KAMA kuna kitu ambacho mashabiki wa Tabora United wanajivunia ni uwepo wa washambuliaji wawili waliowahi kutamba na timu ya Yanga, Mkongomani Heritier Makambo na Mburkina Faso, Yacouba Songne kutokana na mchango wao ndani ya kikosi hicho.
Makambo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Al Murooj SC ya Libya huku Yacouba Songne akitokea AS Arta/Solar7 ya Djibouti, walianza taratibu maisha yao kikosini humo, ingawa hadi sasa wamechangia mabao 12 kati ya 16 ya kikosi kizima.
Yacouba pekee amehusika na mabao saba ya timu hiyo akifunga manne na kutoa asisti za mabao men-gine matatu huku kwa upande wa Makambo akichangia matano, akifunga mawili na kusaidia kuasisti matatu na kurejesha matumaini ndani ya kikosi hicho.
Mbali na Yacouba aliyefunga mabao manne ndani ya kikosi hicho, nyota mwengine ambaye amekuwa katika kiwango bora katika michezo ya hivi karibuni ni Offen Chikola mwenye manne tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea Geita Gold.
Ubora wa wachezaji hao umeifanya Tabora kufufua matumaini ya kufanya vizuri baada ya kuuanza msimu vibaya ambapo ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC Novemba 29, umeifanya kufikisha michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza.
Katika michezo hiyo mitano, Tabora imeshinda minne ikizichapa Pamba na Mashujaa kwa bao 1-0, ikai-funga Yanga mabao 3-1, ikashinda 2-0, mbele ya KMC FC, huku sare pekee ikiwa dhidi ya Singida Black Stars ya mabao 2-2, Novemba 25, mwaka huu.
Akizungumzia viwango vya wachezaji hao kocha wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi alisema siri kubwa ni uzoefu walionao, huku akieleza sababu nyingine ni kujituma.