Hatari ya ‘utani’ kwenye uhusiano

Dar es Salaam. Licha ya mazungumzo kuwa nguzo muhimu katika ndoa na uhusiano, lakini maneno haya huweza kugeuka mwiba na sumu kali inayoweza kuleta madhara endapo yatatumika vibaya.

Dhihaka, matusi, kejeli na maneno ya udhalilishaji dhidi ya mwenza yanaelezwa kuwa chanzo pia cha maumivu yanayoweza kusababisha changamoto ya afya ya akili.

Angel Willium ni miongoni mwa waathirika wa dhihaka katika ndoa na kwa sababu hiyo, amejikuta akipoteza hamu ya kuwa kwenye taasisi hiyo ambayo ni msingi muhimu wa kujenga familia.

“Nilijifungua kwa upasuaji baada ya njia kushindwa kufunguka, nilikaa siku kadhaa hospitalini na baadaye niliruhusiwa kutoka hospitali na kwenda kujiuguzia nyumbani,” aanasimulia Angel.

 Anasema siku zilienda na miezi ikapita na hatimaye akapona mshono na kubaki na kovu ambalo limebaki kama alama ya ushujaa wa mama jinsi alivyoweza kumpambania mtoto wake aingie duniani akiwa salama.

“Kumbe mume wangu alikuwa anakerwa na kovu lile, ilifika wakati nikitoka kuoga naambiwa kavalie bafuni, sikujua sababu hasa, siku moja nikarudia kuvalia nguo chumbani akanitamkia wazi kuwa, natia kinyaa na huu mshono wangu niwe navalia nguo bafuni,” anaeleza.

 Angel anasema aliumizwa mno na maneno hayo ambayo yalikuwa yakiendelea siku hadi siku na alishindwa kuvumilia, akaamua kuomba talaka.

Mwingine aliyepitia kadhia kama hiyo ni Rose Geofrey mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, ambaye amelazimika kuvunja uhusiano na mzazi mwenzie kwa sababu ya maneno ya dhihaka.

Rose alikutana na mchumba wake 2018 akiwa chuo kikuu, kipindi hicho akiwa na miaka 22 na mwaka 2022 Mungu aliwajalia kupata mtoto.

“Nilipokaribia kujifungua ilibidi nirudi kwa wazazi wangu kwa ajili ya kujifungua na matunzo ya kipindi cha uzazi, ninachoshukuru nilijifungua salama,” anasema Angel.

Anasema alikaa nyumbani kwa miezi mitatu ili apate matunzo kama ilivyo desturi ya kipindi cha uzazi na baada ya muda, mchumba wake alitakiwa kuja nyumbani kujitambulisha.

“Lakini alipokuja kuniona nikagundua kama ananishangaa vile, na mwisho akasema ‘siku hizi hata hupendezi umekuwa mbaya ulivyonenepa, huvutii tena kama mwanzo.”

“Ile kauli ilinikera, niliwaza nikajiuliza haoni kama nimenenepa baada ya kumzalia? Haikutosha hata niliporejea nyumbani alioneshwa kukerwa na vilio vya mara kwa mara vya mtoto,” anasema na kuongeza;

“Aliwahi kunitamkia wazi kuwa hataki kelele za mtoto zinamsumbua, yote haya yamenifanya nipoteze shauku ya kufunga naye ndoa kwa sababu nimegundua siwezi kuishi na mtu wa aina hii.”

Walichopitia Angel na Rose kinasadifu maandiko mbalimbali ya tafiti ukiwemo uliofanywa na mtaalamu wa uhusiano, John Gottman unaothibitisha athari kubwa wanazokumbana nazo wanandoa hutokana na maneno ya dhihaka kati yao.

Katika utafiti wake, Gottman alichunguza namna wawili wanavyohusiana kupitia lugha zao na kugundua kuwa maneno ya dhihaka, matusi au ya kubishana, ukosoaji na dharau yanaweza kuchangia kasi ya kuharibika kwa ndoa.

 Gottman alithibitisha kupitia uchunguzi wake kuwa maneno mengi ya dhihaka na matusi ni moja ya dalili za mapema kabisa kabla ya kupeana talaka na kutengana kwa wanandoa.

Sehemu ya utafiti huo inasema, “ Maneno ya dhihaka huvunja imani, huchochea hasira, machungu, hupunguza mawasiliano na kudhoofisha heshima na kisha kuleta hatari kwenye utu wa mtu.

Dhihaka pia husababisha matatizo ya kisaikolojia, hisia za huzuni, hasira, wasiwasi na mfadhaiko ambao humsababishia mtu kujihisi kuwa kwenye mazingira hatarishi na yasiyokuwa na furaha.”

Utafiti mwingine kuhusu unyanyasaji wa kihisia ulifanyika mwaka 2011 na Taasisi ya Afya ya Marekani.

 Kwa mujibu wa utafiti huo, unyanyasaji wa kihisia na dhihaka unachukua sehemu kubwa katika maisha ya uhusiano na wanandoa, matokeo yakionesha asilimia 48.8 wanaume na asilimia 48.4 ya wanawake duniani kote wanaishi katika maisha ya unyanyasaji wa kihisia au shambulio la kisaikolojia katika maisha yao.

Aina ya unyanyasaji ulioripotiwa, ni ule wa dhihaka za maneno machafu ambao wengi waliuchukulia kawaida, aina ya wanawake waliokumbwa na adha hii ni wale wa nchi za Kiarabu na Korea huku ukihusisha makundi yote kiumri.

Mtaalamu wa saikolojia, Neema Mwankina amesema madhara ya dhihaka kwenye uhusiano husabisha maumivu ya kihisia.

Anasema maumivu ya kihisia, mara nyingi humjengea muhusika hasira ambayo, hata si kukuonesha wewe tu, bali kila mmoja ataiona hasira yake.

“Unapompa mtu maumivu ya kihisia kwa kupitia maneno mabaya kwenye uhusiano kuanzia hapo, hakutakuwa na upendo na kama ni tendo la ndoa, basi kuanzia hiyo siku utakuwa unambaka, dhihaka huwa na kawaida ya kuondoa hisia na upendo baina ya watu.

“Kutokana na maneno aliyotamkiwa, basi huwa na hasira kwa kila mtu huku akihisi kile alichoambiwa ni kila mtu anamuona hivyo,” anasema.

Anasema mtu aliyeathiriwa na dhihaka, mara nyingi huwa na tatizo la afya ya akili ambalo litamfanya amchukie kila aliyekaribu naye na kuhisi muda wote ananafikiwa, kila kitu yeye huweka upande hasi na si chanya.

“Madhara ya dhihaka ni makubwa sio tu nyumbani, bali hata katika maeneo ya kazi, utakuta muathirika utendaji wake wa kazi hupungua siku hadi siku kutokana na sononeko la nafsi.

Kadhalika, Mwankina aanasema maneno hayo hayaathiri uhusiano kati ya wenza pekee, bali hata kwa watoto.

“Hasira hii kwa wanandoa mara nyingi huhamishiwa kwa watoto, hujikuta wakipigwa na kutukanwa hata katika kosa dogo na mama zao, hali hii hutokana na uchungu alionao mzazi huyo.

“Mzazi unapomtakia mtoto maneno yasiyo sahihi, hulichukua na kuliona kweli kitu ambacho huharibu mustakabali mzima wa maisha yake na kushindwa kuona jema lolote atakalolifanya litaonekana baya tu,” anasema Mwankina.

Hali ikifikia hapo, basi hata maisha ya mtoto nayo hugeuka na kujikuta naye anakuwa mti wa kubeba visasi moyoni mwake.

“Mtoto anaposhindwa kulipiza kisasi kwa mzazi wake kwa kile alichomwambia, mara nyingi hujiapiza kulipiza kisasi kwa yeyote atakaye mtamkia dhihaka kwa mara nyingine,” anasema mtaalamu huyo.

Hivyo ameonya juu ya wenza au watu walio katika uhusiano kuepuka kutamkiana maneno ya dhihaka kila mara ili kuepukana na maumivu hayo.

Related Posts