Dar es Salaam. Tarehe 1 Desemba 2024: Baada ya kutoa huduma zenye ubora wa kimataifa kwa mwaka mzima, Benki ya CRDB imeingia mwezi Desemba kwa kushinda tuzo mbili kutambua juhudi zake za kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake kote nchini.
Tuzo hizo zilizotolewa na Consumer Choice Awards Africa (CCA) 2024, zimezingatia maoni ya wateja na wadau tofauti walioshirikishwa na kupiga kura kumchagua mtoa huduma bora.
Benki ya CRDB imenyakua tuzo ya benki chaguo namba moja ukanda wa mashariki mwa Afrika (the most preferred, convenient, and accessible bank in eastern Africa) kutokana na urahisi wa kufikika pamoja na tuzo ya benki yenye promosheni bunifu inayowanufaisha wateja wake (the most creative and innovative consumer benefiting campaign of the year).
“Nawapongeza sana. Juhudi zenu zinaonekana kwa namna mnavyowahudumia wateja na kushirikiana na wadau tofauti kuongeza ubunifu wenye tija. Hongereni sana Benki ya CRDB,” amesema Waziri Nyongo.
Akipokea tuzo hizo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema ubunifu unaomzingatia mteja ndio msingi wa huduma za Benki ya CRDB kila siku hivyo ni furaha kuona jamii inalitambua hilo.
“Sisi ni benki inayomsikiliza mteja. Wateja wetu waliosambaa nchi nzima wana mahitaji tofauti ambayo tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kuyakabili. Kwa walio mbali na tawi, tunawasogezea na wale wanaohitaji huduma mahali popote walipo na wakati wowote tunawapa wanachokitaka. Tunaamini mteja akifurahi biashara yetu itakuwa endelevu,” amesema Raballa.
Kuhusu tuzo ya benki bora inayopendwa, inayopatikana popote na rahisi kufikika ukanda wa mashariki mwa Afrika (the most preferred, convenient, and accessible bank in eastern Africa), Raballa amesema Benki ya CRDB inaongoza kwa mtandao mpana wa matawi ambayo ni zaidi ya 260 yaliyopo katika halmashauri zote nchini pamoja na mawakala zaidi ya 25,000 wanaosaidia kutoa huduma.
“Mambo haya yote yanaonyesha ni kwa namna gani hatupati usingizi tusipomhudumia mteja wetu mahali popote alipo. Hakuna benki nyingine yenye ukubwa huo,” amesema Raballa.
“Kupitia SimBanking mteja anaweza kupata huduma yoyote aitakayo kuanzia kufungua akaunti, kuomba mkopo, kufanya uwekezaji au kufahamu viwango vya kubadilisha fedha. Haya yote yanafanyika kupitia simu ya mkononi. Kwa mwaka mzima, tulikuwa na promosheni inayohamasisha kufanya miamala kidijitali na washindi waliopatikana tunawazawadia gari jipya aina ya Nissan Dualis, bajaji au pikipiki pamoja na zawadi nyingine kemkem,” amesema Raballa.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Consumer Choice Awards Africa, Diana Laizer amesema Benki ya CRDB ni mdau mkubwa wa tuzo hizo na imekuwa ikishiriki mara nyingine.
“Kila mwaka tunakuwa na Benki ya CRDB. Kura za wateja ndizo zinazoipa ushindi kutokana na jinsi wanavyoridhishwa na huduma inazozitoa,” amesema Diana.
Akieleza kuhusu namna ambavyo Benki ya CRDB haimwachi mteja wake njiani pindi akihitaji msaada, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo amesema kipo kituo cha huduma kwa huduma kwa wateja kinachofanya kazi muda wote.
“Tunamsikiliza mteja atakayepiga simu, kutuma baruapepe au barua hata yule atakayewasiliana nasi katika akaunti zetu za mitandao ya kijamii. Tunafanya hivi ili kuhakikisha changamoto yoyote inayomkabili mteja inatatuliwa kwa wakati,” amesema Yolanda.