Dar es Salaam. Chama cha Bodaboda na Bajaji Wilaya ya Kigamboni kimesema kifo cha mbunge wao, Dk Faustine Ndugulile na mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika ni pigo kwao huku kikigusia alivyowapambania washushiwe tozo kwenye Daraja la Mwalimu Nyerere.
Chama hicho kimeeleza hayo kupitia mwenyekiti wao, Patrick Kayanda kwenye muendelezo wa maombolezo ya kiongozi huyo nyumbani kwake Kigamboni, Dar es Salaam.
Dk Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India.
Mwili wa Dk Ndugulile tayari umerejeshwa Tanzania na kesho Jumatatu, Desemba 2, 2024 utaagwa rasmi katika vuwanja vya Karimjee na utazikwa Kigamboni Jumanne ya Desemba 3.
Akizungumza Dar es Salaam, Kayanda amesema waliishi naye vizuri na hata kilio cha tozo kilipokuja walimuangukia, walipunguziwa na kuleta ahueni katika uendeshaji wa biashara hiyo.
“Ili kuvuka katika daraja lile bajaji ilikuwa Sh1,500 lakini ilishuka hadi Sh500, pikipiki za magurudumu mawili ilikuwa Sh600 lakini imeshushwa hadi Sh300 jambo hilo tunampongeza zaidi Dk Ndugulile alitubeba ni pigo kwetu,” amesema Kayanda.
Amesema mbali na uhusiano wao, walishirikiana katika kumbeba ili aingie madarakani katika nafasi ya ubunge mwaka 2010 na katika sakata la bodaboda na bajaji kupigwa marufuku kuingia mjini, alijitosa kuwasaidia.
“Tulikuwa tunaishi naye vizuri kuna mambo alikuwa anatusaidia hata kipindi ambacho bodaboda na bajaji tumezuiliwa kuingia mjini, nilimpigia simu akiwa bungeni alipokea baada ya kumueleza akanijibu analifanyia kazi kwa kuongea na waziri mwenye dhamana na tangazo likatolewa tuingie mjini,” amesema Kayanda.
Mfanyabiashara maarufu nchini, Azm Dewji amemzungumzia Dk Ndugulile akisema urafiki kati yao haukuanza kutokana na nafasi yake ya ubunge ila ulikuwa wa muda mrefu.
“Huku Kigamboni nina nyumba yangu kule Mbutu na kila mara nilikuwa napita hapa kwake kusalimiana naye na kuna wakati nilikuwa namualika kuja Mbutu lakini hakuna hata siku moja aliwahi kumdharau wala kumkejeli mtu,” amesema Dewji.
Amesema kitu kikubwa alichokuwa nacho Dk Ndugulile ambacho waliowengi wakipata madaraka wanakosea ni kupandisha mabega lakini marehemu huyu alikuwa anaishi na jamii vizuri.
Mbunge wa Singida Magharibi na Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu amesema: “Nimefahamiana na Dk Ndugulile miaka 14 iliyopita nilipokuwa mtumishi wa umma serikalini na baadaye mkuu wa wilaya, Dk Ndugulile alinisaidia na kunipa moyo kwa kupambana.”
Amesema hata alipoingia bungeni mwaka 2015 uhusiano wao na Dk Ndugulile uliongezeka zaidi, ilikuwa akiwa na jambo alikuwa anamfuata na kushauriana.
“Taifa tumepoteza mtu mzalendo, nikiwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge na yeye akiwa kwenye kinyang’anyiro alikuwa makamu wangu nimefanya naye kazi vizuri na alikuwa mwenye msimamo na hasiti kukuambia ukweli inapobidi,” amesema
“Mara ya mwisho nilisafiri naye kwenda Zambia kwenye mikutano, tulikuzungumza na tulilala hoteli moja na tukaja kwenye msiba wa (Lawrence) Mafuru anasafiri kwenda kwenye matibabu aliniaga,” amesema.
Msiba huo wa Mafuru ulitokea nchini India Novemba 9, 2024 alikokuwa anapatiwa matibabu. Mwili wake uzilikwa jijini Dar es Salaam, Novemba 15, 2024.
Mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula amesema kwa nafasi hiyo alikuwa karibu na Dk Ndugulile na baba yake mzazi alianza kufanya naye kazi siku moja.
“Baba yake nilianza kufanya naye kazi siku moja Wizara ya Mambo ya Nje, ni familia ya karibu kitaaluma na hata tulipokuwa bungeni tulikuwa karibu na kushauriana,” amesema.
Balozi Mulamula amesema Bunge limepoteza mtu makini, mnyenyekevu na mwerevu na hata baada ya kuteuliwa katika nafasi mpya aliendelea na ukarimu wake.
“Baada ya vikao vya mwisho vya Bunge tulikuwa pamoja kantini tukinywa chai tukawa tunapiga stori tukimueleza baada ya kupata nafasi mpya asitusahau wapambe wake,” amesema.
Balozi Mulamula amesema walimueleza hayo kwa kujenga hoja kuwa watu wa Afrika Magharibi wakipata nafasi kama hizo huwa wanakwenda kuwabeba wenzao huku akieleza mwisho Dk Ndugulile alikubali na kuahidi kuwavuta Watanzania.