Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya kodi wameitaka Serikali kupitisha Mkataba wa Kodi wa Umoja wa Mataifa, ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi nchini Tanzania.
Wito huu ulitolewa wakati wa mdahalo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Policy Forum na Norwegian Church Aid (NCA), kujadili umuhimu wa Tanzania kupitisha mkataba huo.
Wadau hao wanaamini kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza uwezo wa Tanzania kukusanya kodi, kupunguza mtiririko haramu wa fedha sambamba na kuboresha utoaji wa huduma za umma.
Mkurugenzi mkazi wa (NCA) nchini Tanzania, Berte Marie Ulveseter, amesema Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kodi, ni juhudi muhimu inayolenga kubadili mwelekeo wa sera za kodi duniani na kuhakikisha kwamba zinawanufaisha watu wote.
“Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kodi utasaidia kuhakikisha kwamba mashirika ya kimataifa, taasisi za kifedha na watu wenye utajiri mkubwa, wanawajibika katika michango yao ya kodi, huku ukifunga mianya inayoruhusu ukwepaji na upotoshaji wa kodi kwa kiwango kikubwa,” anasema Ulveseter.
Ulvester alirejea Ripoti ya Tax Justice Network, iliyochapishwa Novemba 19 mwaka huu, ikibainishwa kuwa Dola za Marekani 500 bilioni zinapotea kila mwaka kutokana na ukwepaji wa kodi, kiasi ambacho ni mara mbili ya misaada inayotolewa na nchi tajiri kwa nchi zinazoendelea.
Akizungumza katika mdahalo huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Norah Kawiche, alibainisha changamoto zinazotokana na uchumi uliounganishwa kimataifa.
“Kampuni kubwa mara nyingi huhamisha faida bila kutozwa kodi kupitia mtiririko haramu wa fedha, hali inayosababisha Tanzania kushindwa kukusanya kodi kwa sababu ya vikwazo vya kisheria,” amesema.
Ameongeza kuwa kupitisha Mkataba wa Kodi wa Umoja wa Mataifa , kutairuhusu Tanzania kushirikiana na nchi nyingine kubadilishana taarifa muhimu kuhusu ukwepaji wa kodi.
“Hii pia itaimarisha uwezo wetu wa kurejesha kodi ambazo tayari zimetolewa nje ya nchi,” Kawiche ameeleza.
Licha ya Tanzania kuwa na sheria thabiti za ndani za kodi, amesisitiza kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu ili kukabiliana na fedha zinazohamishwa nje ya nchi.
“Mpaka sasa Tanzania imesaini mikataba ya kodi na nchi tisa pekee, ikilinganishwa na Afrika Kusini ambayo ina mikataba na nchi 80. Mkataba wa Umoja wa Mataifa, utatoa fursa ya kushirikiana na zaidi ya nchi 100, na hivyo kuimarisha ushirikiano na kubadilishana taarifa,” amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Madhehebu ya Dini, Askofu Nelson Kisare, ameunga mkono hoja hiyo, akisisitiza umuhimu wa Mkataba wa Kodi wa Umoja wa Mataifa katika kuboresha juhudi za ukusanyaji kodi nchini.
“Hivi sasa, Tanzania inakusanya chini ya asilimia 50 ya mapato yake yanayotarajiwa, huku sehemu kubwa ikipotea kutokana na rushwa, ukwepaji kodi na udanganyifu,” amesema Askofu Kisare.
Ameongeza kuwa “Kodi zinapaswa kupunguza umasikini kwa kufadhili huduma muhimu kama maji safi, afya, miundombinu, na huduma nyingine za msingi”
Amebainisha kuwa ukusanyaji mzuri wa kodi unaweza kupunguza utegemezi wa mikopo na mzigo wa ulipaji kwa kuzuia rushwa na kuhakikisha watu wanatii sheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Young Feminist Movement, Magdalena Gisse, ameeleza changamoto zinazokumba Tanzania katika kutoza kodi kwa kampuni za kimataifa, akihusianisha na mzigo mkubwa wa kodi kwa vijana wa Kitanzania wanaojiajiri mtandaoni.