuma cha pande zote au chuma kisichochanganywa, karanga na chupa kutoka Tanzania.

Dhahabu inachangia zaidi ya nusu ya bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka Tanzania. Takwimu za URA zinaonyesha kuwa Uganda iliagiza dhahabu yenye thamani ya Shs1.08 trilioni mwaka 2023.

Data zinaonyesha kuwa asilimia 42.56 ya bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka ndani ya Afrika katika mwaka ulioishia Juni 2024, zilikuwa kutoka Tanzania, ikilinganishwa na asilimia 19.55 kutoka Kenya na asilimia 6.43 kutoka Afrika Kusini.

Ivory Coast na Burkina Faso zilimaliza orodha ya vyanzo vikubwa vitano vya bidhaa zinazoingizwa Uganda ndani ya Afrika, zikichangia asilimia 5.27 na asilimia 5, mtawalia.

Benki ya Uganda inaonyesha zaidi kuwa katika mwaka ulioishia Juni 2024, Uganda ilitumia zaidi ya Sh4.66 trilioni kuagiza bidhaa kutoka Tanzania, zaidi ya mara tatu ya zaidi ya Sh1.18 bilioni) iliyorekodiwa mwaka ulioishia Juni 2023.

Kenya, ambayo kwa miaka mingi imekuwa chanzo kikuu cha bidhaa za Uganda barani Afrika, sasa ipo nafasi ya pili, ikichangia zaidi ya Sh2.15 trilioni, ambayo ni punguzo kidogo kutoka zaidi ya Sh2.26 trilioni) iliyorekodiwa mwaka ulioishia Juni 2023.

Kenya inafuatiwa na Afrika Kusini yenye bili ya bidhaa za zaidi ya Sh708 bilioni, likiwa ni ongezeko kutoka zaidi ya Sh480.55 bilioni, huku bidhaa kutoka Ivory Coast na Burkina Faso zikionyesha ongezeko kubwa, kutoka zaidi ya Sh39.19 bilioni hadi zaidi ya Sh580.38 bilioni na zaidi ya Sh132.15 bilioni hadi zaidi ya Sh550.22 bilioni mtawalia.

Uganda kwa kiasi kikubwa huagiza saruji, chuma cha pande zote au chuma kisichochanganywa, mafuta ya petroli, mabaki ya vyuma, na plastiki kutoka Kenya, huku kutoka Afrika Kusini ikiagiza hasa lulu, vito vya thamani, metali, sarafu, magari, chuma na mashine mbalimbali.

Bidhaa kutoka Ivory Coats na Burkina Faso ni pamoja na vipodozi, magari makubwa ya ujenzi, sabuni na plastiki.

Nje ya Afrika, China ni chanzo kikuu cha bidhaa za Uganda, ikichangia bidhaa zenye thamani ya $1.93 bilioni (zaidi ya Sh5 trilioni) asilimia kubwa zikiwa ni vifaa vya mawasiliano, chuma cha moto kilichoviringishwa, vipuri vya mashine, viuatilifu na nyinginezo.

China inafuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zaidi ya Sh2.5 trilioni na India zaidi ya Sh2.37 trilioni.

Ruto apongeza, Wakenya wamshukia

Kufuatia hatua hiyo,  Rais William Ruto ameisifu Tanzania alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha Novemba 29, 2024, akikiri kupungua kwa nafasi ya Kenya kama kinara wa biashara ya kanda na kupongeza maendeleo ya Tanzania.

“Ninapongeza Tanzania kwa kuipiku Kenya katika bidhaa na huduma tunazofanya biashara ndani ya Afrika Mashariki. Kenya ilikuwa nchi inayoongoza kwa bidhaa na huduma katika ukanda huu. Leo, Tanzania imeipita Kenya,” Ruto alisema.

Alisisitiza umuhimu wa soko imara la kikanda, akiongeza kuwa, ili tuweze kustawi, tunahitaji soko kubwa linalowezesha watu wetu kufanya biashara na kuwekeza.”

Hata hivyo, kauli hiyo ya Ruto imeibua hisia mseto kwenye mtandao wa X, ambapo Wakenya wengi walionyesha kutoridhika.

Wakosoaji walihusisha sera zake na changamoto za kiuchumi zinazoikumba Kenya.

“Mtu wa aina gani huyu? Uchumi wetu umeharibika, na yeye anapongeza Tanzania badala ya kujiuzulu!” aliandika mtumiaji mmoja.

Hata hivyo, baadhi walimuunga mkono Ruto, wakimpongeza kwa kukubali ukuaji wa biashara za kikanda na kuhimiza ushirikiano wa kikanda.

Related Posts