Mwanaisha (52) ni mama wa watoto wanne. Mwanawe wa kwanza, Bashir (28) anapitia wakati mgumu kwenye uhusiano na mchumba wake. Jitihada za kurekebisha changamoto hizo hazijafanikiwa kuleta ufumbuzi.
Kabla hajakutana na mchumba wake wa sasa, Bashir amekuwa na uhusiano na wanawake kadhaa ambao kama inavyoelekea kwenye uhusiano huu wa sasa, uliishia kuvunjika.
Hanifa (26), mtoto wa pili wa Mwanaisha, naye ana changamoto nyingi za uhusiano. Ingawa mwenyewe anasema hana mpango wa kuolewa, tathmini ya mazungumzo yake inaonekana ana changamoto nyingi za afya ya akili. Kwanza, hajui namna bora ya kusema hisia zake. Ukimtazama usoni, huoni uangavu wa uso. Uso umezizima hasira na simanzi.
Ingawa sikuzungumza na wanawe wawili, ninaona uhusiano mkubwa wa changamoto wanazopitia Bashir na Hanifa na malezi. Kwa mfano, Mwanaisha anaonekana kuwa mkali, mgomvi na mtu mwenye msimamo mkali. Ndoa yake ya kwanza haikudumu kwa muda mrefu baada ya kuwazaa watoto wake wawili wa mwanzo.
Ndoa ya pili, yenye watoto wawili, nayo haionekani kuchukua uelekeo tofauti. Mwanaisha anamlalamikia mume wake kuwa ni mtu katili asiyejali familia yake, lakini ukimsikiliza vizuri, hata yeye ana kiasi fulani cha ukatili asichotaka kukiona kwa wengine.
Miaka ya 1950, John Bowlby, mwanasaikolojia wa Uingereza, aliwachunguza watoto waliokuwa wamepoteza, au kutengwa na wazazi wao mara baada tu ya vita vya pili vya dunia.
Wakati huo, iliaminika kuwa mwanadamu ana mahitaji matatu makubwa ambayo ni chakula, malazi na mavazi. John Bowlby alibaini kuwa watoto wengi waliotengwa na wazazi wao walikuwa na matatizo mengi ya kitabia kama vile ugomvi na ubabe.
Bowlby akajiuliza, kwa nini iwe kwa watoto hawa walioishi bila wazazi? Hatimaye, Bowlby akawa amegundua kuwa pamoja na mahitaji matatu ya msingi kwa mwanadamu, tunalo hitaji la nne la kujisikia salama.
Tunajisikia salama tunapokuwa na mtu tunayeweza kuwa na uhakika atakuwa mlinzi wetu. Mtu huyu, kwa wengi, wetu ni mama. Tangu anapozaliwa, kimaumbile, tunajiweka karibu na mama zetu.
Ukaribu huu una kazi kubwa ya kutuliza nafsi zetu. Tukiukosa ukaribu huu, kwa sababu yoyote, tunaanza kuishi maisha ya hofu, na hapa ndipo zinapojitokeza hitilafu nyingi za kitabia.
Usalama ni upendo. Miaka ya 1960, mwanasaikolojia Harry Harlow aliviwekea vitoto vya nyani mfano wa mama nyani wawili. Nyani wa kwanza alikuwa ni nyaya zilizowekewa maziwa, tumwite ‘mamawaya.’
Nyani wa pili alikuwa kigodoro kisichokuwa na maziwa, tukiite ‘mama godoro.’ Harlow alitaka kujua mtoto nyani angekaa wapi kati ya mama hao wawili.
Katika hali ya kushangaza, mtoto nyani alipendelea zaidi kukaa kwa ‘mama godoro’ hata kama hakuwa na maziwa. Ingawa kitoto hiki kilinyonya maziwa kwa ‘mama waya’, kilikimbilia kukumbatia kigodoro mara baada ya kunyonya. Harlow akawa amehitimisha kuwa pamoja na chakula, nyani anahitaji pia kujisikia ‘kuna mtu anajali.’ Nasi, kama ilivyo kwa nyani, tunahitaji kupendwa. Ukiukosa upendo katika miaka ya mwanzo ya safari ya maisha yako, unaanza kuhisi dunia si mahali salama pa kuishi. Huwezi kuwa binadamu mwenye akili tulivu na timamu katika mazingira kama haya.
Baadaye miaka ya 1970, Mary Ainsworth, mwanasaikolojia wa Kimarekani, alifanya utafiti kuona namna hitaji hili la kupendwa linavyoathiri afya ya akili ya mtoto.
Tunapozungumzia afya ya akili, kimsingi tunazungumzia utulivu anaokuwa nao mtu, unaomfanya awe na uwezo wa kuwapenda wengine, kuhusiana vyema na wengine na kufanya uamuzi usioleta athari kwa wengine.
Ainsworth alichunguza uhusiano wa mama na mwanawe na namna uhusiano huo unavyojidhihirisha kupitia tabia za mtoto.
Katika utafiti wake, mama alikaa na mtoto wa miaka isiyozidi mitatu kwenye chumba kisicho na mtu mwingine.
Mtoto alikuwa anacheza wakati mama akiendelea na shughuli zake, mara mwanamke mgeni aliingia. Akawa anazungumza na mama huyo kwa muda halafu mama akaondoka kimya kimya na kumwacha mtoto na mgeni.
Anasema hapo kilichokuwa kinachunguzwa ni tabia ya mtoto pindi mama yake anapoondoka. Je, huwa na wasiwasi wa kuachwa na mama?
Kisha, akachunguza baada ya muda kidogo, mama aliporudi, hali ilikuwaje? Je, angemkimbilia au angepuuza ujio wake?
Ainsworth baada ya kuwachunguza watoto wengi, aligundua wangeweza kugawanyika kwenye makundi makuu matatu kulingana na utimamu wao wa afya ya akili. Kundi la nne liliongezwa baadaye.
Huyu ni mtoto anayejisikia huru kucheza, anayecheza bila kumsumbua mama yake. Uso wake una furaha na matumaini na mara kwa mara alishirikiana na mama michezo yake.
Mama alipoondoka mtoto huyu hakuonesha wasiwasi. Hakutaka mama aondoke lakini hakuonekana kusumbua kubaki na mgeni. Utulivu huu ulionesha imani aliyokuwa nayo kwa mama na mgeni.
Hata hivyo, mama aliporudi mtoto huyu alimkimbilia kwa bashasha kuonesha ukaribu na mama yake.
Ainsworth aligundua kuwa kila mtoto mtulivu, basi mama yake naye alikuwa na tabia ya kupatikana kwa mtoto kimwili na kihisia.
Pia, mama alikuwa na tabia zinazotabirika kwa maana ya mtoto kuelewa kwa hakika mama angeondoka saa ngapi na kurudi muda gani na hakuonekana kuwa mtu mwenye huzuni na ishara za maisha yenye simanzi.
Mtoto wa kundi hili, huwa na utimamu wa afya ya akili inayomwezesha kuwa na mtazamo chanya na watu.
Ukubwani hagombani na watu na anajali hisia za mtu mwingine. Kwenye migogoro, huyu ni mtu asiyetumia nguvu. Unapomkosea, anajali hisia zako, mwepesi kusamehe na anapokosea hapati shida kuomba msamaha.
Kwenye uhusiano wa kimapenzi, huyu ni mtu mwaminifu. Usaliti ni msamiati mgumu kwake na hawezi kufanya mapenzi na mtu asiye na hisia naye.
Mtoto huyu haoneshi tabasamu mama akiwepo chumbani wala hafanyi jithada za kuwa karibu naye.
Hata anapoondoka haoneshi wasiwasi. Kuna namna anakuwa kama hana haja na mama yake.
Mama anaporudi chumbani wala hakujali. Haonekani kuwa na haja ya kumfuata mama na anaweza kuendelea na michezo yake kama vile hajamwona.
Hivyo, Ainsworth alihusisha tabia za mtoto huyu na tabia za mama yake. Ingawa mama yake angeweza kupatikana kwa mtoto kimwili, Ainsworth aligundua huyu ni mama asiyejali hisia za mwanawe hata pale anapokuwa na hitaji kubwa la kueleweka, kusikika na kujisikia kuthaminika.
Tabia hii ya kutokujali hisia za mtoto ilichangia tatizo la mtoto hutokusumbuka kutafuta ukaribu na mama yake. Kwa lugha nyingine, mtoto alishajenga kiburi kama mbinu ya kufanya maisha yaendelee bila usumbufu.
Ukubwani, huyu ni mtu anayeonekana kujiamini kupindukia, hivyo uhusiano wake na watu unaingia dosari. Kuanzisha uhusiano wa karibu wa kimapenzi inakuwa changamoto hasa kwa sababu hawezi kumuamini sana mtu mwingine.
Hata pale anapoanzisha uhusiano huo, uwezekano wa kuwepo migogoro mingi ni mkubwa. Huyu, mathalani ni mtu anayeweza kufanya mapenzi na mtu yeyote hata kama hakuna upendo.
Ingawa darasani wanaweza kuwa na akili nyingi, tatizo la ushindani sambamba na matarajio makubwa kupindukia linaweza kuwaingiza kwenye changamoto nyingi za kihisia na matokeo yake ni kuishi maisha yenye wivu, husda, majivuno yanayoweza kumnyang’anya furaha.
Huyu ni mtoto ‘anayemganda’ mama na muda wote anaweza kutaka abebwe. Uso wake hujaa wasiwasi kwa hofu ya kubaki mwenyewe.
Kuondoka kwa mama huleta kizaazaa na kumnyamazisha pale anapomwacha si kazi nyepesi. Kimsingi hana imani na usalama wake akiwa mbali naye na hisia za kutafuta huruma humtawala.
Mama anaporudi chumbani, mtoto huyu angeweza kulia kama namna ya kusema, ‘Kwa nini umenionea kwa kuniacha mwenyewe?’ Huyu ni mtoto asiyejiamini, asiyeamini watu na tabia zao, kwa kiasi kikubwa hutegemea wengine wanataka nini.
Mama wa mtoto huyu, kitabia anajali hisia za mtoto, anajua kupenda, lakini hatabiriki. Kukosa uhakika ni wakati gani hasa atapata upendo wa mama yake huleta hali ya wasiwasi unaoathiri imani yake kwa mama.
Woga huu wa mtoto, ukubwani hujidhihirisha kwenye utegemezi kupindukia kwa watu wengine. Sababu kubwa ni kutokujiamini na hivyo kuamini kuwa usalama wake uko mikononi mwa watu wengine.
Kwenye uhusiano wa kimapenzi, huyu ni mtu asiyejipa muda wa kutosha kumwelewa mtu na hivyo anayeweza kuishia mikononi mwa matapeli watakaomuumiza.
Kutokujiamini kunaweza kumfanya akafanya mapenzi na mtu asiyempenda kama namna ya kujihakikishia uhusiano. Maisha yake yanaweza kutawaliwa na hisia za wasiwasi, hofu, kukata tamaa na sonona.
Huyu ni mtoto asiyeelewa mbadala wa nguvu na mabavu. Katika utafiti wa Ainsworth, huyu ni mtoto ambaye angeweza kucheza kwa kumpiga piga mama na midoli yake.
Kuondoka kwa mama hakumsumbui kama ilivyokuwa kwa mtoto jeuri, lakini anaonekana kumchangamkia mgeni kuliko mama yake, kumaanisha ni mwepesi kuamini watu asiowajua kuliko familia yake.
Mama anaporudi chumbani, mtoto huyu angeweza kumkimbilia, lakini kinachoshangaza ni kwamba angeweza hata kumpiga kama namna ya kusema ‘ulikuwa wapi muda wote?’
Ukatili unaoonekana kwa mtoto, ni matokeo ya kulelewa na mama mkali kupindukia, asiyeelewa hisia zake, asiyetabirika anataka nini.
Katika mazingira yetu, huyu anaweza kuwa mama mwenye matusi, mbabe, anayetumia mabavu kuadabisha na huenda anaweza kumwacha mtoto alie bila msaada.
Kwa hakika, huyu ni mtoto anayeweza kupigana na wenzake anapocheza, hana imani na watu na kuna uwezekano mkubwa wa kuwa hana hisia na anaweza kumuumiza mtu mwingine na asione shida.
Ukubwani hawa ni watu wanaokuja kuwa katili, wababe, wagomvi, wanaoweza kuumiza watu wengine na wasijisikie hatia. Hisia zinazowatawala ni chuki, hasira, kisasi kinachoweza kuwasababisha wakaishia gerezani.
Hatuwezi kuzungumzia afya ya akili bila kuzungumzia umuhimu wa kujenga uhusiano wa karibu na watu.
Uhusiano huu unaanza tangu tunapozaliwa na kwa kiasi kikubwa, unamtegemea mama. Kuna umuhimu wa mama kupatikana, kuelewa hisia za mtoto na yeye mwenyewe kuonekana kweli ana uso wenye matumaini.
Hili lina tafsiri kubwa kwenye sera zetu za ajira. Je, ni kwa kiwango gani tunamruhusu mama kupatikana katika kipindi cha mwanzo cha uzazi?
Je, ni sahihi wazazi kuwapeleka watoto kwenye shule za bweni katika umri mdogo? Pamoja na maendeleo yao kitaaluma, ni kwa namna gani shule hizi zinaelewa umuhimu wa mtoto kujenga uhusiano wa karibu na wazazi wake?.