Wananchi Mkata, Manga kula sikukuu wakiwa na majisafi, RC atoa angalizo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imesema wananchi wa vijiji vya Manga hadi Mkata katika Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga,  vitaanza kupata majisafi na salama mwishoni mwa Desemba 2024.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa Dawasa kuhakikisha inaboresha huduma ya maji kwa wananchi zaidi ya 41,000 wa vijiji hivyo na tayari Sh500 milioni za utekelezaji wa mradi huo zimetolewa.

Leo Jumamosi, Novemba 30, 2024, utekelezaji huo umeanza kwa vifaa  ikiwemo mabomba ya inchi sita kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani.

Mwakilishi wa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema mradi utatekelezwa ndani ya wiki tatu na ifikapo mwishoni wa mwezi Desemba, 2024 wakazi wa Manga na Mkata watanufaika na huduma ya majisafi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Buriani amesema Dawasa ni taasisi ya mfano na ya viwango vya kimataifa, hivyo ana imani mradi utatekelezwa ndani ya muda uliopangwa na wakazi wa maeneo ya Manga na Mkata watanufaika na huduma ya majisafi na salama.

“Tunamshukuru sana Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa kutimiza ahadi yake na leo sote tumekuwa mashahidi kwa kupokea vifaa vya kuanza utekelezaji wa mradi,” amesema Balozi Buriani.

“Sasa Maji Tanga ni mwaa mwaa, tunaomba katika utekelezaji wa mradi huu muwape kipaumbele vijana wa maeneo haya ya Manga na Mkata ambao ni wanufaika wa mradi huu, ili na wao wanufaike na uwekezaji huu.

“La mwisho niwaombe kama tulivyokubaliana Waziri kwa wananchi ambao hawatamudu kulipia gharama za kuunganishiwa, huduma kwa pamoja basi wapewe kwa mkopo wakulipia kidogo kidogo,” ameongeza.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando ameshukuru kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo na kuhaidi kusimamia ukamilike kwa wakati ikiwemo ulinzi wa miundombinu hiyo kutoharibiwa.

“Kijiji cha Manga ni moja ya vijiji katika Wilaya ya Handeni vilivyowekewa miundombinu ya maji mwaka 1974, wakati huo ulilenga kuhudumia wakazi 120,000 na sasa tuko zaidi ya wakazi laki nne,  hivyo mradi huu utasaidia kutatua changamoto ya huduma ya maji ndani ya wilaya yetu,” amesema Msando.

Related Posts