Viongozi wa dini wataka mabadiliko ya kisera, sheria kudhibiti ndoa za utotoni

Dar es Salaam. Ili kuwalinda watoto na ndoa za utotoni, viongozi wa dini wameshauri hatua za kisheria na kisera,  huku wakigusia msimamo wa imani mbalimbali kuhusu ndoa na umri unaofaa.

Miongoni mwa masuala yaliyoshauriwa wakati wa majadiliano ya viongozi wa dini na asasi , ni marekebisho ya sera ya elimu kuongeza kiwango cha elimu ya msingi kuwa kidato cha sita na kuweka msisitizo kwenye sheria nyingine zinahusika na masuala ya ndoa.

Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Bakwata Sheikh Khamis Mataka , amesema sera ya elimu ikisema elimu ya msingi ni hadi kidato cha sita na kupiga marufuku ndoa kwa mwanafunzi wa elimu ya lazima,  itawafanya watoto wote walioko kwenye mfumo wa elimu kuepuka ndoa za utotoni.

Hata hivyo,  amesema mbali na sera hiyo sheria mbalimbali nazo zinapaswa kuweka msisitizo juu ya umri wa kuolewa, nchi itakuwa kwa sehemu kubwa imeshughulikia suala la ndoa za mapema.

Sheikh amesema Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, inapaswa kuweka marufuku ya kuoa au kuolewa kwa mwanafunzi wa elimu ya lazima, Sheria ya Ndoa Namba 5 ya mwaka 1971 iweke marufuku ya ndoa kwa wanafunzi wa elimu ya lazima.

Vilevile sheria ya kujamiiana kuweka marufuku ya kujamiana na mwanafunzi wa elimu ya lazima

“Kwa njia hii tunaweza kufikia lengo  la kumlinda mtoto hususan mtoto mwanamke na kumsaidia kufikia ndoto na malengo yake bila ya kutuhumiana na kudhaniana vibaya na wanadini,” amesema.

Aidha, alikumbusha mafundisho ya dini akisema hata Baraza la Ulamaa linawataka Waislamu kuzingatia uzito wa suala la elimu kama alivyoelekeza Bwana Mtume (Rehma na amani zimshukie) bila ya kubagua kati ya watoto wanawake na watoto wanaume.

“Baraza la Ulamaa linawataka wazazi/walezi kusimamia vyema suala la malezi ya watoto katika maadili yetu ya Kiislamu na kuhakikisha kwamba mazingira ya kutafuta elimu yanalenga pia katika kuwalinda na uchafu,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha Songea Catholic Institute of Technical Education, kilichopo Jimbo Kuu Katoliki la Songea, mkoani Ruvuma, Padri Longino  Kamuhabwa yeye amesema, Kanisa linaelekeza kuwa ndoa ni kati ya watu wawili lakini lazima watu hao wawe wamekomaa kiakili na kimwili ili wawe na uwezo wa kutimiza haki na wajibu wa unganiko hilo.

“Wanaoozesha watu katika umri mdogo wanapingana na mapenzi ya Mungu lakini pia ni ukatili, wanaingizwa kwenye makubaliano bila kuwa na utimamu wa akili kufanya maamuzi hayo pengine akikua angeweza kuamua tofauti,” amesema Padri Kamuhabwa.

Monica Lugome ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mashariki na Pwani amesema kwa upande wa Kanisa lake,  linaamini katika ndoa za umri wa utu uzima.

“Kanisa letu hali ungi mkono ndoa za utotoni,”amesema.

Ameeleza viongozi wa dini wana jukumu la kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya ndoa za utotoni, kwani mambo wanayoyaharakia watakutana nayo wakikua.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi ameeleza malengo ya mkutano huo na viongozi wa dini kuwa ni tafakari ya pamoja  na kuangalia uzoefu wa mataifa mengine na namna unavyoweza kufaa hapa kwetu.

“Viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa na wanafikia kundi kubwa la watu na siku zote tunajifunza kuwa tukiwa na ushirikiano na kuunganisha nguvu hakuna lisilowezekana,” amesema.

Related Posts