Makamba asimulia mikiki aliyopitia Dk Ndugulile hadi ubosi WHO 

Dar es Salaam. Mbunge wa Bumbuli na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesimulia mambo aliyoyapitia, Dk Faustine Ndugulile hadi kutwaa ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Ndugulile aliyekuwa mkurugenzi mteule wa WHO Afrika, alifariki dunia Novemba 27, 2024 akipatiwa matibabu nchini India.

Katika safari ya Ndugulile kuwania nafasi hiyo aliyoshinda Agosti 27, 2024 awali alianza kampeni wakati Waziri wa Mambo ya Nje akiwa Makamba kabla ya kubadilishwa na wadhifa huo kuteuliwa Mahmoud Kombo.

Akisimulia turufu zilizombeba Ndugulile hadi kushinda nafasi hiyo Makamba amesema ni pamoja na weledi na umahiri wake.

“Dk Ndugulile kilichomsaidia alikuwa na uwezo wa juu ukilinganisha na wagombea wengine wote kuna vitu vilikuwa vinampatia turufu kwanza weredi wake binafsi, pili uzoefu wake wa kuwa kwenye utaalamu,”amesema Makamba.

Pia, Makamba amesema uzoefu wa Ndugulile katika siasa ulimsaidia kutengeneza sera za kipekee kati ya washindani wake 17.

Makamba amesema hayo leo Desemba mosi, 2024 nyumbani kwa Ndugulile ambako waombolezaji mbalimbali wamekusanyika.

Makamba amesema akiwa Waziri wa Mambo ya Nje alipigiwa simu na Dk Ndugulile mwaka 2023 mwishoni akimuomba miadi akisema kuna jambo anataka kumuambia.

“Baada ya kuonana naye alinieleza nia yake ya kugombea nafasi mpya, alinitaka nikaongee na Rais Samia Suluhu Hassan kumjulisha na kweli nilifanya hivyo na Rais alikubali.

“Baada ya Rais kuridhia tulianza kutengeneza timu za ushindi na kazi ilikuwa ngumu kwani waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro walikuwa wengi kama 17 na wengine kutoka WHO,”amesimulia Makamba.

Amesema kazi ya kampeni haikuwa nyepesi na kwa kiasi kikubwa mgombea mwenyewe alikuwa anajibeba na haikuwa kazi kumuuza kwa wapigakura.

“Kazi yangu ilikuwa ni kumtambulisha lakini mwenyewe alikuwa anaongea…Rais alitupatia ndege yake na mjumbe maalumu, Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu kuzunguka nchi nane kupiga kampeni,” amesema.

Akikumbuka safari yake ya mwisho na Dk Ndugulile, amesema walienda Ghana kufanya mkutano na mawaziri wa huko.

Akizungumza namna anavyomkumbuka Dk Ndugulile, Makamba amesema, alifahamiana naye bungeni wote wakiwa hawana cheo huku akimkumbuka zaidi kwa hoja ya kivuko cha Kigamboni.

“Dk Ndugulile nilifahamiana naye baada ya kuingia pamoja bungeni mwaka 2010 wakati ule wote tulikuwa ‘back bencher’ alikuwa rafiki yangu na alikuwa mahiri mwema na mwanataaluma na mkweli na mwenye msimamo.

“Nitamkumbuka kwa suala la kivuko cha Kigamboni, alikuwa anataka kuona ufanisi wa usafiri huo uwe wa haraka na shabaha yake ilikuwa watu wavuke kwa urahisi kwenda na kutoka Kigamboni,”amesema Makamba.

Related Posts