Miaka 41 ya kudhibiti Ukimwi, maambukizi yakipungua

Dar es Salaam. Mapambano ya kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, kwa mara ya kwanza yalianza baada ya kuwagundua wagonjwa watatu Novemba, 1983 katika Hospitali ya Ndolage mkoani Kagera.

Wakati bado haijajulikana ni nini hasa kinawasumbua wagonjwa hao, maambukizi ya VVU yalienea kwa kasi kubwa, kukawa na wagonjwa wengi wa Ukimwi miaka iliyofuata.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha mwaka 1984 wagonjwa wengine wapya wapatao 106 walitambuliwa na idadi iliongezeka kufikia wagonjwa 295 mwaka 1985 na wagonjwa 1,121 mwaka 1986.

Leo Desemba Mosi, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Ukimwi, Tanzania inatimiza miaka 41 tangu ugonjwa huu uingie nchini yapata miongo minne iliyopita. Taifa limeendelea kupambana kudhibiti maambukizi ya VVU.

Kilele cha maadhimisho hayo yaliyoanza Novemba 25, katika Uwanja wa Majimaji uliopo mjini Songea mkoani Ruvuma kinafikiwa leo, Makamu wa Rais, Dk Isdory Mpango akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Novemba 29, akifungua kongamano la kisayansi na uzinduzi wa usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi mwaka 2022/2023, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema kiwango cha ushamiri wa maambukizi ya VVU kimepungua kitaifa kutoka asilimia saba mwaka 2003/2004 mpaka asilimia 4.4 mwaka 2022/2023.

Alisema kiwango cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, nacho kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 mpaka asilimia 8.1 kwa mwaka 2023.

Waziri Mhagama alisema juhudi za Serikali na wadau wote waliojielekeza katika kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanakuwa salama na kwamba, usalama wa watoto wanaozaliwa kutopata maambukizi hivi sasa ni mkubwa kutokana na jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuwekeza na kutekeleza afua mbalimbali za masuala ya VVU na Ukimwi.

“Tujielekeze katika kuratibu mapambano dhidi ya Ukimwi na VVU na kutengeneza mikakati unganishi na shirikishi kufika katika mafanikio, lazima kuona thamani ya tathimini yetu inayotuonyesha tulipotoka na tunakoelekea.

“Kila mmoja ana kila sababu ya kuwa mshiriki namba moja kulinda mafanikio tuliyofikia na kuhakikisha tunakokwenda tunafanya vizuri zaidi katika mapambano ya VVU na Ukimwi. Tacaids endeleeni kuweka utaratibu wa kushughulikia unyanyapaa kwa Waviu ili kuongeza nguvu za mapambano,” alisema.

Mhagama alisisitiza umuhimu wa kufuata mila na desturi katika mapambano ya VVU na Ukimwi kwa kuendeleza utoaji elimu kwenye shule na vyuoni.

Katikati ya mafanikio, takwimu za matukio muhimu ya binadamu 2023 zilizotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) Septemba 2024, kati ya magonjwa 20 yaliyotajwa kuwa chanzo cha zaidi ya nusu ya vifo vyote nchini, magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kukosa hewa baada ya kuzaliwa na maambukizi ya VVU ni kinara.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea alisema jitihada zinaendelea kufanyika ili kudhibiti kuendelea kuenea kwa maambukizi ya VVU na kwamba, kwa sasa uhamasishaji unafanyika hadi ngazi ya kijiji ili watu wajue namna ya kujilinda na kuepuka.

Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na Ukimwi ilivyo nchini. Matokeo ya awali ya utafiti huo yalionyesha nchi imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Utafiti huo unaotambulika ‘Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi kwa mwaka 2022/2023’ ulipima matokeo ya mwitikio wa kitaifa wa Ukimwi nchini miongoni mwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15.

Lengo lilikuwa kukadiria kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, ushamiri, ufubazaji kwa watu wanaoishi na VVU na utumiaji wa dawa kitaifa na kimikoa.

Utafiti ulionyesha watu wanaoishi na VVU kiwango cha ushamiri wenye umri zaidi ya miaka 15 ni asilimia 4.4. Kati ya hao asilimia 4.5 ni wa upande wa Tanzania Bara na asilimia 0.4 ni wa upande wa Zanzibar na kwa kigezo cha jinsia wanawake ni asilimia 5.6 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 3.0.

Kiwango cha ushamiri kwa kuzingatia kigezo cha makazi, maeneo ya mjini ni asilimia tano na vijijini ni asilimia nne.

Utafiti huo ulibaini miongoni mwa watu wazima zaidi ya miaka 15 maambukizi yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023 sawa na upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume.

Vilevile, utafiti ulibaini kiwango cha kufubaza VVU kiliendelea kukua, kwa sasa ni wastani wa asilimia 78. Kwa upande wa wanawake kiwango kimekua kwa asilimia 80.9 na wanaume asilimia 72.2 ikilinganishwa na asilimia 52 iliyokuwepo kulingana na utafiti wa mwaka 2016/2017.

Kwa kuzingatia malengo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi Duniani (Unaids) ya 95-95-95 (yaani, asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua afya zao, asilimia 95 ya wote waliopima na kuwa na maambukizi kuanza kutumia dawa na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU).

Utafiti ulionyesha asilimia 83 wanajua hali zao za maambukizi ikilinganishwa na asilimia 61 ya mwaka 2016/2017. Asilimia 98 ya wanaojua hali zao za maambukizi wameanza kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU kutoka asilimia 94 pia wanaotumia dawa asilimia 94 wamefubaza VVU ikilinganishwa na asilimia 87 mwaka 2016/2017.

Kutokana na matokeo hayo, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kufikia malengo ya 95-95-95 ifikapo mwaka 2025.

Hata hivyo, tafiti zilionyesha wanaume wamefubaza kidogo kuliko wanawake na wakati huohuo vijana wamefubaza kwa asilimia kidogo ikilinganishwa na watu wazima.

Related Posts