Mpango ataja mambo yanayochochea maambukizi ya VVU

Songea/Dar. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametaja mambo matano yanayochochea maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini akisema yanachangia kutofikiwa kwa malengo ya kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Dk Mpango ametaja mambo hayo ni unyanyapaa kuwa kizingiti hatari, mitazamo hasi, wanaume kutokupima, elimu duni na tabia hatarishi.

Hata hivyo, imeelezwa bado kuna idadi kubwa ya wanaume wanaotegemea majibu ya vipimo vya maambukizi ya VVU kutoka kwa wake zao jambo linalotajwa kuwa hatari kwao.

Dk Mpango amesema hayo leo Desemba mosi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kitaifa yaliyoadhimishwa katika viwanja vya Maji Maji vilivyopo mjini Songea mkoani Ruvuma, yenye kauli mbiu, “Chagua Njia Sahihi, Tokomeza Ukimwi.”

Amesema ubaguzi, unyanyapaa na mtazamo hasi kwa walioathirika hurudisha nyuma mapambano ya Serikali na wadau.

“Unyanyapaa husababisha woga unaoathiri upimaji kwa hiyari na upatikanaji wa huduma zingine kama za unasihi na utumiaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU yaani ARV kwa wanaoishi na maambukizi,” amesema akisisitiza kuwa ni muhimu kuungana kwa pamoja kutoa elimu kuanzia ngazi binafsi na familia ili kuachana na mitazamo hasi.

Dk Mpango amesema hali ya maambukizi mapya inaonekana kuchochewa zaidi na tabia hatarishi na hususan ulevi uliopindukia na ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi na matumizi ya dawa za kulevya.

“Haya yanachangia maambukizi mapya ya VVU, kuzingatia maudhui ya vipindi kwa ajili ya kubadili tabia na kuachana na mila zinazochochea kasi ya maambukizi kwa kundi la vijana tutafanikiwa kwani tatizo bado linaonekana kuwa kubwa,” amesema.

Amesema kundi la vijana hasa wa kike lipo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya ya VVU, hivyo aliwataka wadau na jamii kwa jumla kuweka mkazo kudhibiti tabia zinazochochea maambukizi, vijana kujitambua na kujitathmini na kutunza maisha yao na waonaishi na maambukizi watumie dawa kwa usahihi.

Dk Mpango pia amesema tabia ya wanaume kutegemea majibu ya wake zao inachangia kuendeleza maambukizi, “wanaume wenzangu twende tukapime na nitoe shukrani Waziri Mkuu, nakuomba usichoke kutuhamasisha wanaume. Niwahamasishe wanaume wote tukitoka hapa tukapime.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema bado kuna idadi kubwa ya wanaume wanaotegemea majibu ya maambukizi ya VVU kutoka kwa wake zao akisema wanajidanganya.

Majaliwa amesema kuna umuhimu kwa wanaume kupima kwani, tafiti za Serikali kwa jumla zinaonesha wanaojitokeza ni wanawake na wanaume wameendelea kutegemea majibu ya wake zao.

“Wanaume wenzangu mpo hapa msiniangushe mimi ni balozi wenu nawawakilisha ninyi, nimeshapima na ninatoa wito kwa wanaume wote twende tukapime.

“Ipo tabia ya wanaume badala ya kufuatana na mkeo kwenda kupima, huendi akirudi yupo safi unajitutumua msijidanganye! Balozi wenu nawahamasisha kwenda kupima, baada ya tukio hili tuvunje rekodi tukajitokeze kupima kama ambavyo wanawake wanapima,” amesema Majaliwa.

Aidha, Majaliwa amesema kuna miradi kadhaa ya wasichana na kinamama wadogo nchini ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi mapya.

Mkurugenzi Tiba na Mafunzo Mradi wa Afya Hatua wa  Shirika la Tanzania Health promotion (THPS) Dk Fredrick Ndosi amesema kauli hiyo imewakumbusha wanaume kujenga tabia ya kupima afya zao na kuacha kutegemea majibu ya wake zao hasa kipindi cha ujauzito.

Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Songea (HOMSO) Dk Majura Magafu amesema mtu anapaswa kupima afya yake na kujua maendeleo yake kama ameambukizwa au la!  Na si kutegemea majibu ya mwenza wake.

Kibaiolojia kwa wenza wanaoishi pamoja mmoja anaweza kukutwa na maambukizi na mwingine kukutwa salama. Aliyekutwa salama alienda kupima mara kwa mara, mwenza wake naye ataamini yupo salama kwa kutumia majibu ya mwenzie hivyo kuendelea kumweka mwenza wake kwenye hatari ya maambukizi na anaendelea kuambukiza wengine.

“Kila mtu ana vinasaba vyake kibailojia, hivyo unaweza kuwa na mwenza aliyeambukizwa Virusi vya Ukimwi na akitumia majibu yako ataweza kukuambukiza pia,” amesema Dk Magafu.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema Serikali inatumia Sh400,000 kwa Mtanzania mwenye maambukizi ya VVU kila mwaka, sawa na Sh750 bilioni kwa Waviu milioni 1.7  katika kuhakikisha wanafubaza VVU nchini.

Amesema Ukimwi bado ni janga, akiiasa jamii kuacha ngono zembe na kwamba Serikali imeendelea kuona jukumu kubwa kugharamia matibabu.

“Gharama ni kubwa, tuna kila sababu kuzuia maambukizi mapya nchini na kuhakikisha walio katika dawa wanafubaza virusi kwa kutoa tiba stahiki na kuhakikisha waviu wote wanaendelea kufubaza VVU na wataendelea kulindwa katika uhai wao,” amesema Waziri Jenista Mhagama.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dk Christin Mzava amesema vifo vitokanavyo na Ukimwi, vitapunguzwa nchini, iwapo Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itaanza kutekelezwa.

“Matibabu yanatolewa bure lakini kuna magonjwa nyemelezi mtu mwingine hazuiwi kuwa nayo, bima kwa wote itawapa fursa wote waweze kuhudumiwa bila vikwazo vyovyote, itawawezesha kupima na kutibiwa magonjwa mengine bila kuwa na vikwazo vya fedha,” amesema Dk Mzava.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa maambukizi ya Ukimwi mwaka 2021 yaliua watu 25,000 na mwaka 2023 idadi hiyo ilipungua hadi vifo 22,000 kwa mwaka.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Jarome Kamwela amesema kwa kutambua rasilimali kutoka nje zinapungua, Serikali ilianza kufanya maandalizi mwaka 2015 kuanzisha mfuko wa ATF na imeendelea kutenga fedha kupitia mfuko huo.

Related Posts