Busia. Mkazi mmoja nchini Kenya, Margaret Agutu amefariki dunia baada ya kung’atwa na nyoka wakati wa ibada ya tambiko iliyokuwa ikifanywa na mganga wa kienyeji.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko, tukio hilo limetokea Kijiji cha Murende Jimbo la Matayos, Kaunti ya Busia nchini Kenya jana Jumamosi, Novemba 30, 2024.
Mashuhuda wamesema Margaret aling’atwa na nyoka lakini kilio chake cha kuomba msaada kilipuuzwa huku hali yake ikizidi kuwa mbaya na kusababisha mganga kuondoka eneo la tukio akiwa na nyoka huyo na vifaa vyake.
Mume wa marehemu, Alloyce Okumu, pamoja na binti yao Stella Athieno, wamesema Margaret alikuwa amekwenda kushiriki ibada hiyo akiwa na majirani wengine.
“Wakati wa maombi, nyoka alimng’ata marehemu kwenye kidole chake na akamjulisha mganga akitarajia atapewa msaada wa haraka. Hata hivyo, kilio chake cha kuomba msaada kilipuuzwa, na tambiko liliendelea huku maumivu yakizidi,” inaeleza taarifa ya Tuko.
Badala ya kumsaidia Margaret, mganga huyo haraka haraka alimchukua nyoka na zana zake kwenye gunia na kutoroka eneo hilo na kumuacha akilia.
Margaret alikimbizwa hospitalini na familia yake na majirani, lakini alifariki dunia baada ya sumu kusambaa mwilini kabla ya kupata matibabu.
Hata hivyo, wakazi wa eneo hilo wametoa wito kwa vyombo vya sheria kuanzisha uchunguzi wa kina ili kumfikisha mahakamani mganga huyo ambaye kwa sasa ametoroka.
Aidha, familia ya marehemu inaomba msaada wa kifedha ili kugharamia mazishi huku mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Busia.